Makambo aongeza mzuka Tabora United

UWEPO wa mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Heritier Makambo ndani ya kikosi cha Tabora United, umeonekana kuwafurahisha mashabiki wa timu hiyo.

Mashabiki hao wamesema Makambo ameongeza staili ya tatu ya kushangilia kutoka mbili walizozizoea.

Tambo hizo zinakuja ikiwa ni siku chache baada ya timu yao kuichakaza Namungo mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa wikendi iliyopita katika Uwanja wa Majaliwa, Lindi baada ya mchezo wa kwanza kuchapwa 3-0 na Simba.

Akizumgumza na Mwanaspoti, Said Mgeleka, mmoja wa  mashabiki hao walisema Makambo ameamsha ari kikosini.

“Makambo ile staili yake ya kushangilia kwa kuwajaza imetuongezea na kuwa ya tatu ukiachilia mbali na ya kushangilia kama nyuki, kushangilia kama tumbaku na sasa kuwajaza hivyo kwa kikosi kilivyo naamini hatutakamatika,” alisema

Jafari Kishoka, alisema Tabora United ya msimu huu ni moto tofauti na misimu mingine kutokana na usajili uliofanyika.

“Baada ya kutazama hizi mechi mbili nimegundua tuna timu tofauti na misimu mingine maana nimeangalia safu ya ulinzi iko imara, kiungo tumekamilika na ushambuliaji ndio usiseme.” alisema

Rashid Fondogolo ambaye ni mwenyekiti wa mashabiki wa Tabora United alisema wanaandaa mapokezi bab’kubwa kwa timu baada ya kutoonekana muda mrefu mjini hapa.

Tabora United imefanikiwa kuwasajili baadhi ya nyota ambao wamewahi kucheza Ligi Kuu Bara wakiwamo Yacouba Sogne, Makambo, Salum Chuku na wengine ambao wameifanya timu hiyo hiyo, baada ya msimu uliopita kuponea chupuchupu kushuka.

Related Posts