Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amesema mgawanyiko na migogoro inayoendelea kufukuta kwenye vyama vya upinzani ikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ni turufu ya chama hicho kupata ushindi wa heshima katika uchaguzi ujao.
Amesema utabiri huo anaona utaanza kutimia kuanzia kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika kuanzia Novemba 27, 2024 na kuwataka wananchi kuendelea kuwa na imani, kwani ari ya kuendelea kuwapa maendeleo bado wanayo.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, amekanusha taarifa za chama chao kuwa na migogoro huku akitupa dongo kwa CCM kuwa hakukaliki.
“CCM wana mvutano mkubwa ndiyo maana unaona nafasi ya Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara haijazibwa hadi sasa. Ni mgogoro mkubwa kiongozi yule mwenye busara zake akaona ajiweke pembeni,” amesema Mrema
Akimjibu kuhusu CCM kupata ushindi wa heshima, Mrema amesema kwa kauli hiyo wanathibitisha ukweli katika uchaguzi uliopita hawakushinda kwa haki.
“Tumejipanga uchaguzi ujao kuanzia wa serikali za mitaa hautakuwa rahisi hatuwezi kukubali waibe kura tunatoa elimu kwa wananchi walinde kura wenyewe vituoni wajaribu wataona,” amesema Mrema.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara alioufanya jana Agosti 27, 2024 Kata ya Tungi Wilaya ya Kigamboni, akiwa kwenye mwendelezo wa kumalizia ziara yake aliyoanza Juni mwaka huu kwa majimbo matatu ya Uchaguzi kati ya 10 ya mkoa wa Dar es Salaam, Makalla amesema kutokana na mivutano hiyo CCM kwa sasa kimeimarika kuliko jana.
“Chadema wamegawanyika wale viongozi wakubwa kila mmoja ana upande wake, CCM tunashangilia kwakuwa tunajiona tunaenda kushinda uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kishindo na tunataka kushinda kwa heshima kuanzia asilimia 99.8,” amesema
Amesema chama hicho hakina hiyana pamoja na migawanyiko yao kitaendelea kuvisaidia vyama vya upinzania ili kuendelea kuziishi 4R zilizoasisiwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
“Tutaendelea kusaidia, kuvumiliana.Binafsi nafurahi tumekuwa tukiwachangia fedha wanapoonekana wana matatizo mfano tulifanya harambee ya kumchangia Tundu Lissu na tulimchangia Sh5 milioni na tunamwambia kama matengenezo ni magumu atuambie tumnunulie gari lingine mpya,” amesema
Makalla ambaye ni mlezi kichama katika Mkoa wa Dar es Salaam, amesema chadema kimekuwa chama cha matukio kwa kuvizia jambo gani limetokea.
“CCM itatumia udhaifu huo wa migogoro ya vyama kupata ushindi wa kishindo, lakini sababu nyingine ya kushinda tumeendelea kupata wanachama kutoka upinzani na unatuimarisha zaidi,” amesema
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameeleza changamoto zinazowasumbua wakazi wa kigamboni ikiwemo ubovu wa barabara ya Kibada Mwasonga.
“Barabara hii ina urefu wa kilomita 40 na mkataba umeshasainiwa lakini tatizo linalokwamisha ni kumlipa ‘Advance payment’ (malipo ya awali) mkandarasi ili aanze kazi nilishaongea na Serikali tunachosubiri malipo,” amesema Chalamila
Chalamila ameeleza mafuriko na maji kujaa kwenye makazi ya watu yanayotokana na barabara nyingi kujengwa bila mifereji ni tatizo lingine linalowasumbua wakazi wa eneo hilo.