Mwanza. Serikali inatarajia kuongeza rada mbili za utabiri wa hali ya hewa Juni, 2025 na kufanya kuwa na jumla ya rada saba zitakazosaidia wataalamu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), kutoa taarifa mapema zaidi za majanga yanayohusiana na hali ya hewa.
Inakadiriwa kutokana na miundombinu na rada tano zilizopo mikoa ya Mwanza, Dar es Salaam, Dodoma, Mtwara na Kigoma, zaidi ya asilimia 94 za taarifa na tahadhari ya hali ya hewa inayotolewa na TMA ni sahihi.
Akizungumza leo Jumatano Agosti 28, 2024 kwenye mafunzo ya matumizi ya rada katika utabiri wa hali ya hewa yaliyoanza Agosti 26 na yatakamilika Agosti 30, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema kutokana na usahihi wa taarifa hizo, wananchi wasipuuze tahadhari za majanga ya hali ya hewa zinazotolewa ili kupunguza athari.
“Katika utabiri wa hali ya hewa rada ni kifaa ambacho kinatupa utabiri mzuri wa hali ya hewa hasa kwa kulitambua hilo Serikali imewekeza fedha nyingi kuzinunua.
“Kuwa na rada ni jambo jingine lakini kuweza kutafsiri hizo data ni jambo jingine, hawa wataalamu wetu tunawapa course (mafunzo) ili baada ya kupata zile picha za rada waweze kuzichambua na kupeleka ujumbe mapema kuhusu janga linaloweza kutokea la hali ya hewa,”amesema Profesa Mbarawa.
Katika mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani (WMO), Profesa Mbarawa amesema licha ya rada hizo kuongeza tija kwenye utoaji mapema wa taarifa za hali ya hewa pia zitasaidia kufanya uchambuzi wa kina wa masuala ya utabiri wa hali ya hewa ili matokeo chanya yapatikane nchini.
“Watanzania tukipewa ule utabiri wa hali ya hewa tupokee kuzingatia…Tusiwe tukiambiwa utabiri wa hali ya hewa kesho msiende kuvua mkasema aah hakuna kitu…Utabiri wa hali ya hewa tupo nao sasa ni zaidi ya asilimia 94, tukikwambia kesho kuna mvua nyingi lazima zitatokea kwa hivyo naomba Watanzania wenzangu tukipewa utabiri wa hali ya hewa tuupokee, tuuzingatie na tuufanyie kazi,” amesema.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu TMA na Makamu Mwenyekiti wa jopo la kimataifa la sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, Dk Ladislaus Chang’a amesema jumla ya wataalamu wa utabiri wa hali ya hewa 82 kutoka nchi 12 za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika watapewa mafunzo kwaajili ya matumizi sahihi ya rada.
Dk Chang’a amesema miundombinu iliyowezeshwa na Serikali pamoja na umairi unaofanywa na watalamu wa TMA umewezesha kuimarisha ubora na usahihi wa utabiri ambao unasaidia kupunguza majanga na athari zake nchini, akiwataka wananchi kuendelee kutumia taarifa ya hali yahewa kwa maendeleo endelevu.
Kuhusu rada mbili zinazotarajiwa kuingia nchini 2025, amesema zitaendelea kuongeza ubora akidai maono yao makubwa ni nchi kuwa sehemu ya mafunzo ya rada barani Afrika.
“Kwahiyo kuongezeka kwa rada kuna tafsiri kubwa kwa sababu pale tutakapoomba mafunzo yafanyike tutakuwa tunaonesha ni jinsi gani Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika miundombinu ya rada,” amesema Dk Chang’a.
Mshiriki wa mafunzo hayo kutoka nchini Burundi, Alexandre Ntahondi amesema mafunzo hayo yatawawezesha kutumia rada nchini mwao, kuwatahadharisha majanga na kuwanufaisha wananchi.