Mwanza. Wakati Mkoa wa Simiyu ukiongoza kitaifa kuwa na waganga wa tiba za asili zaidi ya 9,000 kati ya 57,000 nchini, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imechunguza dawa za asili zaidi ya 2,000 za waganga wa tiba hiyo.
Mikoa mingine inayoongoza kuwa na waganga wengi wa tiba za asili ni Geita yenye waganga zaidi ya 6,000 na Mwanza yenye waganga Zaidi ya 4,000.
Akizungumza leo Jumatano Agosti 28, 2024 kwenye maadhimisho ya wiki ya tiba asili ya mwafrika jijini Mwanza, Kaimu Msajili Baraza la Tiba asili na Tiba Mbadala, Martin Magongwa amesema Kanda ya Ziwa inaongoza kwa usajili wa waganga hao huku, akiwapongeza kwa kuitikia wito wa Serikali wa kutoa huduma hiyo endapo wamesajiliwa.
“Waganga wanasajiliwa kwa kigezo cha kupata barua na muhtasari kutoka Serikali ya mtaa…Serikali ya mtaa ndio ina wajibu kwanza wakuthibisitisha huyu ni mganga halisi kwa sababu ili asajiliwe ni lazima awe amekaa kwenye eneo hilo kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitatu na wananchi wa eneo hilo wanamtambua,”amesema
Kuhusu dawa za tiba asili zilizosajiliwa na baraza hilo ni 127 kati ya zaidi ya dawa 2,000 zilizochunguzwa na maabara ya mkemia mkuu wa Serikali.
“Mpaka sasa hivi dawa zilizopitia kwa mkemia mkuu wa Serikali zikapata idhini ya usajili, zimesajiliwa na kutambulika kimataifa ni dawa 127 miongoni mwa dawa hizo ni dawa ambazo zinatumika kwenye mfumo jumuishi wa hospitali saba za rufaa za mkoa,”amesema Magongwa.
Meneja wa Kanda ya Ziwa wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, John Faustine amewatoa hofu waganga wanaosita kupeleka dawa zao kwaajili ya uchunguzi wa kimaabara wakihofia gharama kubwa ambayo awali ilikuwa zaidi ya 700,000 lakini sasa imeshuka hadi 300,000.
“Gharama za uchunguzi zilikuwa juu lakini kupitia Wizara ya Afya ilitoa mwongozo na maelekezo kwamba kwa mtu yeyote ambaye uwezo wa kuleta dawa kupimwa ni mdogo anapita Baraza la Tiba Asili, kuna fomu maalum wanampa anaijaza akiishaijaza wanampa punguzo la bei,” amesema.
Faustine amewataka wadau wanaotengeneza dawa za asili kuzipeleka kuchunguzwa ili kama ni salama ziweze kulasimishwa na kusaidia matibabu pasipo changamoto yoyote ile, huku akiwataka watumiaji wa dawa hizo kutumia zilizosajiliwa kwakuwa tayari mamlaka hiyo inajua uhakika, usalama na ubora wake.
“Tunawasisitiza ni namna gani ya kusindika zile dawa na vifungashio vinavyotumika. Kuna changamoto zimekuwepo wanafunga kwenye vifungashio vilivyokuwa vimefunga dawa za viwandani, sasa ile ukienda kuchunguza unakuta kuna viambata vya dawa za viwandani… ile sio dawa ya asili tena kwahiyo tumekuwa tukiwapa elimu hiyo watumie vifungashio ambavyo si vifungashio vingine ila vifungashio maalumu kwaajili ya dawa wanazozitengeneza,” amesema.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amewataka waganga hao kuungana na Serikali kukemea vitendo vya kikatili ikiwemo mauaji ya watu wenye ualbino pamoja na wimbi la kupotea kwa watoto vinavyodaiwa kuchochewa na baadhi ya waganga wanaofanya ramli chonganishi