KAMATI YA BAJETI YA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR YAIPONGEZA NSSF KWA MAFANIKIO KATIKA UTENDAJI

Na MWANDISHI WETU,Dar es Salaam.

Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Mwanaasha Khamis Juma wameupongeza Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa mafanikio makubwa uliyopata katika utekelezaji wa majukumu yake ya msingi ambayo ni kuandikisha wanachama, kukusanya michango, kuwekeza na kulipa mafao.

Mhe. Mwanaasha ametoa pongezi hizo mwishoni mwa wiki wakati walipofanya ziara ya kikazi NSSF jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kujifunza utendaji kazi wa Mfuko ikiwemo matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma na hatua mbalimbali ambazo ilipitia tokea ulipoanzishwa mpaka sasa.

“Sisi kama Kamati ya Bajeti tunawashukuru sana NSSF na tumefaidika kwa namna moja ama nyingine, tumeona kwa upande wa uwekezaji tunawapongeza kwa kufikia hatua kubwa ya uwekezaji pamoja na matumizi ya TEHAMA,” amesema Mhe. Mwanaasha.

Mhe. Mwanaasha amesema NSSF imepiga hatua kubwa kiutendaji ikiwemo kufanya maboresho mbalimbali kama vile ya mifumo ya fedha, mifumo ya uandikishaji, ukusanyaji michango na ulipaji wa mafao.

Naye, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Dkt. Soud Nahodha Hassan amepongeza utaratibu mzima ambao NSSF inafanya hususan kwenye utekelezaji wa majukumu yake ya msingi jambo ambalo limechochea mafanikio.

Kwa upande wake, mjumbe wa kamati hiyo, Mhe. Asha Abdallah Juma ameeleza kufurahishwa kwake na kazi kubwa zinazofanywa na NSSF hasa katika ukusanyaji wa michango ya wanachama tokea ilipoanzishwa mpaka sasa.

Mhe. Suleiman Masoud Makame amepongeza mabadiliko mbalimbali yaliyofanywa na NSSF tokea ikiitwa NPF mpaka sasa na imepiga hatua kubwa ya kiutendaji.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba

amesema Mfuko umeboresha huduma zake kupitia mifumo ya TEHAMA kwa lengo la kurahisisha huduma kwa wanachama ili waweze kuzipata hukohuko waliko bila ya kulazimika kufika ofisi za NSSF.

Bw. Mshomba amesema maeneo mengine ambayo wameyaboresha ni ukaguzi, uwekezaji na utendaji kwa ujumla jambo ambalo limechagiza mafanikio ambapo kwa sasa thamani ya Mfuko imefikia trilioni 8.6.

Related Posts