Mganga wa kienyeji atuhumiwa kwa mauaji ya watu 10

Dar es Salaam. Mapya yamebainika ikidaiwa mganga wa kienyeji aliyetuhumiwa kwa mauaji mkoani Singida ana mji mwingine wilayani Chemba, Mkoa wa Dodoma ambako yamebainika mashimo sita walimozikwa watu.

Jeshi la Polisi limesema limebaini jumla ya miili ya watu 10 waliouawa, ikiwa ni mwendelezo wa uchunguzi na mahojiano yaliyofanywa dhidi ya watatu wanaotuhumiwa kwa mauaji ya Samwaja Said, akiwamo mganga huyo wa kienyeji.

Miongini mwa miili hiyo imo miwili ya watoto wa watuhumiwa wawili waliokuwa na miezi minne na mwingine miwili.

Agosti 26, 2024 Jeshi la Polisi lilitoa taarifa kwa umma kuhusu uchunguzi na mahojiano yaliyofanywa dhidi ya watuhumiwa hao wanaodaiwa kumuua Samwaja kwa kumnyonga hadi kufa, kisha kukata sehemu zake za siri na kufukia mwili shimoni.

Taarifa kwa umma iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime leo Agosti 28, 2024 imesema katika mwendeleo wa uchunguzi wamebaini miili ya watu 10 waliouawa, kati ya hiyo mitatu ilipatikana mkoani Singida na Dodoma ilipatikana saba.

Kati ya miili hiyo, amesema mmoja ulitupwa porini na mingine tisa ilizikwa kwa kukalishwa kwenye shimo kwa namna wahusika walivyosukumwa na imani zao za kishirikina.

Miili zaidi ilivyobainika

Kwa mujibu wa Misime, baada ya taarifa ya Agosti 26 kuhusu mauaji ya Samwaja yaliyobainika kutokana na mahojiano na ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi, walibaini mashimo mawili ambayo yalipofukuliwa ulipatikana mwili wa Gidion Mnyawi, aliyekuwa mkazi wa Makuro mkoani Singida.

Kwa mujibu wa Polisi, Nkamba Kasubi ambaye ni mganga wa kienyeji alielekeza Mnyawi atolewe kafara kutokana na kuuza shamba kwa watu wawili tofauti kwa madai wakifanya hivyo fedha zitarejeshwa.

Shimo lingine imeelezwa na Polisi zilipatikana sehemu za mwili wa binadamu ambazo ni nyonga, mkono wa kulia na wa kushoto. Haikubainika ni mwili wa nani, hivyo kulihitajika uchunguzi zaidi.

“Baada ya uchunguzi na mahojiano ya kina na watuhumiwa ambao ni Selemani Nyalandu maarufu kama Hango, Said Msanghaa ‘Mangu’ na Nkamba Kasubi walieleza mwili huo ni wa Seleman Idd (23), mkazi wa Makuro, Singida ambaye walimuua kwa kumnyonga na kumfukia kwenye shimo Juni 23, 2024,” inaeleza taarifa ya Polisi.

Misime amesema mahojiano zaidi yalipofanyika kwa ushirikiano wa wananchi, Jeshi la Polisi lilipata taarifa kuhusu mtuhumiwa mwingine, Miraji Nyalandu.

Amesema Agosti 25, 2024 Miraji alikamatwa katika Kijiji cha Misughaa mkoani Singida akijaribu kutoroka kwa kutumia pikipiki iliyokuwa na namba MC 262 CYU, mali ya Daudi Msanku ambaye wanadaiwa walimuua na kumzika kwenye Kijiji cha Porobanguma wilayani Chemba, Mkoa wa Dodoma.

“Uchunguzi uliendelea na baada ya mtuhumiwa huyu kukamatwa na kukutanishwa na watuhumiwa wenzake, ndipo Kasubi, mganga wa kienyeji Agosti 27 alikubali kuwaongoza askari Polisi hadi kwenye mji wake mwingine uliopo Kijiji cha Porobanguma, Tarafa ya Kwamtoro wilayani Chemba na kuonyesha mashimo sita waliyofukia watu wengine waliowaua na kuwazika,” inaeleza taarifa hiyo.

Misime amesema baada ya taratibu za ufukuaji kufanyika, ilipatikana miili ya Seni Jishabi (28), mkazi wa Kijiji cha Porobanguma ambaye alipotea tangu Machi 3, 2024. Amesema watuhumiwa wamedai walimuua na kumzika Aprili 2024.

Mwili mwingine ni wa Mohamed Juma (27), mkazi wa Nyamikumbi A, Mkoa wa Singida aliyepotea Mei 15, 2024. Inadaiwa watuhumiwa wameeleza walimuua kwa kumnyonga na kumzika.

Mwingine ni Daudi Msanku (27), mkazi wa Gawidu mkoani Manyara, aliyepotea Mei 27, 2024 ambaye baada ya kuuawa watuhumiwa wanadaiwa walichoma mwili wake moto, kisha majivu waliyahifadhi kwenye ndoo.

“Huyu (Msanku) ndiye ambaye pikipiki yake alikamatwa nayo Miraji Nyalandu akijaribu kutoroka baada ya kuona watuhumiwa wenzake wanakamatwa mfululizo na askari Polisi,” inaeleza taarifa.

Polisi imemtaja mwingine aliyeuawa kuwa ni Ramadhan Yusuph (26), mkazi wa Kidika mkoani Manyara, aliyeuawa Aprili 2024.

Mwili wa tano ni wa Mwekwa Kasubi, mtoto wa miezi minne wa mganga huyo wa kienyeji aliyeuawa Machi 2023.

Taarifa inamtaja mwingine kuwa ni mtoto wa miezi miwili, Maka Shabani aliyeuawa Juni 2023, ambaye ni wa mtuhumiwa Selemani Nyalandu ‘Hango’.

“Watoto hawa walizikwa wakiwa hai kwenye zizi la mifugo, pia watuhumiwa walikiri kumuua Ramadhani Kilesa (80), mkazi wa Porobanguma na kutupa mwili wake kwenye Pori la Akiba Swangaswanga,” inaelezwa katika taarifa.

Misime amesema mwili wa Kilesa ulipatikana Julai 25, 2024 lakini haikujulikana aliuawa na nani hadi jana Agosti 27, 2024 watuhumiwa walipokiri kumuua na kueleza sehemu walipomtupa ili mwili wake uliwe na wanyamapori lakini lengo lao halikutimia.

“Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za kweli na sahihi na kuendelea kukemeana kuanzia ngazi ya familia, ili kuzuia na kukomesha vitendo hivi vinavyoendelea kutokea ndani ya jamii kwa siri kubwa.

“Kila mmoja wetu tuelimishane kwa dhati, kwa kila mmoja kwa nafasi yake katika jamii ubaya na madhara ya kuendekeza imani za kishirikina, tamaa za mali bila ya kufuata maelekezo ya Mwenyezi Mungu, sheria za nchi na miiko katika jamii, kudhulumiana, kulipiza kisasi na wivu wa mapenzi,” imesema taarifa.

Misime amesema uchunguzi wa mlolongo wa matukio hayo ya Singida na Dodoma unaendelea, pamoja na uchunguzi wa watu wengine wanaotekeleza uhalifu kama huo, akieleza kitakachobainika umma utafahamishwa.

Related Posts

en English sw Swahili