Moshi. Wananchi wa Kijiji cha Korini Kusini, kata ya Mbokomu Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, wamelalamikia kero ya upatikanaji wa maji safi na salama.
Wamesema hali hiyo inawafanya wanunue ndoo moja ya maji kwa Sh500, gharama wanayosema hawawezi kuimudu kwa kuwa kipato chao ni kidogo.
Wanasema kero hiyo ya maji imedumu kwa muda mrefu bila kupatiwa suluhisho na wakati mwingine hulazimika kutumia maji ya mfereji ambayo si safi na salama kwa matumizi ya binadamu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana na leo Jumatano, Agosti 28, 2024, wananchi wa kijiji hicho wameiomba Serikali kuingilia kati suala la uhaba wa maji.
Elly Mrema mkazi wa kijiji hicho, amesema hali hiyo imewafanya kutumia sehemu kubwa ya fedha wanazoachiwa na waume zao kwa ajili ya matumizi ya nyumbani kununua maji, jambo ambalo limeongeza mzigo kwa familia.
“Hatuna maji. Wakati mwingine tunalazimika kununua maji kwa Sh500 kwa ndoo moja. Kwa mfano, unaachiwa Sh5,000 ya chakula cha familia, lakini Sh3,000 yote inatumika kununua maji. Yaani tunanyanyasika tunaiomba serikali itusaidie,” amesema Mrema.
Mkazi mwingine, Oscar Moshi wa kijiji hicho, amesema; “Mwezi wa sita mabomba yalisombwa na mafuriko wakasema watafuatilia baada ya mvua kukatika, lakini kila ukiuliza wanasema wanafuatilia na hakuna kinachofanyika.”
Akizungumzia kadhia hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Moshi (Muwasa), Kija Limbe amesema tatizo hilo linatokana na miundombinu ya maji kusombwa na mafuriko.
Hata hivyo, amesema mamlaka inaendelea na kazi ya kuirejesha kusudi wananchi wapate huduma ya maji safi na salama.
“Mradi wa Mbokomu uliharibiwa sana na mafuriko na zaidi ya Sh100 milioni zilihitajika kuirejesha miundombinu hiyo. Tayari tumenunua mabomba na tunatarajia mwishoni mwa mwezi huu wa Agosti au mwanzoni mwa Septemba tutakamilisha mradi huo,” amesema mkurugenzi huyo.
Wakati Muwasa wakitoa majibu hayo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbokomu, Emmanuel Mrema amesema tatizo la maji ni changamoto kubwa inayowakera wananchi wake.
Ameiomba Serikali kuongeza nguvu katika kurejesha miundombinu iliyoharibiwa na mafuriko haraka.
“Moja ya mambo yanayowakera wananchi ni suala la maji. Mwezi wa tano kulitokea mafuriko makubwa ambayo yaliharibu chanzo cha maji na tangu wakati huo hali hapa kijijini ni mbaya sana,” amesema Mrema huku akiiomba Serikali kuu kuongeza juhudi za kurejesha vyanzo vya maji vilivyoharibiwa na mafuriko.