Mbunge ang’aka kamatakamata ya RC na DC, Spika apigilia msumari

Dodoma. Licha ya hoja iliyowasilishwa na Mbunge wa Mlimba (CCM), Godwin Kunambi kutaka Bunge lijadili kwa dharura vitendo vya baadhi ya wakuu wa mikoa (RC) na wilaya (DC) kukamata wananchi kupata maelekezo mengine, Spika Tulia Ackson ametafakari kuiangalia upya sheria hiyo.

Suala hilo lilizungumziwa pia na Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai Tanzania kuwa sheria hiyo inafaa kuangaliwa upya.

Leo Jumatano, Agosti 28, 2024, Kunambi ametumia kanuni ya 54 kuliomba Bunge lisimamishe shughuli zake na kujadili kwa dharura vitendo vya baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya kutumia mamlaka hayo kuweka ndani watu, hata bila sababu za msingi.

Amesema viongozi wanne na wananchi 11 wamewekwa ndani kwa amri ya mkuu wa wilaya ya Kilombero.

Licha ya Kunambi kutomtaja kiongozi husika, lakini viongozi waliopo kwenye nafasi hizo kwa sasa ni Dunstan Kyobya ambaye ni DC wa Kilombero na Adam Malima RC wa Morogoro.

Hoja ya Kunambi si ya kwanza kujadiliwa ndani ya Bunge, imekuwa ikijitokeza hadi nje ya Bunge na kujadiliwa maeneo mbalimbali, ikiwemo mitandaoni kuwa mamlaka hayo hayatumiki ipasavyo.

Hata hivyo, akijibu hoja ya Kunambi Spika Tulia ametumia kanuni ya 55 inayotoa masharti ya jambo linalotakiwa kujadiliwa kwa dharura, kwamba madai ya wakuu wa mikoa, wilaya na hata baaadhi ya mawaziri kuagiza vyombo vya dola kukamata watu vimekuwepo siku zote.

Spika ametoa maelekezo kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwamba waangalie madai ya mbunge kwa kufuatilia kilichotokea na apewe taarifa ili na yeye awataarifu wananchi wake.

Hata hivyo, Spika amesema sheria hiyo ilitungwa na Bunge kwa dhamira njema kwa kuona hatari kwa mtu au jamii na kwamba mtu anaweza kuwekwa ndani kwa kunusuru maisha yake kwa wananchi wenye hasira au kama anahatarisha maisha ya wananchi na si vinginevyo.

“Pungufu ya hapo, kwa kweli hili alilolieza mbunge (Kunambi) itabidi pengine ile sheria sasa sisi kama Bunge tuitazame upya kama inaleta changamoto kwenye utekelezaji wake.

“Nia ya hii sheria haikuwa mtu kuonyesha nguvu aliyonayo ya kuagiza polisi kamata huyu, hapana. Nia yake ilikuwa ni hiyo ambayo nimeshaieleza sina haja ya kuirejea.

“Kama hicho sicho kinachofanyika basi kuna haja ya kuitazama upya sheria hii ili kuondoa huo mkanganyiko wa viongozi kuanza kuogopwa sasa na wananchi, maana kila wakati watakuwa wanaagiza huyu akamatwe, huyu awekwe ndani na mambo kama hayo,” amesema.

Spika Tulia ameongeza: “Tumeshaona haya yakitokea hata kwa mtu ambaye hana mamlaka kabisa, yaani kwenye sheria hajatajwa na yeye anasema kamata weka ndani, sasa hii haiwezekani, haiwezekani.”

 Amemwelekeza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwamba wafuatilie hoja ya mbunge (Kunambi) na aelezwe kama kuna sababu za watu kukamatwa ili na yeye awaeleze wananchi wake.

“Kwa hiyo mheshimiwa Waziri Mkuu naomba ulifuatiuilie halafu mbunge ajulishwe ni nini kinaendelea huko kwenye jimbo lake, kwa sababu wananchi kuwekwa ndani kwa kusema tu hoja hadharani haipendezi wala si jambo ambalo sheria ilikusudia.

“Lakini kama kuna jambo lingine la ziada lililofanyika basi mheshimiwa Waziri Mkuu ukishalipata mjulishe mbunge ili naye awe na utulivu, lakini pia aweze kuwajulisha wananchi anaowawakilisha kwamba wale wenzetu ambao wako kule ndani sababu ni hizi,” amesema.

Awali, Kunambi amesema kuna vitendo vya wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kukamata wananchi na kuwaweka ndani pasipokuwa na sababu za msingi, jambo linalohatarisha haki za binadamu.

Akitoa mfano, amesema Agosti 26, 2024 mkuu wa Wilaya ya Kilombero (hakumtaja jina) akiwa kwenye ziara kwenye Kijiji cha Chiwachiwa alikokwenda kusikiliza mgogoro wa ardhi baina ya msitu wa hifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na wananchi, alikamata viongozi wanne na wananchi 11.

“Akiwa katika mkutano wa hadhara mheshimiwa spika, diwani alileta hoja kwamba mheshimiwa DC hapa tunahitaji kuhakiki mipaka, wananchi wanaamini bado wako kwenye eneo la sahihi.

“Hoja hii ilimpelekea mheshimiwa DC kusema unaniharibia mkutano, ‘kamata mtendaji wa kata, mtendaji wa kijiji, mwenyekiti wa kijiji na ya wananchi 11. Mpaka sasa ninavyozungumza wako ndani,” amesema Kunambi.

Amesema inasemekana kwenye mkutano huo wa hadhara DC alipokea simu ya mkuu wa mkoa na akaiweka ‘loudspeaker’. “Kwa hiyo maekelezo ya mkuu wa mkoa na DC wakakubaliana kamata watu hao 11 na viongozi wanne, mheshimiwa diwani, lakini pia na mtendaji wa kijiji, mtendaji wa kata na wa kijiji.”

Kunambi ameliambia Bunge kuwa vitendo vya DC vimekuwa vya kawaida akienda kwenye mikutano ya hadhara anakwenda na kamati ya ulinzi na usalama na kuwafanya wananchi kushindwa kutoa hoja zao.

“Lakini, cha ajabu amekuwa akikamata viongozi mbalimbali, ilishawahi kutokea Kata ya Utembule alikamata mwenyekiti wa CCM wa kata na mwenyekiti wa kijiji akawaweka ndani siku sita, nilivyomuomba aliwatoa,” amesema.

Amesema vitendo hivyo vinarudishwa nyuma jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan ambaye aliunda Tume ya Haki Jinai na vile vile vinaenda tofauti na waraka wa utumishi wa umma namba moja wa mwaka 2023, ulitolewa Oktoba30, 2023.

Katika waraka huo, Katibu Mkuu Kiongozi anakataza matumizi ya madaraka ya ukamataji wa watuhumiwa kwa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya.

Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai Tanzania iliyokabidhi ripoti yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan Julai 15, 2023 ilizungumzia malalamiko kuhusu ukiukwaji wa sheria hiyo.

Tume ilisema imejengeka desturi ya baadhi ya wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kutumia Sheria ya Tawala za Mkoa, Sura ya 97 na Sheria ya Baraza la Usalama la Taifa, Sura ya 61 kuminya haki za wananchi katika masuala mbalimbali bila kuzingatia masharti yaliyowekwa na sheria.

Pia, tume ilibaini kuwa, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wamekuwa wakiambatana na wajumbe wa kamati za usalama katika ziara mbalimbali hata zile zisizostahili uwepo wa vyombo hivyo.

Tathmini ya tume hiyo ilibaini, viongozi hao hujitambulisha kama wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama, kitu ambacho ni kinyume na Sheria ya Baraza la Usalama la Taifa, Sura ya 61 inayowatambua kama wenyeviti wa Kamati za Usalama za Mikoa au Kamati za Usalama za Wilaya.

Pia, ilisema desturi ya wakuu wa mikoa na wilaya kuambatana na Kamati za Usalama katika ziara zao inaweza kusababisha hofu kwa wananchi na kuwafanya washindwe kufikisha mawazo na kero zao kwa viongozi hao.

Tume imesema kwa viongozi hao kuambatana na Kamati za Usalama kunasimamisha baadhi ya majukumu yanayotakiwa kutekelezwa na wajumbe hao kwa nafasi zao.

“Mathalan, wakuu wa vyombo vinavyohusika wanakosa muda wa kutosha wa kutekeleza majukumu yao ya msingi na mara nyingi hutumia vyombo vya usafiri vinavyohitajika katika utekelezaji wa majukumu mengine ya chombo kinachohusika,” ripoti ya tume inaeleza.

Kufuatia hali hiyo, tume ilipendekeza Sheria ya Tawala za Mikoa, Sura ya 97 irekebishwe ili kuondoa mamlaka ya ukamataji waliyonayo wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na viongozi wengine kwa nafasi zao, badala yake wafuate utaratibu uliopo katika Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, Sura 20 ambao unaruhusu mtu yeyote kumkamata mtu anayefanya kosa mbele yake.

Endapo ni muhimu kwa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kuendelea kuwa na mamlaka ya ukamataji, viongozi hao waelekezwe kuwa wanapotekeleza mamlaka hayo kupitia vifungu vya 7 na 15 vya Sheria ya Tawala za Mikao, Sura ya 97 mtawalia, wazingatie masharti yote yaliyoelekezwa kupitia vifungu tajwa.

Baadhi ya masharti hayo ni kuwa kosa liwe linatendeka mbele yake, liwe kosa la jinai ambalo mtu anaweza kushtakiwa, kosa hilo liwe limesababisha kuvunjika kwa amani na utulivu na hakuna namna ya kulizuia kutendeka.

Pia, ni lazima mkuu wa mkoa au mkuu wa wilaya, mara baada ya mtuhumiwa kukamatwa, amwandikie hakimu kueleza sababu zilizosababisha mtuhumiwa kukamatwa.

Mara baada ya maelekezo hayo, kiongozi yeyote atakayeyakiuka itabidi achukuliwe hatua kali, na iwapo mwathirika wa maagizo yake atafungua shauri mahakamani, basi huyo kiongozi awajibike yeye mwenyewe na Serikali isiwe sehemu ya shauri hilo.

Serikali itoe maelekezo kwa wakuu wa mikoa na wilaya kusitisha utaratibu wa kuambatana na wajumbe wa kamati za ulinzi usalama pasipo kuwa na ulazima na pia waache kujitambulisha kama wenyeviti wa kamati hizo.

Agosti 27 DC Kyobya akiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya alikwenda katika Msitu wa hifadhi wa asili wa Kilombero (KNR) wenye ukubwa wa hekta 134,511 katika Kijiji cha Chiwachiwa kujionea uharibifu uliofanywa na wananchi.

Baadaye aliagiza kukamatwa kwa watu aliosema wameshiriki kuhamasisha uvamizi kwa kukata na kuteketeza zaidi ya ekari 50 za msitu, akiwemo Diwani wa Mbingu, Nestory Kyelula.

Akiwa katika msitu huo, DC Kyobya alieleza kusikitishwa kwa kitendo hicho huku akieleza umuhimu wa msitu huo wenye mito mitatu ya Chiwachiwa, Londo na Mbingu inayochangia maji kwa ajili ya uzalishaji wa umeme katika Bwawa la Nyerere na mradi wa usambazaji maji wenye thamani ya Sh3 bilioni.

“Naambiwa miti iliyokatwa hapa ina zaidi ya miaka 100, itarudi lini? Hii haikubaliki kabisa, kama mnataka ardhi kwa ajili ya kilimo fuateni taratibu za kisheria zinavyotaka na si kuvamia ardhi,” alisema Kyobya.

Aliwaagiza kamanda wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Jeshi la Polisi Wilaya Kilombero kuhakikisha wanawakamata wote uliohusika bila kujali nafasi zao ili wafikishwe katika vyombo vya dola kwa mahojiano.

Nyongeza na Hamida Sharif (Morogoro)

Related Posts