Sheria kuipa nguvu zaidi TAA, kusimamia viwanja vyote vya ndege

Dodoma. Bunge limepitisha muswada unaoanzisha Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) ambayo sasa sasa itakuwa na jukumu la kusimamia viwanja vyote vya ndege hata vile vidogo ‘airstrip’.

Muswada huo uliopitishwa na Bunge ukisubiri kutiwa saini na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa sheria kamili, pia unataka marekebisho ya sheria, ili TAA iwe na wafanyakazi wake wa zimamoto.

Kwa sasa ilivyo TAA inamiliki vifaa vya zimamoto, lakini wafanyakazi wanatoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, hali inayosababisha ugumu katika masuala ya kinidhamu na kiutawala.

Kabla ya muswada huo, TAA ilikuwa ikitekeleza majukumu yake kama wakala chini ya Sheria ya Wakala wa Serikali, Sura ya 245, na kusimamiwa na Bodi ya Ushauri ambayo ina mamlaka finyu.

Muswada unaipa TAA jukumu la uanzishaji, uendelezaji, usimamizi, uendeshaji na utunzaji wa viwanja vya ndege na kuondoa utata wa kampuni binafsi kuendesha viwanja vya ndege. Mfano, mgogoro uliokuwapo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Muswada huo uliowasilishwa bungeni na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa umeweka masharti yanayolenga kuhakikisha viwanja vya ndege vinavyomilikiwa na Serikali vinasimamiwa na kuendeshwa kwa kuzingatia viwango vya udhibiti vilivyowekwa.

Pia, TAA ipewa wajibu wa kuhakikisha kunakuwapo usalama katika viwanja vya ndege, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa huduma za zimamoto na uokoaji, udhibiti wa wanyama na ndege.

Profesa Mbarawa amesema kutakuwa na Bodi ya Wakurugenzi, mamlaka ya Bodi, uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu na masuala mengine yanayohusu maofisa na watumishi wa mamlaka.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Moshi Kakoso, akiwasilisha maoni ya kamati hiyo amesema ilitathmini hali halisi ya uratibu wa huduma za zimamoto na uokoaji, hivyo imependekeza kufanyike upembuzi wa kina kubaini namna bora za kisheria zitakazowezesha TAA kuwa na kikosi cha kukabiliana na moto na kuongeza weledi utakaokidhi viwango vya kimataifa.

Mbunge wa Kyela, Ali Mlagila amesema sheria mpya ya TAA inakwenda kuviweka viwanja vya ndege chini ya TAA.

“Sheria hii inaenda kuleta sura ya umiliki wa viwanja vya ndege na inaenda kutengeneza usalama mkubwa tofauti na ilivyokuwa nyuma.

“Hapo nyuma kulikuwa na viwanja vingine ambavyo kila mtu alikuwa anaviendesha kwa jinsi anavyojua yeye, kuna wawindaji wako huko porini walikuwa wanaendesha ‘airstrips’ ambazo hazitambuliki na TAA, kwa sheria hii viwanja vyote hivyo vitaenda kuwa chini ya TAA,” amesema.

Mbunge huyo amesema kupitia sheria hiyo masuala kama ya Kadco (Kampuni ya Uendelezaji na Uendeshaji Kiwanja cha Ndege cha Kilimanjaro) yanaenda kufa.

“Hakuna mtu atakayeleta matatizo yaliyotokea hapo katikati, wala atakayelalamika kwa nini sasa kuna Kadco halafu kuna TAA. Hata Kadco ikiwepo itakuwa chini ya TAA, kama itakuwa kuna manufaa na itahitajika kuwa hivyo, lakini ambaye tutakuwa tunamuuliza atakuwa ni TAA,” amesema.

Amesema sheria hiyo itaimarisha utendaji kwa maana inakwenda kuifanya TAA kuwa mtendaji mkuu anayeweza kufanya biashara bila kuingiliwa na kuingiza kipato.

“Katika hili tunaomba sana kusisitiza Serikali ihakikishe inaifanya TAA ifanye biashara zake kama kampuni nyingine, kama mawakala wengine.

“Nizungumzie pesa ambayo abiria wanalipa kwa ajili ya viwanja vya ndege si kwamba hatuiamini TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania), tunaiamini sana, tunachotaka ni kuishauri Serikali ichukue hili kuwa iwe ni mapato ya TAA ifanye mambo yake kwa uharaka.

“Tunaiomba Serikali iache TAA iwe na zimamoto yake, haiwezekani magari ni ya TAA, vifaa vyote vya uokoaji ni vya TAA, lakini kinachotokea wafanyakazi wanavyoviendesha, eti wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, hii haikubaliki katika uwajibishaji inakuwa ni ngumu,” amesema.

“Tunaomba TAA waendeshe zimamoto zao kwa sababu hata mafunzo ya uzimaji wa moto na uokoaji ni tofauti na unavyozima nyumba ikiwaka moto.

“Kwa hiyo tunaomba hiki kitengo kijitegemee na wawe na uwezo kukiendesha na kuwajibishana ili huyu meneja anayeendesha awe na mamlaka ya wafanyakazi wake, sasa tunamnyima mamlaka yake,” amesema.

Mbunge wa Kilombero, Abubakari Asenga, amesisitiza suala la uokoaji na usalama katika viwanja vya ndege, akisema TAA wawe na wafanyakazi wao.

“Sasa kumekuwa na changamoto kubwa, muingilianao wa Jeshi la Zimamoto, tuna mfano wa moto uliotokea Bandari ya Tanga, pale walipokwenda kuhojiwa Mamlaka ya Bandari, sisi kama kamati ilionekana dereva wa zimamoto alikuwa amepangiwa majukumu mengine na kiongozi wake wa zimamoto wa kijeshi.

“Kuwe na kikosi maalumu chini ya mamlaka ya viwanja vya ndege wataweza kusimamia, kuwajibishana na kujua bajeti ya viwanja vya ndege katika kuboresha uzimaji moto na uokoaji.

“Mfano, TAA inanunua gari la zimamoto kwa Sh1.5 bilioni, lakini linanunua kwa ajili ya Jeshi la Zimamoto ambalo liko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Tunashauri Wizara za Mambo ya Ndani, ya Uchukuzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakae waone ni utaratibu gani mzuri wa kutengeneza kikosi ambacho mkurugenzi mkuu wa TAA anaweza kutoa maelekezo kukiboresha kutokana na bajeti yake,” amesema.

Related Posts