Mzee wa miaka 75 kortini akidaiwa kumuua mkewe kwa kumchapa fimbo

Geita. Mkazi wa Kijiji cha Kibanga Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, Bujukano Lusana (75) amefikishwa Mahakama Kuu Kanda ya Geita akishtakiwa kwa kosa la kumuua mkewe bila kukusudia  kwa kumchapa na fimbo.

Katika shauri hilo namba 29166/2024, anadaiwa kutenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 195(1) na 198 cha Kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Kesi hiyo iliyokuja kwa ajili ya kusomwa maelezo ya awali, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Scolastica Teffe ameieleza Mahakama kuwa Februari 28,2024 katika Kijiji cha Kabanga, Bujukano alimuua  bila kukusudia mkewe, Maria Masalu.

Teffe ameieleza Mahakama kuwa siku ya tukio, mshtakiwa alitumia fimbo kumpiga mkewe akiwa amelala chini maeneo ya kichwani na mgongoni, kitendo kilichosababisha kifo chake.

“Taarifa za uchunguzi wa mwili wa marehemu ulionyesha kifo kilisababishwa na majeraha,” amesema Teffe.

Wakili huyo wa Serikali ameeleza katika kesi hiyo watakua na mashahidi tisa na vielelezo viwili.

Mshtakiwa amekana kutenda kosa hilo, Jaji anayesikiliza kesi hiyo, Kelvin Mhina ameahirisha shauri hilo hadi wakati mwingine litakapopangwa kwa ajili ya usikilizwaji.

Mshtakiwa anatetewa na wakili wa kujitegemea, Eliaman Ayoub.

Related Posts