Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema uamuzi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina kufuta na kuchanganya baadhi ya mashirika ambayo hayaonekani kufanya vizuri umesababisha kelele nyingi.
Jambo hilo amesema linasababishwa na watu kuogopa mageuzi yanayofanyika katika mashirika ya umma licha ya kuonekana kufanya vizuri katika baadhi ya maeneo.
Rais Samia ametoa kauli hiyo wakati ambao tayari Ofisi ya Msajili wa Hazina imeshafanya uamuzi wa kuyaunganisha mashirika 19 na kutengeneza saba.
Ametoa kauli hiyo leo Agosti 28, 2024 alipofungua kikao kazi cha pili cha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi za umma kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili ya Hazina.
Rais Samia ametoa mfano wa Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) ambalo amesema tangu anaanza kazi mwaka 1977 amekuwa akilisikia.
“Wakati huo lilikuwa likizalisha betri za redio zilizokuwa zikijulikana ‘National’ baadaye lilizalisha mipira ya magari inaitwa gereral tires lakini tangu hapo halikuwahi kusikika tena.
“Kuanzia hapo, general tire ikafa kabisa, bwana ametoa bwana ametwaa na NDC haijulikani kama ipo au imekufa kwani kila mradi wake ni sifuri,” amesema.
Rais Samia amesema, “Sijui ana mradi gani, hakuna. Sijui ana chuma Liganga, Mchuchuma hakuna. Sasa unajiuliza huyu anafanya kazi gani, lakini lilipokuja pendekezo huyu sasa aondoshwe wizara imeandika mabarua kila sehemu NDC yetu, haiwezi kufutwa.”
Amesema inawezekana malengo yaliyokuwa yamewekwa juu ya NDC yalikuwa mazuri ila huenda yamepitwa na wakati, hivyo yanahitaji yarekebishwe au haina kazi.
Amesema kwa sasa upo ushirikiano wa Taasisi za Umma na Binafsi (PPP) ambao huenda umechukua kazi za NDC lakini kufutwa kwake kunajenga hofu ambayo wakati mwingine isiyokuwa na ulazima.
Ametoa mfano wa mashirika yaliyochanganywa na kutengeneza kitu kimoja ni Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) ambayo iliundwa kutokana na kuunganishwa taasisi ya utafiti ya viuatilifu vya kitropiki na kitengo cha huduma za afya za mimea ambazo zilikuwa zikifanya kazi zinazokaribiana na hayakuwa yanaleta faida.
“Kuchanganywa kwake sasa lile shirika lililoundwa (TPHPA) limeiwezesha Tanzania kupata vyeti vya ubora wa kimataifa kwa sababu malengo yote yamekusanywa na kufanya kazi moja na kukaa katika mlengo ambao ulitakiwa kufanyiwa kazi, sasa Tanzania ina viwango vya ubora wa kimataifa,” amesema.
Amesema kupatikana kwa vyeti hivyo vya ubora kumefanya kazi za Tanzania kutambuliwa kimataifa, masoko hayatakimbia bidhaa za Tanzania na wameweza kukusanya fedha na kutoa gawio serikalini.
Amesema jambo hilo linathibitisha kuwapo faida ya kuchanganya mashirika ambayo hayafanyi vizuri huenda malengo yao yanafanana au yamepitwa na wakati.
“Kufuta pia si vibaya, kama uliundwa huko nyuma, haiui mtu jamani ambaye anazaliwa, anakua, anatumika, anatumika wee… Mpaka anakua basi Mungu anasema basi anamchukua. Sasa itakuwa shirika tuliloliunda wenyewe kama halifanyi vizuri basi liondoke tu, hatuwezi kwenda kulinda nafasi za watu na mashirika hayazalishi, hayana tija haiwezekani,” amesema.
Amesema madhumuni ya Serikali ni mashirika yafanye kazi na kuzalisha, akitoa mfano wa yale yanayotoka nje ya nchi namna ambavyo yamekuwa yakichukua zabuni ikiwemo za kujenga, biashara na kukusanya fedha kwenda nchini kwao.
“Sisi mashirika yetu yako hapahapa ndani, tunawapa nafasi nafasi wale, wabebe fedha zetu wapeleke kwao sisi tunaangalia tu, kwa hiyo nadhani wakati umefika wa kubadilika na kubadilika kweli kweli,” amesema.