Tanzania inaunga mkono mkakati wa kikanda wa usalama wa afya na dharura kwa kipindi cha 2022–2030 kupitia hatua za utekelezaji wa miradi muhimu, kuanzisha mpango wa wafanyakazi wa afya ya jamii ulio jumuishi na kuratibiwa, na kupanga kwa ajili ya kurejesha na kuimarisha mifumo ya afya iliyoathiriwa na janga la COVID-19.
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Agosti 28, 2024 wakati akitoa taarifa ya Tanzania kwenye ajenda ya kipengeke cha 12 kwenye kikao cha 74 cha Shirika la Afya Duniani (WHO-AFRO) ambacho kinajadii mbinu bunifu za kuimarisha muundo wa Kimataifa wa maandalizi na mwitikio wa dharura za kiafya katika Kanda ya Afrika ya WHO.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaunga mkono na inatambua taarifa zilizotolewa na inapongeza Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa mafanikio yake bunifu katika kuimarisha maandalizi na mwitikio wa dharura za kiafya katika Kanda ya Afrika ambapo inakadiriwa kuwa na matukio 102 kila mwaka.” Amesema Waziri Mhagama
Waziri Mhagama amesema, kwa kuendana na mkakati huo, Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuboresha uwezo wa kugundua, kujiandaa, na kuitikia dharura za kiafya (EPR) ambapo amependekeza zichukuliwe jitihada za kuanzisha, kuhamasisha, na kutetea matumizi ya vituo vya umahiri na vituo vya maandalizi na mwitikio wa dharura katika Kanda ndogo wakati wa dharura za kiafya.
“Hili limeonyeshwa na ufanisi wetu katika kushughulikia mlipuko wa ‘Marburg Virus Disease’ mwaka 2023 na matokeo chanya ya tathmini ya pamoja ya nje ya pili (JEE) iliyofanyika mwezi Agosti 2023.” Amesema Waziri Mhagama
Aidha, Waziri Mhagama amesema, kutokana na ongezeko la mara kwa mara na ugumu wa dharura, Tanzania inahimiza WHO kuendelea kutoa msaada wa kimkakati na kiutendaji ili kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika tathmini za hatari za mipakani, ufuatiliaji, ujasusi wa magonjwa, pamoja na usambazaji wa taarifa kwa wakati.
“Pia tunaiomba WHO kuhamasisha usaidizi wa washirika na kuhimiza ufadhili wa ndani ili kukabiliana na changamoto za rasilimali kwa miradi muhimu na operesheni za mwitikio.” Amesema Waziri Mhagama