KIPA wa Namungo FC, Beno Kakolanya amesema kuanza kwao vibaya mechi ya kwanza ya Ligi Kuu dhidi ya Tabora United iliyowafunga mabao 2-0, imewafungua macho kukaza buti.
Alisema Tabora United ilikuwa na kikosi cha wachezaji wazuri kama mshambuliaji Heritier Makambo, hivyo ushindani ulikuwa mkubwa ambao uliwapa wapinzani wao ushindi.
“Hakuna kitu kibaya kama kufungwa nyumbani, lakini imetuamsha kukaza buti zaidi. Msimu umeanza na kasi kubwa, inaonyesha jinsi Ligi Kuu itakavyokuwa ya ushindani,” alisema.
“Kwa sasa tunaweka nguvu dhidi ya Fountain Gate baada ya awali kuahirishwa mechi hiyo, kwani wachezaji wao walikuwa hawana vibali. Wapinzani wetu nao wamepoteza dhidi ya Simba kwa mabao 4-0, hivyo utakuwa mchezo mgumu.”
Kakolanya anakwenda kukutana na timu yake ya zamani (Fountain Gate), alisema kitu kinachotakiwa kwenye mchezo huo ni ushindi na siyo kupoteza.
“Hatutaki kung’ang’aniwa na gundu la kupoteza tena, ila tupate morali na kuambulia pointi iwe moja ama tatu,” alisema.