Rais Samia aruhusu wakuu wa taasisi kumshauri bila hofu

Arusha. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka watendaji wakuu wa taasisi na mashirika ya umma nchini kumwambia ukweli hasa pindi anapowataka wawekeze sehemu ambayo wanaona haiwezi kuwa na tija.

Amesema kabla ya kufanya hivyo ni muhimu kufanyika tafiti na kujiridhisha kabla ya kuweka fedha.

Rais Samia ameyasema hayo leo Jumatano Agosti 28, 2024 alipokuwa akifungua kikao kazi cha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi na mashirika ya umma kinachofanyika jijini Arusha.

Amesema ni muhimu kufanyika utafiti wa kutosha kabla ya kuamua kuwekeza, ili kupunguza hasara ambazo zinaweza kujitokeza pale Serikali inapowekeza katika miradi mbalimbali na kulinda rasilimali za wananchi.

Rais Samia alitolea mfano wa uwekezaji katika mradi wa kwanza wa Mkulazi mkoani Morogoro ambao ulishindwa kutekelezwa chini ya Mtendaji Mkuu wa Shirika la Taifa la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba.

“Mfano mbaya wa Mshomba alipowekeza kwenye Mkulanzi one, limradi likubwa hilo namuuliza ulikuwa na upembuzi yakinifu anasema ilikuwepo mheshimiwa. Nikamuuliza hukuona kwamba mradi mkubwa, aaah najua lakini ndiyo ilikuwa ‘wakati ule’.

“Lakini sasa kama kitu hakikupi faida unawekeza tu kwa sababu ya ‘wakati ule’, haiwezekani, nikamwambia hata nikikuita mimi nikikwambia wekeza pale ukiona pana hasara niambie mheshimiwa Rais pale kuna hasara usiingie, muwekeze mkiwa na uhakika fedha iliyowekezwa itarudi,” amesisitiza Rais Samia.

Amesema yapo mashirika yenye utashi wa kisiasa na wengine wameingiza fedha sehemu ambazo hazitarudi.

“Sina kigugumizi kusema na nalisema hili sijui mara ya pili au tatu, mfano wangu mkubwa ni kama Ubungo Plaza, ilivyofunguliwa ilikuwa mikutano yote tunaswagwa huko, sasa hivi nani anatumia Ubungo Plaza,” amehoji.

Uwekezaji mwingine alioutolea mfano ni wa Benjamin Mkapa Tower yote ya jijini Dar es Salaam na kumtaka Msajili wa Hazina kuwapeleka watendaji hao wakaone jengo hilo linavyotumika na kuwa tangu lilivyokuwa jipya halikuwahi kujaa.

“Katazameni uwekezaji kama ule, muwekeze mkiwa mna hakika fedha inayoingizwa itarudi, sekta binafsi akiweka shilingi yake ameshafanya utafiti wa kutosha. Natoa mifano simlaumu mtu, hivyo kama hamuwezi wapeni sekta binafsi au wauzieni,” amesema.

Uwekezaji maeneo ya kimkakati

Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema ni wakati wa mashirika na taasisi hizo za umma kuwekeza katika maeneo ya kimkakati akitolea mfano wa eneo la usalama wa chakula.

Rais Samia alitolea mfano akiwa kwenye ziara mkoani Morogoro, alipozindua kiwanda cha sukari Mkulazi cha kampuni Hodhi ya Mkulazi (MHCL), chenye wana hisa wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Jeshi la Magereza Kupitia Shirika la Uzalishaji Mali (Shima).

Amesema NSSF na Magereza wamewekeza kimkakati na wameweza kufanikiwa baada ya mageuzi kadhaa ambapo awali mradi huo ulikwama kutekelezwa.

Ameeleza mwanzoni mwa mwaka huu kulitokea uhaba wa sukari, eneo ambalo limewekezwa na sekta binafsi licha ya kutekeleza sera za Serikali ila wana mikakati yao wenyewe.

“Unaweza kuwa na uhaba wa kitu na usiwe na cha kufanya, tuliagiza nje ya wao na kujaza sukari kwenye nchi ili imfikie mnyonge na bei ya sukari ikashuka, lakini kile kimeudhi wenzetu.”

“Ila unajiuliza huyu mwekezaji Mtanzania kwa nini alifanya hivi mjombaake kijijini akanunue kilo kwa Sh6,000 au Sh8,000 kwa kuangalia faida ya kiwanda chake. Lakini tukiwa na wawekezaji mashirika ya umma kama hao wa Morogoro tukipata mikiki ya sekta binafsi, sukari inayozalishwa na shirika la umma itasaidia,” amesema.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amezitaka taasisi na mashirika ya umma nchini kutoogopa mabadiliko ya kiutendaji katika taasisi zao, kwani yamelenga kuwekeza kwa tija, kuondokana na utegemezi na kuwa na uchumi imara.

Aidha amesema Serikali itaendelea kuunganisha na kufuta baadhi ya mashirika na taasisi ambazo zimeshindwa kufikia malengo ikiwemo kushindwa kujiendesha na kutegemea Serikali Kuu.

Amesema agenda ya mageuzi duniani kote ni ngumu kwani binadamu anapenda kuwa na alichokizoea, kwenye baadhi ya maeneo kuwa mageuzi katika miradi au maisha ndiyo maendeleo.

Rais Samia amesema Serikali inaposisitiza kuhusu mabadiliko na ufanisi katika taasisi na mashirika ya umma ni kwa lengo la kuhakikisha yanaleta faida na kulinda rasilimali za wananchi.

“Katika taasisi au mashirika ya umma, zimewekezwa karibu Sh76 trilioni, hivyo tunaposisitiza mabadiliko au ufanisi ni kwa lengo la kulinda rasilimali za wananchi ambazo zimewekezwa humo na kutekeleza lengo la kuundwa kwenu,” amesema.

“Mashirika haya yameundwa ili Serikali ipate nusura ya kwenda kutafuta fedha nje ya nchi na ili yachangie na mambo yaende vizuri, mabadiliko haya tunayafanya kwa nia njema kabisa ya kujenga nchi yetu, Taifa letu,” amesema Samia.

Rais Samia ameongeza kuna baadhi ya taasisi na mashirika ambayo yakitekeleza wajibu wake ipasavyo yatasaidia kuvutia wawekezaji wa nje ya nchi na kuboresha mashirika ya ndani ili yaweze kufanya uzalishaji mzuri.

Ametolea mfano Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuwa endapo litakuwa makini na kusimamia viwango vya uzalishaji wa ndani itawafanya wazalishaji wa ndani kufikia viwango vya kimataifa, hivyo kusaidia  kuzuia bidhaa zilizo chini ya kiwango kuingia nchini.

Nyingine ni Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) ambao wakiweza kuwapa njia waliofikia uzalishaji wa bidhaa kwa viwango vya kimataifa namna ya kwenda kwenye masoko ya nje, hiyo itasaidia wawekezaji wa ndani.

“TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) kwa mfano wakifanya kazi yao vizuri sana kuwafanya wawekezaji wanaofanya kazi nje kuja ndani, walipe viwango ambavyo havileti malalamiko, hakuna kuchukua mashine za watu, hakuna kubambika, tutavuta wawekezaji wengi waje kuwekeza,” amesema.

 Uwekezaji nje ya mipaka

Kuhusu uwekezaji nje ya mipaka, Rais Samia amesema kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka jana iliangazia mashirika 76,000 duniani kote na katika nchi 91 ilibainisha kuwa robo tatu ya nchi hizo, zina mashirika yanayofanya uwekezaji nje ya nchi.

Amesema ripoti hiyo inaonyesha baadhi ya nchi hizo mashirika yake ya umma yanachangia asilimia 30 ya mapato ghafi katika nchi zao.

“Nilipoiona hii na kusoma ripoti ya msajili nchini, mashirika yangu yananichangia pato ghafi la ndani kwa asilimia moja, angalau tungekuwa tunachangia asilimia 8 au 10 au 11, kama Mtanzania sijui tunajisikiaje.

Rais Samia amesema Afrika nchi zinazoongoza katika kufanya biashara nje ya nchi zao ni pamoja na Angola, Botswana na Mouritius na kuwataka watendaji hao kujadili suala hilo kwa upana na kuangalia namna wanavukaje, lakini ni lazima zifanye kwanza vizuri nchini.

Kuhusu mashirika kufutwa au kuunganishwa Rais Samia amesema suala hilo limekuwa likileta kelele akitolea mfano Shirika la Maendeleo (NDC) ambalo halijulikani lipo au limekufa.

“Mfano NDC hujui yupo hujui kafa, kila mradi wake sifuri, sijui alikuwa na mradi gani hamna, unajiuliza huyu anafanya nini lakini lilivyokuja pendekezo huyu sasa aondoshwe, wizara imeandika barua kila mahali NDC haiwezi kufutwa,” amesema Samia.

Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Augustine Vuma amesema sababu zinazofanya taasisi kufanya vibaya ni kukosa mitaji, uwezo mdogo wa viongoza, kukosekana uwajibikaji na mnyororo wa utendaji.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema suluhisho za changamoto hizo za mashirika ya umma kushindwa kufanya vizuri zitatatuliwa na sheria ya mfuko wa uwezeshaji ambao watasaidiwa mitaji, lakini pia viongozi watapatikana kwa ushindani.

“Zaidi tutawapa mashirika na taasisi mbinu za kutekeleza kuvuka mipaka lakini pia mitaji, watakaokuja na barua ya maombi inayoonyesha mafanikio ya uwekezaji huo,” amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha ,Paulo Makonda  amesema amepanga hafla ya kipekee kwa ajili ya kuwakutanisha wafanyabiashara wa mkoa huo na wakuu hao wa taasisi na wenyeviti wao.

Amesema lengo la kuwakutanisha ni kuwapa fursa wafanyabiashara na viongozi hao kufahamiana na kujenga mahusiano yatakayorahisisha shughuli zao za kibiashara.

Related Posts