Trump na Harris kushiriki mdahalo wa televisheni Septemba 10 – DW – 28.08.2024

Hata hivyo hakukuwepo uthibitisho juu ya maafikiano hayo kutoka kwa makamu wa rais Kamala Harris.

Donald Trump ameandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth kwamba wapinzani hao wamekubaliana kuwa mdahalo huo kwenye kituo cha televisheni cha ABC News utaendeshwa chini ya sheria sawa na mdahalo wa kituo cha CNN uliofanyika mnamo Juni 27, bila kuwepo watu jukwaani na kipaza sauti cha kila mgombea kuzimwa wakati mwenzake anapozungumza.

Licha ya kukishtumu kituo cha televisheni cha ABC News kwa kuna na upendeleo, Trump amesema kituo hicho kimempa hakikisho kwamba mdahalo huo utakaofanyika mjini Philadelphia, utaendeshwa kwa njia ya haki na usawa.

Soma pia: Robert F. Kennedy Jr asitisha kampeni ya urais, amuidhinisha Trump

Wakati huo huo, makamu wa rais Kamala Harris na gavana wa Minnesota Tim Walz, wamekubali kufanya mahojiano yao ya kwanza ya pamoja.

Wanasiasa hao watafanyiwa mahojiano na kituo cha televisheni cha CNN katika jimbo la Georgia siku ya Alhamisi.

Mahojiano hayo yatakuwa ya kwanza ya kina na chombo cha habari tangu Rais Joe Biden alipojiondoa kwenye kinyang’anyiro cha urais zaidi ya wiki tano zilizopita na kumuidhinisha Kamala Harris kama mbadala wake.

Marekani I Donald Trump - Uchaguzi 2024 - Bozeman
Mgombea urais wa chama cha Republican Rais wa zamani Donald Trump akihutubia mkutano wa kampeni huko BozemanPicha: Janie Osborne/AP/picture alliance

Tangu apewe nafasi ya kuipeperusha bendera ya chama cha Democrat, wapinzani wake Republican wamemkosoa kwa kuonekena kuepuka mahojiano na vyombo vya habari na wamemtuhumu pia kwa kuwaacha wapiga kura gizani juu ya mipango yake iwapo atachaguliwa kuwa rais.

Wachambuzi wanasema mahojiano hayo yatakuwa mtihani wa kwanza kwa Harris na Walz kama wagombea wenza, japo yatatoa fursa ya moja kwa moja kuzima sauti za wakosoaji wao.

Pia yanatimiza ahadi aliyoitoa Kamala Harris ya kufanya mahojiano na vyombo vya Habari kabla ya mwisho wa mwezi huu.

Soma pia: DNC: Kamala Harris aihimiza Marekani kuchukua mwelekeo mpya 

Mahojiano hayo na kituo cha televisheni cha CNN yanatokea baada ya hotuba walizozitoa wakati wa kongamano la kitaifa la chama cha Democrat lililofanyika mjini Chicago- hafla iliyoandaliwa kwa ustadi wa hali ya juu.

Mara baada ya mahojiano hayo, Kamala Harris amepanga kufanya ziara katika jimbo lenye ushindani mkubwa la Georgia ili kunadi sera zake.

Mahojiano hayo ni mojawapo ya fursa adimu kwa wapiga kura nchini Marekani kusikia kwa undani zaidi juu ya sera za tiketi ya Harris na Walz kuelekea uchaguzi mkuu wa mwezi Novemba.

 

Related Posts