Kesi ya Mpina, Mawaziri na taasisi nyingine kusikilizwa Septemba 18

Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Masjala ya Dar es Salaam, imepanga Septemba 18, 2024 kuanza kusikiliza kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhanga Mpina, dhidi ya Waziri wa Kilimo na Waziri wa Fedha pamoja na taasisi nyingine saba zikiwemo kampuni.

Tarehe hiyo imepangwa leo Jumatano, Agosti 28, 2024 na Jaji Anold Kirekiano, wakati kesi hiyo ilipotajwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza tangu ilipofunguliwa.

Kesi hiyo ya kikatiba namba 18383 ya mwaka 2024 imefunguliwa na Mpina, akipinga uamuzi wa Waziri wa Kilimo kutoa vibali vya ununuzi wa sukari kupitia Bodi ya Sukari kwa kampuni ambazo hazimiliki viwanda vya sukari wala sukari.

Pia, anapinga Waziri wa Fedha kuruhusu Kamisha wa Mamlaka ya Mapato (TRA) kuamuru kampuni za vocha kuingiza sukari nchini bila kulipa kodi na kupelekea Serikali kupoteza mapato ya zaidi ya Sh1.548 bilioni.

Mpina pia, ameshtaki kampuni za sukari kwa kukubali kuingiza sukari na kukubali kupewa msamaha wa kodi.

Mbali na mawaziri hao, wajibu maombi wengine ni Bodi ya Sukari, Kampuni ya Itel East Africa Limited na Zenj General Merchandize,  Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Leo kesi hiyo ilipotajwa Mpina waliwakilishwa na jopo la mawakili mawakili sita wakiongoza na Dk Rugemeleza Nshala, Rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS). Wengine ni  John Seka ambaye pia mi rais mstaafu wa TLS, rais wa sasa wa TLS, Boniface Mwabukusi, Ferdinand Makore na Edson Kilatu.

Kwa upande wa wajibu maombi ambao ni Mawaziri na taasisi za Serikali waliwakilishwa na jumla ya mawakili watano wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Hangi Chang’a.

Chang’a amedai kuwa walipewa nyaraka za kesi hiyo Agosti 21, 2024 badala ya Agosti 6, 2024 kama amri ya mahakama ilivyokuwa imeeleza.

Hivyo amedai kuwa kwa kuwa sheria inaelekeza wadaiwa wanatakiwa kujibu ndani ya siku 14, hivyo bado wana muda hadi Septemba 4, kujibu na kuwasilisha kiapo kinzani.

Baada ya maelezo hayo Jaji Kirekiano amehoji sababu za upande  mdai kuchelewa kuwapa nyaraka hizo.

Akijibu swali hilo, Dk Nshala amedai kuwa mdaiwa  namba tatu hawakuweza kumpata hivyo hawakuweza kumpatia nyaraka hizo, na kwamba mdaiwa namba 4 na 5 wao walipatiwa nyaraka, lakini hawakufika mahakamani hapo.

Dk Nshala amedai kuwa walichelewa kuwapatia nyaraka hizo kwa sababu waliongeza muda wa kuwasilisha nyaraka hizo.

Kutokana na hali hiyo Jaji Kirekiano alielekeza mdai kumpatia nyaraka mdaiwa namba tatu ambaye hapo awali walishindwa kupamta na pia anatakiwa kupeleka kiapo cha uthibitisho kama wamewapa hizo hati za madai.

Baada ya kueleza hayo, Jaji Kirekiano aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 18, 2024 saa nane mchana kwa ajili ta usikilizwaji.

Mpina alikuwepo mahakamani hapo wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Related Posts