Omar ameyasema hayo leo Oktoba 28 mara baada ya kuwasili na kupokelewa katika ofisi ndogo za makao makuu ya Chama hicho Vuga Mjini Unguja kufuatia kuteuliwa kwake kushika nafasi ya Naibu katibu mkuu wa Chama Zanzibar katika kikao cha halmashauri mkuu kilichomalizika hivi karibuni jijini Dar es Salam.
Amesema Chama cha ACT Wazalendo kushinda na kushika Dola ni jambo ambalo halina mbadala ukizingatia uwepo wa hali ngumu ya maisha kwa wananchi wa kawaida maeneo yote Unguja na Pemba.
Pia amesema kuwepo kwa ufisadi mkubwa kwenye miradi mingi inayofanywa na Serikali,ufisadi ambao umekua ukibainishwa kila mwaka kupitia ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) lakini hakuna hatua yoyote hile inayochukuliwa.
‘’Mimi naamini uwepo wa mazingira haya ni fursa adhimu kwetu ya kuimaliza CCM uchaguzi ujao,jambo la kufanya kila mmoja wetu anapaswa kuhakikisha anafanya kazi ipasavyo kuleta mabadiliko’’amesema.
Aidha Naibu katibu mkuu huyo amesema ahatakikisha kuanzia ngazi ya Taifa kwenye chama hicho mpaka tawi kila mmoja anasimamia ipasavyo jukumu lake akiamini kuwa mashirikiano ya pamoja na ujenzi wa Chama imara yatasaidia kukipa ushindi mkubwa zaidi uchaguzi wa mwezi oktoba 2025.
Sambamba na hilo amewataaka wanachama wa Chama hicho kufahamu pamoja na uwepo wa hali ngumu ya maisha watashindwa kufanikiwa kuiondoa CCM madarakani iwapo kila mwanachama hatafanya wajibu wake.
Katika hatua nyengine Naibu katibu mkuu huyo mpya wa Chama hicho ameleza masikitiko yake juu ya uwepo wa sheria ya kura ya mapema na kueleza kuwa jambo hilo halikubaliki na linapaswa kupingwa na kila mpenda demokrasia.
Amesema uwepo wa kura hiyo ya mapema ni ishara ya kuhujumu na mikakati ya wizi wa kura kwenye kila uchaguzi mkuu,na ni miongoni mwa dalili za kutokubalika kwa chama cha Mapinduzi CCM kwa wananchi walio wengi.
Amesema pamoja na uwepo wa mazingira hayo, watasimama na wananchi wa Zanzibar kupinga uwepo wa kura hiyo wakijua kuendelea kuwepo kwake ni kusababisha maafa makubwa kama yaliotokea uchaguzi uliopita ambapo watu 21 waliuwawa bila ya kuwa na hatia yoyote hile.
‘’Na nataka niseme wazi kwa sababu suala hili la kura ya mapema husababisha vurugu na mauaji ya watu wasiokua na hatia ni wakati sasa kila mwananchi wa Zanzibar,asasi za kiraia na majukwaa ya dini kupinga hadharani kuwepo kwa kura hii ya mapema bila ya woga kwa lengo la kuepusha maafa na mauaji ya wananchi wasio na hatia’’alisema.
Awali Katibu wa habari na uenezi wa Chama hicho Salim Abdalla Bimani akimkaribisha Naibu katibu huyo alisema ni wajibu wa kila mwanachama kuhakikisha anakipa ushindi chama hicho.
Alisema Zanzibar inahitaji kutolewa ilipo sasa ukizingatia hali ya maisha imezidi kuwa ngumu kila siku huku kukishindwa kufanyika kwa juhudi zozote zile za kuwakwamua wananchi na hali hii ngumu ya maisha.
Kwa upande wake Katibu wa Ngome ya wanawake Taifa Bi Fatma Alhabib Fereje amewataka wanawake wa Chama hicho na wengine wote kujitokeza kuunga mkono harakati za Chama chao wakifahamu, kufanya hivyo ni wajibu wao kama wanawake