Agosti 17, mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc – Organ Troika) kwenye mkutano wa kawaida wa 44 wa Sadc uliofanyika Harare, Zimbabwe.
Katika mkutano huo, Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Sadc huku Rais wa Madagascar, Andry Rajoelina akiwa ni mwenyekiti ajaye baada ya Mnangagwa kumaliza muda wake wa mwaka mmoja.
Nafasi ya mwenyekiti wa asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ni ya mwaka mmoja na inakwenda kwa mzunguko kama ilivyo kwa nafasi ya mwenyekiti wa Sadc, hivyo anayeteuliwa anakutumikia kwa mwaka mmoja kabla ya kukabidhi kijiti kwa mwingine.
Katika nafasi hiyo, Rais Samia ataongoza asasi hiyo akiwa pamoja na viongozi wengine ambao ni pamoja na mwenyekiti ajaye wa taasisi hiyo, Rais wa Malawi, Lazarus Chakwera pamoja na mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema.
Kwa mujibu wa tovuti ya Sadc, jukumu la Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama itakayoongozwa na Rais Samia ni kutoa ushauri na maelekezo kwa nchi wanachama kwenye mambo yanayotishia amani, usalama na ustahimilivu katika ukanda huu.
Viongozi watatu wa asasi, wanaratibu na kutoa maelekezo kwa nchi zinazokabiliwa na mizozo ya kiusalama, kisha watatoa ripoti yao kwenye mkutano mkuu wa Sadc kuhusu mizozo waliyoishughulikia na mapendekezo yao.
Moja ya majukumu yaliyo mbele yake ni kuendeleza utatuzi wa mgogoro uliopo nchini Lesotho unaotishia amani na usalama wa nchi hiyo. Mzozo huo wa muda mrefu, bado haujapata ufumbuzi wa kudumu.
Taarifa ya pamoja (communique) ya viongozi wa Sadc waliohudhuria mkutano huo wa 44, inaeleza kwamba kuna maendeleo chanya yamepatikana kwenye Mabadiliko ya Taifa ambapo wameitaka Serikali ya Lesotho na vyama vya siasa bungeni kuharakisha kupitishwa kwa marekebisho ya vifungu vya 10, 11 na 12 vya Muswada wa Marekebisho ya Katiba, 2024.
Wakuu wa nchi, kwenye taarifa hiyo, wamelipongeza jopo la marais wastaafu wakiongozwa na Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete kwa jitihada zao za kuendelea kusimamia mabadiliko katika taifa la Lesotho. Pia, wamehimiza ukamilishaji wa mchakato huo wa mabadiliko Lesotho.
Rais Samia na viongozi wenzake wataendeleza juhudi hizo zilizoanzishwa na viongozi waliotangulia kwenye asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama katika kukamilisha mabadiliko ya Katiba nchini Lesotho yatakayoimarisha Amani katika taifa hilo dogo Kusini mwa Afrika.
Suala la kudorora kwa amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ni jukumu jingine lililo mbele ya Rais Samia. Jitihada kadhaa zinafanyika ikiwemo usuluhishi unaofanyika jijini Luanda, Angola kumaliza uhasama baina ya Rwanda na DRC.
Mkutano wa Sadc umempongeza Rais wa Angola, Joao Lourenco kwa jitihada zake za kuleta Amani katika eneo lililoathirika la Mashariki mwa DRC kupitia majadiliano kati ya Rwanda na DRC ya kuzitaka nchi hizo kuacha mzozo.
Chaguzi ni moja ya michakato inayotishia ulinzi na usalama katika mataifa mengi Afrika licha ya kuwa ni njia ya kidemokrasia ya kupokezana madaraka. Kutokana na umuhimu wa jambo hilo, Sadc kupitia asasi yake, itakuwa mguu sawa kufuatilia siasa kwa wanachama wake.
Baadhi ya mataifa ya Sadc yanatarajia kufanya uchaguzi kuanzia sasa hadi Desemba 2024, miongoni mwa mataifa hayo ni pamoja na Msumbiji (Oktoba 9), Botswana (Oktoba), Namibia (Novemba 27) na Mauritius (Novemba 30).
Kati ya nchi hizo, Msumbiji ndiyo nchi ambayo imekuwa ikikabiliwa na tishio la usalama kutokana na kuwepo kwa vikundi vya wapiganaji wa kigaidi katika eneo la kaskazini la Cabo Delgado.
Viongozi wa Sadc katika taarifa yao ya pamoja wameipongeza Serikali ya Msumbiji kwa kutoa ushirikiano kwa vikosi vya Sadc vilivyokuwa vikiimarisha ulinzi Msumbiji (SAMIM) kabla ya kuhitimisha majukumu yao nchini humo.
Usalama wa mipaka na watu wake, mfumo wa uchaguzi na masuala ya uchumi ni miongoni mwa mitihani migumu itakayomkabili Rais Samia katika nafasi hiyo kama inavyoelezwa na Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (Out), Dk Revocatus Kabobe.
Dk Kabobe anaeleza ukanda wa Sadc unakabiliwa na changamoto ya usalama wa mipaka na watu wake na hilo linathibitishwa na uingiaji wa wahamiaji haramu kutoka eneo moja kwenda lingine.
“Tumeshuhudia wahamiaji haramu kutoka eneo moja kwenda eneo jingine hasa wengi wakitokea Somalia na kusambaa kwenye ukanda wa Sadc. Juhudi za pamoja zinahitajika kukabiliana na wimbi hili la wahamiaji haramu,” anasema.
Changamoto nyingine itakayomkabili Rais Samia kwa mujibu wa mwanazuoni huyo, ni kukosekana mifumo imara ya kusimamia haki hasa kwenye chaguzi.
“Tumeshuhidia mara kadhaa machafuko na hali ya kutoelewana pindi uchaguzi unapotamatika. Walioshindwa mara nyingi huwanyooshea kidole walioshinda kwa kusema hawakushinda kihalali,” anaeleza.
Anaeleza hayo yanasababishwa na kukosekana kwa imani katika mifumo ya kusimamia chaguzi za nchi wanachama wa Sadc.
“Kibarua hiki anakiweza maana hapa kwetu tayari ameanza kufanya mabadiliko kwenye tume yetu ya uchaguzi kwa kubadilisha sheria. Ingawa bado mabadiliko hayajakidhi matakwa ya wadau wa uchaguzi ila nina imani ni mwanzo mwema wa safari ya kwenda mbele ili kujenga mifumo imara na ya kuaminikana kwa wadau wote wa uchaguzi,” anasema.
Mtihani mwingine kwa Rais Samia, anasema ni uwepo wa dhana kuwa nchi za ukanda huo hazijiwezi kiuchumi.
“Dhana hii inaweza kubadilishwa kama kutakuwepo na juhudi za pamoja za kujenga uchumi wa pamoja kwa nchi hizi ili kuwezesha mtemgamano wa sekta za kibiashara na kilimo. Hili linawezekana kama utakuwepo utashi wa kisiasa kwa washirika wa Sadc,” anaeleza.
Dk Kabobe anasema changamoto nyingine inayomkabili Rais Samia katika nafasi hiyo ni mahusiano hafifu kati ya vyama tawala na vyama vya upinzani.
“Kumejengeka dhana ya uadui na kutoshirikiana baina ya pande hizi hizi. Kila upande unauona pande wa pili kama adui. Hii ni changamoto kubwa kwenye siasa za ukanda wa SADC,” anasema.
Hata hivyo, anaweka wazi kuhusu uwezekano wa kupatikana ufumbuzi wa changamoto hiyo kwa kuwa mkuu huyo wa nchi amekuwa akisimamia mambo hayo kupitia falsafa yake ya R4 nchini.
Mtihani mkubwa kwa Rais Samia katika nafasi hiyo, kwa mujibu wa Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Conrad Masabo, ni changamoto za kisiasa zilizopo katika taifa analoliongoza.
Kwa mujibu wa mwanazuoni huyo, kama kasoro za kisiasa zilizopo ndani ya taifa lake imeshindikana kuzimaliza, atawezaje kushughulikia za mataifa yote wanachama wa Sadc.
Uhalisia wa changamoto za kisiasa na demokrasia zilizopo nchini, Dk Masabo anasema zinaiondolea nchi uhalali wa kuwa kinara wa masuala hayo.
“Tumepata uongozi katika kipindi ambacho kama nchi hatuko imara kisiasa, hata kama tutajidanganya kwa kusema tuko sawa lakini kiuhalisia hatuko sawa, sasa wewe mwenyewe una changamoto unatarajia utaweza kutatua za wenzako,” anasema.
Hata hivyo, anaeleza kwamba pamoja na jukumu la asasi hiyo la kusimamia masuala ya siasa, amani na ulinzi, itifaki za utendaji wake zinatoa mwanya kwa kiongozi wake kuleta ubunifu katika kushughulikia masuala hayo.
“Hiyo ni taasisi ndogo ndani ya Sadc, (Rais Samia) hawezi kuamua tofauti na mdundo wa Mwenyekiti wa Sadc wa wakati husika na shida ya taasisi za Afrika, tunafanya uamuzi kwa kukubaliana na kutoa msimamo wa pamoja,” anasema.
Kama Sadc imeshindwa kushughulikia masuala ya amani, ulinzi na usalama, anasema usitegemee asasi iliyo ndani yake itafanikiwa kulitekeleza hilo.
“Asasi hiyo haiwezi kufanya zaidi ya ambacho Sadc inaweza kufanya na ‘reflection’ yake tunapaswa kuiona ndani ya Sadc inavyofanya, ndipo tutaona,” anasema.
Anasisitiza kwamba ili kupima magumu yatakayomkabili Rais Samia katika nafasi hiyo, ni vema kujua mipaka na itifaki za uenyekiti wake zinaishia wapi.
Kwa upande wake, mkufunzi wa masuala ya diplomasia kutoka Taasisi ya Diplomasia ya Salim Ahmed Salim, Godwin Amani anasema Rais Samia anaingia katika nafasi hiyo wakati ambao baadhi ya nchi wanachama zipo kwenye machafuko.
Anataja mfano wa nchi hizo ni Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Msumbiji na juhudi mbalimbali za kusaka suluhu zimefanyika bila mafanikio.
Amani anaeleza kwa uzoefu wa Tanzania katika usuluhishi, anaamini suluhisho litapatikana chini ya uenyekiti wa Rais Samia.
“Kwa nafasi yake Rais Samia anategemewa ndiye atakayekuwa chachu ya kusaidia amani kupatikana katika nchi zenye machafuko na Tanzania inaongoza kwenye masuala ya amani kwenye ukanda wa Sadc, hivyo anaamini tutafikia mafanikio,” anasema.
Matumaini yake yanatokana na kile alichokifafanua kuwa kwa muda mrefu Tanzania imekuwa moja ya nchi zinazosuluhisha migogoro ya mataifa mengi Afrika na inafanikiwa.a