Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ni miongoni mwa watu waliojitokeza kusikiliza shauri la viongozi wa Baraza la Vijana wa Chadema Wilaya ya Temeke wanaodaiwa kuweka kizuizini mahali kusikojulikana.
Viongozi hao wa Bavicha ni Mwenyekiti wa Wilaya ya Temeke, Deusdedith Soka na Katibu wake, Jacob Mlay pamoja dereva wao wa pikipiki, Frank Mbise, ambao wanadaiwa kukamatwa na Polisj katika kituo cha Polisi Chang’ombe, Temeke tangu Agosti 18, 2024.
Mpaka leo Jumatano, Agosti 28, 2024 ni siku 10 zimepita hawajafikishwa mahakamani na wazazi na ndugu zao hawajui mahali waliko, huku ikielezwa wamefuatilia kuulizia katika vituo mbalimbali vya Polisi Temeke ikiwemo Chang’ombe na vinginevyo jijini Dar es Salaam bila mafanikio.
Kutokana na hali hiyo kupitia, jopo la mawakili linaloongozwa na Wakili Peter Madeleka wamefungua shauri la maombi Mahakama Kuu Dar es Salaam dhidi ya viongozi wakuu wa Jeshi la Polisi na wa Temeke, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Katika shauri hilo linalosikilizwa na Jaji Wilfred Dyansobera, wanaomba wajibu maombi hao wajieleze kwanini wanawashikilia kizuizini isivyo halali na Mahakama itoe amri ya kuwaachilia huru.
Shauri hilo lilitajwa jana Jumanne, Agosti 27, 2024 na mawakili wao wakaiomba Mahakama kabla ya kuanza kusikiliza shauri hilo itoe amri ya kuwaachia kwa dhamana au iamuru wafikishwe mahakamani ili wakati shauri lao linasikilizwa nao waweze kusikia.
Mawakili wa Serikali Monica Ndakidemi na Cuthbert Mbilinyi walipinga maombi hayo wakidai mawakili hao hawana uhakika na hawajawasilisha ushahidi kuwa waombaji hao wanashikiliwa na Jeshi la Polisi.
Jaji Dyansobera baada ya kusikiliza hoja za pande zote aliahirisha shauri hilo mpaka leo Jumatano kwa ajili ya kutoa uamuzi wa maombi ya mawakili wao ya kuwapa dhamana au kuamuru wafikishwe mahakamani.
Ndani ya ukumbi wa wazi namba 01 hapa mahakamani watu mbalimbali wamejotokeza kusikiliza uamuzi huo na kile kitakachoendelea, wakiwemo viongozi wa Chadema wakiongozwa na Mbowe, wanachama, wazazi wa viongozi hao wanashikiliwa na ndugu jamaa na marafiki.
Kwa sasa (saa 5:50 asubuhi) umati unaendelea kumsubiri Jaji Dyansobera aingie mahakamani kwa ajili ya kutoa uamuzi huo pamoja na maelekezo mengine ya mahakama.
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa mbalimbali