Dodoma. Ndani ya nyumba walimolala familia ya watu sita ya Michael Richard (36), damu imetapakaa ukutani, godoro na sehemu ya kitanda vikiwa vimeungua moto.
Moja ya dirisha la chumba hicho pia limeungua moto, huku vitu vilivyokuwa sebuleni katika nyumba hiyo ya vyumba viwili iliyopo Mtaa wa Mbuyuni, Kata ya Kizota mkoani Dodoma, vikinusurika kuungua baada ya majirani kuzima moto.
Usiku wa kuamkia leo Agosti 28, 2024 wanafamilia hao walivamiwa na watu wasiojulikana waliomuua Michael na kisha kuwajeruhi mke na watoto wake watatu, kabla ya kuchoma moto nyumba hiyo.
Waliojeruhiwa ambao wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma ni Agnes Eliah ambaye ni mke wa Michael na watoto Ezra, Witness na Ephrahim Michael. Mtoto mdogo mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu aliathiriwa na moshi.
Balozi wa Shina Namba Tisa katika Mtaa wa Mbuyuni, Angela Faustine amesema usiku wa kuamkia leo walisikia yowe, hivyo majirani waliamka na kwenda kwenye nyumba hiyo iliyokuwa ikiwaka moto.
“Tulifanya jitihada za uokozi, tukawapeleka majeruhi hospitali, tuliporudi kuangalia ndani kumbe kuna mtu alikuwa amebakia naye alikuwa ameungua kwa moto. Baada ya hapo tulitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ambao walikuja na kutupa ushirikiano,” amesema.
Amesema baada ya uchunguzi, Polisi walichukua mwili na kuupeleka hospitali.
Amesema Michael alikuwa mfanyabiashara ndogondogo (machinga) aliyehamia mtaani hapo baada ya kujenga nyumba hiyo miaka miwili iyopita.
“Hili dirisha ndilo lilikuwa na moto sana na godoro pia lilishika moto,” amesema Angela.
Clement Mganga, ambaye ni rafiki wa Michael amesema alipigiwa simu na rafiki yake na alipofika eneo hilo alielezwa walivamiwa na watu wasiojulikana ambao walimpiga hadi wakamuua kabla ya kuchoma moto nyumba.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi amesema tukio hilo limetokea saa 9.00 usiku wa Agosti 28.
“Baada ya kuvamiwa alipigwa na kitu chenye ncha butu kichwani na kusababisha kifo cha huyu mwanaume. Baada ya tukio hilo walichoma moto godoro, lakini inaonekana huyu mtu alishauawa na baadaye kuwashambulia na kuwajeruhi watoto wawili na mke wake,” amesema.
Amesema uchunguzi wa awali unaonyesha chanzo cha tukio hilo ni kulipa kisasi na kuwa wanaendelea na msako wa waliohusika na tukio hilo.
“Kwa sasa vijana wanaendelea na uchunguzi mkali na bado hatujajua hasa kisasi hicho kilitokana na nani. Tunaendelea na msako na tunaamini tutafanikiwa kuwakamata,” amesema.
Amesema watu hao walichoma moto godoro ili kupoteza mazingira ya ushahidi.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma, Dk Sara Ludovick amesema usiku wa kuamkia leo walipokea mwili mmoja wa marehemu na majeruhi wanne, wote wa familia moja.
Amesema mwili wa Michael ulikuwa na majeraha mchanganyiko ya moto na yasiyo ya moto na umehifadhiwa hospitalini hapo. Amesema majeruhi wanaendelea na matibabu.