Kesi ya Mpina, Wizara ya Kilimo na taasisi nyingine kusikilizwa Septemba 18

Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Masjala ya Dar es Salaam, imepanga Septemba 18, 2024 kuanza kusikiliza kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhanga Mpina, dhidi ya Wizara ya Kilimo na taasisi nyingine saba zikiwemo kampuni.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumatano, Agosti 28, 2024 na Jaji Anold Kirekiano, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa kwa mara ya kwanza tangu ilipofunguliwa.

Kesi hiyo ya kikatiba namba 18383 ya mwaka 2024 imefunguliwa na Mpina, akipinga uamuzi wa Waziri wa Kilimo kutoa vibali vya ununuzi wa sukari kupitia Bodi ya Sukari kwa kampuni ambazo hazimiliki viwanda vya sukari wala sukari.

Pia, anapinga Waziri wa Fedha kuruhusu Kamisha wa Mamlaka ya Mapato (TRA) kuamuru kampuni za vocha kuingiza sukari nchini bila kulipa kodi na kupelekea Serikali kupoteza mapato ya zaidi ya Sh1.548 bilioni.

Mpina pia, ameshtaki kampuni za sukari kwa kukubali kuingiza sukari na kukubali kupewa msamaha wa kodi.

Mbali na Wizara ya Kilimo, wajibu maombi wengine ni Bodi ya Sukari, Kampuni ya Itel East Africa Limited na Zenj General Merchandize.

Nyingine ni Wizara ya Fedha, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Shauri hilo lilipangwa leo kwa ajili ya kutajwa na waleta maombi waliwasilishwa na mawakili sita wakiongoza na kiongozi wa jopo hilo, Dk Rugemeleza Nshala akishirikiana na John Seka, Boniface Mwabukusi, Ferdinand Makore na Edson Kilatu.

Kwa upande wa wajibu maombi ambao ni taasisi za Serikali wao waliwakilishwa na jumla ya mawakili watano wakiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Hangi Chang’a.

Katika kesi hiyo, Chang’a amedai shauri hilo limeitwa kwa ajili ya kutajwa na wao walipewa nyaraka hizo Agosti 21, 2024 badala ya Agosti 6, 2024 kama amri ya mahakama ilivyokuwa imeeleza.

Changa amedai kwa kuwa sheria inaelekeza wajibu maombi wanatakiwa kujibu ndani ya siku 14, hivyo bado wana muda hadi Septemba 4, kujibu na kuwasilisha kiapo kinzani.

Baada ya maelezo hayo Jaji Kirekiano amehoji sababu za waleta maombi kuchelewa kuwapa nyaraka hizo.

Akijibu swali hilo, Dk Nshala amedai kuwa mjibu maombi namba tatu hawakuweza kumpata hivyo hawakuweza kumpatia nyaraka hizo.

Kwa upande wa mjibu maombi namba 4 na 5 wao walipatiwa nyaraka, lakini hawakufika mahakamani hapo.

Dk Nshala amedai sababu ilisababisha mpaka wakachelewa kuwapatia nyaraka hizo ni kwa sababu waliongeza muda wa kuwasilisha nyaraka hizo.

Kutokana na hali hiyo Jaji Kirekiano alielekeza waleta maombi kumpatia nyaraka mjibu maombi namba tatu ambaye hapo awali walishindwa kupamta.

Pia, waleta maombi wanatakiwa kupeleka kiapo cha udhibitisho kama wamewapa hizo hati za madai.

Baada ya kueleza hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 18, 2024 saa nane mchana kwa ajili ta usikilizwaji.

Hata hivyo, mleta maombi katika shauri hilo Mpina alikuwepo mahakamani hapo wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Related Posts