Maestro: Azam FC tatizo kila msimu ina timu mpya

Mchezaji wa zamani na mchambuzi wa soka, Ibrahim Masoud ‘Maestro’ amesema kutolewa kwa timu za Zanzibar za JKU na Uhamiaji kunatokana na ubora mdogo wa wachezaji, wakati Azam wao wakisumbuliwa na kukosa muunganiko.

Maestro, aliyewahi kuichezea KMKM ya Zanzibar amesema timu za visiwani humo zina tatizo la ubora mdogo wa wachezaji tofauti na zamani ambako kulikuwa na wachezaji wenye ubora mkubwa.

Maestro amesema timu hizo hazitakiwi kuwekwa daraja moja na klabu kongwe za Simba na Yanga ambazo zimejitengenezea dunia tofauti ya ubora, unaozibeba timu hizo.

Akizungumzia upande wa Azam, Maestro amesema timu hiyo licha ya kuwa na wachezaji bora inateswa na mabadiliko ya mara kwa mara ya wachezaji ambao umeifanya kukosa mafanikio.

Mchambuzi huyo ambaye alikuwa anacheza nafasi ya kiungo amesema mafanikio ya timu yanahitaji ubora wa wachezaji na muunganiko wa nyota wa timu husika na Azam licha ya kuwa na wachezaji wenye ubora wanakosa muunganiko wa wachezaji kutokana na kubadili wachezaji kila msimu.

“Tangu walipofungwa na Yanga (4-1) kwenye fainali ya Ngao ya Jamii, unaweza kuona wachezaji wa Azam wanacheza taratibu sana. Hawaupeleki mpira kwa haraka. Ilikuwa hivyo hata walipocheza mechi ya kwanza dhidi ya APR na hata ya pili waliyotolewa katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa. Inashangaza kuona timu hiyo ambayo ni wawakilishi wa nchi kwenye michuano ya Afrika wanacheza na JKT Tanzania leo hadi wakati wa mapumziko hawana shuti hata moja lililolenga lango,” amesema.

Amesema timu hiyo inatakiwa kutafuta dawa ya tatizo hilo huku kuangalia utulivu wa benchi la ufundi ambalo bado limekosa kueleweka kwa makocha walionao wengine kukosa sifa.

OSIAH: HAKUNA SABABU YA KWENDA MISRI

Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Angetile Osiah amesema kushindwa kupata nafasi ya kucheza michezo ya ushindani kabla ya kuanza kwa michezo ya kimataifa ni kati ya sababu zilizozifanya timu nne za Tanzania kutolewa mapema katika michuano hiyo ya kimataifa.

Osiah alitolea mfano Misri ambako kipindi kama hiki ligi yao imechanganya hivyo ni ngumu kushindana nao wakati huku ndio kwanza timu zipo kwenye maandalizi ya msimu mpya kama ilivyokuwa kwa Yanga na Azam ambazo zimeanzia katika raundi ya kwanza ya michuano hiyo.

“Yanga haijacheza mechi yoyote ya Ligi kabla ya kupambana na Vital’O, Azam nayo haikucheza mechi yoyote ya ligi, Simba nayo ingeanzia katika raundi ya kwanza nayo ingekuwa hivyo hivyo, nadhani hata kwa timu za Zanzibar, kalenda ilivyobadilika na sisi tunatakiwa kubadilika, Azam imesajili wachezaji wazuri lakini imepata wapi nafasi ya kujaribu hiyo timu kimashindano?” amesema Osiah.

“Timu inaenda kambini Misri, inahitaji siku mbili hadi nne za kusafiri, unapata wapi muda wa kukaa na wachezaji wako kwa ajili ya maandalizi ya msimu. Ni bora kubaki hapa ukakaa na wachezaji wako ukapata muda sahihi wa kujiandaa,” amesema Angetile ambaye pia mwanahabari nguli nchini.

“Ishu sio uwekezaji. Kama kuwekeza Azam ndio timu ambayo imewekeza pengine kuliko timu yoyote hapa Tanzania, lakini bado imefeli. Ishu ni muda wa maandalizi na maandalizi sahihi.”

Osiah ameyabainisha hayo leo, Agosti 28, 2024 wakati akichangia mjadala kwenye Mwananchi Space unaoandaliwa na Mwananchi Communications Limited (MCL) wenye mada isemayo; Tumekosea wapi timu nne za Tanzania kutolewa mashindano ya klabu Afrika? 

BABI: TFF IWAANGALIE VIONGOZI WA KLABU WANAOKOSA SIFA

Kiungo wa zamani wa Yanga, Mlandege ya Zanzibar, Abdi Kassim ‘Babi’ amesema mbali na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na wenzao wa Zanzibar (ZFF) kuwaangalia makocha na wachezaji wenye sifa pia wanatakiwa kuwamulika viongozi wa klabu za soka hapa nchini.

Gwiji huyo aliyefahamika pia kwa jina la ‘Ballack wa Zanzibar’ amesema katika uchunguzi wake amebaini pia zipo baadhi ya klabu ambazo zinaongozwa na viongozi wa soka wanaokosa sifa zitakazosaidia kunyoosha mambo ya kiutawala.

Babi, nahodha wa zamani wa Taifa Stars na Zanzibar Heroes, ambaye ndiye mchezaji wa kwanza kufunga bao kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ulipomalizika kujengwa 2007, amesema ni wakati wa TFF na ZFF kuanza kuwaangalia na viongozi hao, ambao ndio wanashindwa kuzisaidia klabu zao kupiga hatua kwenye mashindano makubwa.

GAMBO JR: AZAM IKAOMBE MSAHAMA ILIKOKOSEA

MDAU wa soka nchini, Hosea Gambo Paul ‘Gambo Jr’ amesema kama kuna sehemu Azam FC ilikosea ni vyema ikaenda kuomba msamaha kutokana na kushindwa kufanya vyema katika michuano ya kimataifa, kwani ni klabu iliyokamilika kwa kila kitu.

Amesema kutolewa kwa JKU na Uhamiaji inaweza kuwa na mashiko, lakini kwa Azam FC inashangaza kwani ina kila kitu kuanzia benchi la ufundi na wachezaji, huku akisema kwa Coastal Union iliyotolewa Kombe la Shirikisho inatokana na kuangushwa na uzoefu na kupoteza ugenini kwa mabao 3-0.

“Coastal ina matatizo mengi ina mizozo na wachezaji wake, lakini kwa hawa Azam kama kuna sehemu walikosea ni vyema wakaenda kuomba radhi kwa hali inayowakuta,” amesema Gambo Jr.

KANYAMA: KLABU ZINAHITAJI WATU WA SAIKOLOJIA

Mdau wa soka nchini, Mbaruku Kanyama amesema, shida kubwa inazozikumba klabu zetu ni kuona waongeleaji ni wengi na sio watendaji, huku akigusia changamoto hii ni katika sekta zote lakini akisisitiza umuhimu wa klabu kuwa na wanasaikolojia wa kusaidia wachezaji.

“Mpira ni Sayansi na sio sanaa, kuna vitu vingi vya kuvifanyia kazi ili tupate matokeo mazuri, Azam FC ni mfano mzuri kwa sababu ina uwekezaji mzuri ila imekuwa ikipitia wakati mgumu, tunapaswa kuandaa kuanzia jopo la ufundi  na sio benchi la ufundi tu,” amesema Kanyama.

Kanyama aliongeza, ili klabu zetu zifanye vizuri zinapaswa kuongeza uimara katika watu wa saikolojia kwani wachezaji wanapitia changamoto nyingi za kimaisha hivyo, itakuwa ni chachu ya wao kupata muda mzuri wa kujiandaa kifikra.”

Klabu za Azam, Coastal Union, JKU na Uhamiaji ni kati ya timu nne zilizong’olewa mapema CAF baada ya kuchemsha mechi za raundi ya awali na kuziacha Simba na Yanga zikiendelea kupeperusha bendera.

Yanga inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika imepangwa kukutana na CBE ya Ethiopia baada ya kuitoa Vital’O ya Burundi kwa jumla ya mabao 10-0, huku Simba ikiwa imeanzia hatua hiyo katika Kombe la Shirikisho ikitarajiwa kupambana na Al Ahli Tripoli ya Libya iliyoitoa Uhamiaji kwa jumla ya mabao 5-1.

MUKULU: TIMU ZETU ZIMEKOSEA KATIKA MAANDALIZI

Mchambuzi wa soka, Lilian John Mukulu amesema moja ya sababu zinazozifelisha timu za Tanzania kimataifa ni aina ya maandalizi yanayofanyika.

Amesema Coastal Union kutolewa mapema haijamshangaza sana kutokana na ugeni wao katika michuano hiyo, lakini Azam hawakuwa wamefanya maandalizi ya kutosha katika kuwasoma wapinzani wao APR ambao walikuwa hapa nchi kwa muda mrefu wakishiriki michuano ya Kagame.

“Tumeona APR walikuja katika michuano ya Kagame, Azam ilikuwa na nafasi nzuri ya kuwasoma sidhani kama walifanikiwa katika hilo, lakini pia wameenda ugenini wakiwa na mtaji wa bao 1-0 cha kushangaza wakaanza kujilinda mwanzo mwisho wakapoteza,” amesema Lilian.

“Kwa sasa wanapaswa kurudi kujiuliza wapi wanakosea, lakini lazima tuangalie maandalizi yanayofanyika yanakidhi michuano tunayokwenda kushiriki?”

MAENDAENDA: TUNAFELI KWA KUTOJIFUNZA KWA WENGINE

Mdau wa soka nchini, Timotheo Philipo ‘Maendaenda’ amesema tunapaswa kuondoa hoja ya hakuna anayekosea, kwani mpira ni mchezo wa mbinu za ndani na nje ya uwanja kuanzia uwekezaji kwenye klabu kutokana na malengo ambayo zimejiwekea kwa msimu, huku akibainisha klabu nyingi zinakwama kwa kutopenda kujifunza kwa klabu za mataifa mengine.

“Usajili wa Azam wangefanya mwanzoni mwa msimu naamini wangefanya vizuri, wana wachezaji bora lakini sio kwa wakati sahihi kwa sababu ndio inatakiwa kujipanga, kwani ukiangalia malengo ya usajili yanapaswa kuambatana na msimu husika.”

Maendaenda ameongeza, timu nyingi zinafeli michuano hiyo mikubwa Afrika kwa sababu hazitaki kujifunza na kuangalia wengine wanafanya nini.

“Kwa mfano timu kama Simba kuna mtu wa skauti ambaye anasaidia kwa kiasi kikubwa katika kupendekeza wachezaji, hii unaweza kuona jambo dogo ila ni kubwa mno, ni lazima timu nyingine zijifunze kwa waliofanikiwa ili zifanye vizuri,” amesema Maendaenda.

Maendaenda amewataka pia, wadau mbalimbali wa soka nchini kuzisaidia Coastal Union, JKU na Uhamiaji katika suala la kiuchumi na sio kuwalipa ‘Goli la Mama’, kwani hii itazisaidia kujiandaa vizuri katika mashindano hayo makubwa Afrika.

Klabu za JKU na Azam ziling’olewa Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati Uhamiaji na Coastal zimetolewa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya awali na kuviacha vigogo Simba na Yanga zikiendelea katika raundi ya pili ya michuano hiyo ya Afrika. Simba ilianzia raundi hiyo na itakutana na Al Ahli Tripoli ya Libya iliyoing’oa katika Kombe la Shirikisho, wakati Yanga itakutana na CBE ya Ethiopia baada ya kuitoa Vital’O ya Burundi kwa jumla ya mabao 10-0.

MASANJA: TATIZO NI UWEKEZAJI

MDAU wa michezo Masanja Ngwau, ameeleza tatizo kubwa lililozikumba timu nne zilizotolewa mapema kwenye mashindano ya Afrika kwa klabu ni uwezekezaji duni.

Masanja amesema klabu za Zanzibar na hata ile moja nje ya Azam, zimekumbana na kutolewa raundi ya awali kutokana na kukosa maandalizi mazuri ya mashindano hayo na kujikuta zinatolewa mapema.

Masanja amesema wadau wa michezo hususani kampuni mbalimbali zinatakiwa kujitokeza kuzisaidia klabu nyingine ambazo zina uchumi wa kati.

Hata hivyo, Masanja hakumalizia vizuri mchango wake baada ya mawasiliano yake kukatika akiwa hewani.

MWITA: AZAM IONGEZE MASHABIKI IPATE PRESHA YA MATOKEO

Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Awadh Maulid Mwita amewataka Azam FC kuongeza wigo wa mashabiki wa timu yao ili ipate presha ya kusaka matokeo chanya kwenye mechi zao.

Mwita amesema Azam FC ina karibu kila kitu katika timu hiyo kinachohitajika ili iweze kuwa timu bora, lakini imeshindwa kufanya vizuri kutokana na wachezaji wake kukosa presha ya kutakiwa kufanya vizuri.

Mwita amesema klabu zingine za Simba na Yanga zinakutana na presha kubwa ya mashabiki wao pale wanapokosa matokeo mazuri hatua ambayo inawafanya viongozi na wachezaji kujituma na kupata matokeo mazuri.

“Hata kwa vyombo vya habari visaidie katika hili, kwa mfano anavyokoselewa Fei Salum kwa Azam kutolewa raundi ya awali, ni tofauti na atakavyokosolewa Clatous Chama, kutokana na presha ya mashabiki,” amesema Mwita.

Akizungumzia timu za Zanzibar ambazo nazo zimetolewa mapema zikiwamo JKU na Uhamiaji, Mwita amesema tatizo linalozikwamisha timu hizo ni ukosefu wa fedha ambapo ametaka wawekezaji kuendelea kujitokeza kuokoa jahazi.

RAMADHAN: BADO HATUJAWA TAYARI KIMATAIFA

Ramadhan Elias ambaye ni mdau wa michezo, amesema ishu kubwa ambayo inazitesa timu za Tanzania katika michuano ya kimataifa ni kutokuwa tayari.

Mdau huyo amesema ukiangalia timu nne za Tanzania Bara ambazo zimekuwa zikipata nafasi ya uwakilishi wa nchi kimataifa zimekuwa zikienda kutokana na kanuni inavyotaka, lakini hazipo tayari kwa mashindano hayo.

Akitolea mfano wa wawakilishi waliowahi kutolewa mapema, ameitaja KMC ambayo ilipopata nafasi hiyo haikutoboa wakati Biashara United ilishindwa hadi kusafiri kwenda kucheza mchezo wa marudiano ugenini.

“Tuliopia hata kwa Geita Gold, ambayo ilitolewa hatua kama hiyo na safai hii imekuwa kwa Azam na Coastal Union, mbali na JKU na Uhamiaji,” amesema Elias.

Ameongeza kwamba kwa kuwa Tanzania Bara ina nafasi ya kupeleka timu nne kimataifa, mbali na Simba na Yanga, timu zingine zimekuwa zikipambana angalau zimalize nafasi nne za juu kwenye msimamo wa ligi ili kuona namna ya kupata nafasi hiyo, tukitofautiana na klabu za nchi za Morocco au Misri.

Ushauri wake ni kwamba, timu zilizobaki Simba na Yanga ziendelee kupambania Tanzania kubakisha wawakilishi wanne, kisha wengine wajifunze lakini pia wadhamini wanapaswa kujitokeza kwa wingi.

NGALE: AZAM, COASTAL HAZIEPUKI LAWAMA CAF

Mchambuzi wa soka nchini, Salama Ngale amesema, klabu za Azam na Coastal Union haziepukiki lawama kwa kutolewa mapema katika michuano ya kimataifa kutokana na kutojua vyema kutumia viwanja vya nyumbani.

“Timu ni lazima iangalie malengo yake ni yapi, kwa mfano ukiangalia Azam inahukumiwa kwa sababu ya matokeo yake ya kutoridhisha nyumbani, Coastal ilipata faida ya kuanzia ugenini, lakini ilipoteza mabao 3-0, ambayo ni mengi japo iliporudi nyumbani utakumbuka ilipata penalti dakika ya tano tu na ikakosa,” amesema Salama.

Ameongeza, timu inapoenda katika mashindano hayo ni lazima iangalie malengo iliyojiwekea kwani kitendo cha miamba hiyo kutolewa mapema sio kigezo cha kuepuka lawama, kwani zipo klabu ambazo zimefanya makubwa ambayo hayakutarajiwa.

“Tumeshuhudia matokeo ya kuchukiza sana kwa mfano UD Songo na Simba na Jwaneng Galaxy na Simba pia, timu ikijipanga na kutambua malengo yake inaweza kupata kile ilichokikusudia, hivyo Azam na Coastal Union haziepuki lawama,” amesema Salama.

Salama ameyabainisha hayo leo Agosti 28, 2024 wakati akichangia mada katika Mwananchi Space, inayoandaliwa na Mwananchi Communications Limited (MCL) yenye mada isemayo; Tumekosea wapi timu nne za Tanzania kutolewa mashindano ya klabu Afrika?

Related Posts