Waziri mkuu wa Uingereza Keir Starmer amesema anataka kuanzisha ukurasa mpya wa mahusiano na Umoja wa Ulaya, lakini akisisitiza kwamba nchi yake haiwezi kurudi ndani ya Umoja huo wa Ulaya.
Kiongozi huyo wa Uingereza amefanya mazungumzo mjini Berlin na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, ambako pia ameahidi kufikia makubaliano mapya ya ushirikiano na Ujerumani.
Keir Starmer ameweka wazi mipango yake ya kutaka kurejesha mahusiano mazuri na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya akiitaja kwanza azma ya kuingia kwenye makubaliano mapya na Ujerumani kama sehemu ya mkakati mpana wa kutengeneza tena mahusiano yake na Umoja wa Ulaya.
Ameridhia kusaini makubaliano na Ujerumani kufikia mwishoni mwa mwaka huu baada ya kuzungumza na Kansela Olaf Scholz hii leo, akiita kuwa fursa ya kipekee kwa nchi yake Uingereza.
“Kama ilivyoonekana leo, Uingereza inaweza kutanuwa maslahi yake kwa ufanisi ikiwa tunasimama pamoja na marafiki na washirika wetu. Mkataba huu ni sehemu ya mpango mpana wa kuanzisha msingi wa kuleta mwamko mpya wa ushirikiano kwa kuwepo maelewano ya pamoja, ambayo yataimarishwa kwa kasi na tunataraji kufikia makubaliano kufikia mwishoni mwa mwaka huu. Kurudi kwenye Jukwaa la Umoja wa Ulaya,ni mwanzo mpya kwa Uingereza katika mahusiano yetu na kuyatambuwa tena maslahi yetu ya pamoja ni kutimiza ahadi yetu ya pamoja kwa watu wetu.”
Waziri mkuu huyo wa Uingereza amesema makubaliano mapya kati ya nchi yake na Ujerumani yatafunguwa ushirikiano mkubwa zaidi katika masuala ya sayansi,teknolojia,maendeleo,jamii,biashara,utamaduni na hata kuimarisha kwa kiwango cha juu mahusiano ya kibiashara kati ya pande hizo mbili.
Soma pia: Starmer afanya ziara Berlin kujadili mkataba na UjerumaniMwenyeji wake mjini Berlin, Kansela Olaf Scholz amempongeza kwa kuchukuwa mwelekeo huo wa kutaka tena urafiki na mahusiano mema na Umoja wa Ulaya,akisisitiza kwamba Uingereza na Ujerumani toka hapo walikuwa ni marafiki wa karibu na wenye kuaminiana.
”Nimefurahishwa na tangazo la Starmer kwamba ataanzisha mahusiano mapya na Umoja wa Ulaya. Tunataka kuupokea mkono huu tulionyooshewa. Uingereza siku zote imekuwa sehemu muhimu ya utatuzi wa masuala makubwa yanayoiathiri Ulaya nzima. Hilo halijabadilika tangu ilipoondoka kwenye Umoja wa Ulaya.”
Lakini pia Kier Starmer ametia mkazo kwamba Uingereza haiwezi kurudi katika soko la pamoja au umoja wa forodha ingawa itakuwa na mahusiano ya karibu yanapohusika masuala kadhaa ikiwemo ya kiuchumi na kiulinzi.Soma Pia: Keir Starmer: Mpango wa kuwapeleka wahamiaji Rwanda umekufa
Kansela Scholz na waziri mkuu Starmer pia wamekubaliana kuanzisha mpango wa pamoja wa kukabiliana na uhamiaji haramu kupitia njia ya kuvuka bahari ambapo huenda,mpango huo ukahusisha maafisa watakaopewa jukumu la kuzizuia boti zinazovuka kupitia mataifa mbali mbali ya Ulaya na kuelekea kaskazini mwa Ufaransa.
Viongozi hao pia wamelijadili suala la Ukraine na wote wawili wamesema hakuna maamuzi mapya yaliyofikiwa,sio London wala Berlin kuhusu namna ya matumizi ya silaha zilizopelekwa Ukraine. Ikumbukwe kwamba Ukraine imekuwa ikiutia kishindo Umoja wa Ulaya,Uingereza na Marekani kuipatia idhini ya kutumia silaha ilizopokea kushambulia ndani ya ardhi ya Urusi.