Dar es Salaam. Tanzania imekusudia kuifanya Brazil kuwa miongoni mwa nchi 10 zinazoleta watalii wengi nchini kutokana na kuwa na idadi kubwa ya watu.
Brazil ambayo mwaka huu inakadiriwa kuwa na watu zaidi ya milioni 212 tayari mawakala wake wa utalii, vyombo vya habari kutoka nchi hiyo wamekuja nchini ili kuangalia vivutio mbalimbali vinavyopatikana kabla ya kuanza kuleta wageni.
Hayo yameelezwa leo Agosti 27, 2024 na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Hassan Abbas baada ya kumaliza mazungumzo aliyoyafanya na ujumbe wa mawakala wa utalii na vyombo vya habari kutoka nchini Brazil.
Dk Abbas amesema ujio wa wageni hao ni matokeo ya jitihada ya utangazaji wa vivutio unaofanywa na nchi ikiwemo mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika maeneo mbalimbali.
“Wanajifunza wao kwanza kabla ya kuleta watalii, tuko nao Dar es Salaam baadaye watakwenda Arusha huko watatembelea Serengeti, Ngorongoro Tarangire, maeneo ya utamaduni na pia watakwenda Zanzibar. Wameonyesha utayari wa kuanza kuleta watalii,” amesema Dk Abbas.
Ujumbe huo unakuja nchini kuangalia vivutio kwa ajili ya soko lao wakati ambao Tanzania imerekodi idadi ya watalii milioni 1.9 hadi mwishoni mwa Mei mwaka huu kwa mujibu wa ripoti ya tathimini ya mwezi iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Balozi wa Tanzania nchini Brazil, Profesa Adelardus Kilangi amesema ujio wa wageni hao ni matokeo ya makongamano yaliyoandaliwa nchini mwao Aprili mwaka huu.
Kwa upande wake mratibu wa ujumbe huo kutoka nchini Brazil, Luciana Teixeina amesema wanaamini kwa kushirikiana na ubalozi wao wataiwezesha nchi hiyo kuwa miongoni mwa nchi 10 zinazoleta watalii wengi Tanzania.
“Tayari tumeona kuna hoteli nzuri, miundombinu, tunakwenda kuangalia vivutio vilivyopo na sisi tutakwenda kuwafumbua macho watu wetu ili waanze kuitazama Tanzania kama sehemu ya kwenda kufurahia mapumziko,” amesema Luciana.