Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeiweka njia panda hatima ya kufunguliwa kesi ya Kikatiba ya kupinga Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kusimamia uchaguzi wa Serikali za mitaa baada ya kuibua pingamizi dhidi ya shauri la maombi ya ridhaa ya kufungua kesi hiyo.
Shauri hilo la maombi ya ridhaa ya kufungua kesi kupinga uchaguzi huo kusimamiwa na Tamisemi limefunguliwa na wanaharakati watatu, ambao pia wanaojitambulisha kuwa ni raia waliosajiliwa katika Daftari la Kidumu la Wapiga Kura.
Waombaji hao ni Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Bob Wangwe, mwanahabari mstaafu, Ananilea Nkya na Bubelwa Kaiza na wajibu maombi ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Katika shauri hilo la maombi namba19721/21, waombaji wanaomba Mahakama iridhie wafungue shauri la kupinga pamoja na mambo mengine, uchaguzi wa serikali za mitaa kusimamiwa na Tamisemi badala ya Tume Huru ya Uchaguzi
Shauri hilo linalosikilizwa na Jaji Wilfred Dyansobera leo Jumatano, Agosti 28, 2024, lakini limekwama kusikilizwa baada ya Serikali kuibua pingamizi la hoja za kisheria.
Kiongozi wa Jopo la Majibu Maombi, Wakili wa Serikali Mkuu, Mark Mulwambo ameieleza Mahakama baada ya kupitia nyaraka za shauri hilo wamebaini kuna mambo ya kisheria ambayo yanapaswa yaamuriwe kwanza kabla ya kusikiliza shauri hilo.
“Kwa sababu hiyo, tumeleta mapingamizi manne ambayo mahakama yako inapaswa kuyafanya kazi ili kama itakubaliana nayo basi tusipoteze muda na kama haitakubaliana nayo basi tuendelee na usikilizwaji. Sisi tuko tayari kuendelea na usikilizwaji wa mapingamizi haya,” amedai Mulwambo.
Kiongozi wa Jopo la mawakili wa waombaji, Mpale Mpoki, amesema wamepewa mapingamizi hayo leo mchama na kwamba hivyo wanaomba muda kama jopo la mawakili wa waombaji waweze kuyapitia, ili kulitendea haki na akaomba usikilizwaji ufanyike Keshokutwa Ijumaa ya Agosti 30, 2024.
Pia, Mpoki amependekeza pingamizi hilo lisikilizwe sambamba na maombi ya kibali ili kuokoa muda.
Hata hivyo, Wakili Mulwambo alipinga hoja hiyo ya kusikilizwa Ijumaa bali akapendekeza usikilizwaji ufanyike kesho Alhamisi ya Agosti 29, 2024.
Wakili Mulwambo amedai kwa mujibu wa sheria wa sheria shauri hilo linapaswa lisikilizwe na kuamuriwa ndani ya siku 14, na kwamba shauri hilo limefunguliwa chini ya hati ya dharura, hivyo hakuna haja ya kusogeza mbele.
Wakili mwingine wa waombaji, Dk Rugemeleza Nshala amesisitiza kuongezewa muda ili wasikilizwe Ijumaa pamoja na mambo mengine akidai wanahitaji kupata muda hata wa kuwaandaa wateja wao, ili Mahakama itende kwa usawa.
Hata hivyo, Jaji Dyansobera baada ya kusikiliza hoja zote ameamuru pingamizi hilo lisikilizwe Jumatatu asubuhi ya Septemba 2, 2024 sambamba na shauri la maombi ya ridhaa huku akielekeza waombaji wawasilishe Mahakamani majibu yao kesho Alhamisi.
Mbali na Mpoki na Dk Nshala, mawakili wengine wa waombaji ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, Jebra Kambole, Peter Madeleka, Edson Kilatu na Paul Kisabo.
Kwa upande wa wajibu maombi mbali na Wakili Mulwambo, pia kulikuwa na mawakili wengine saba na kufanya idadi yao kuwa wanane.