Tabora. Wakati bodi ya tumbaku nchini ikiendelea kuhamasisha wakulima wapya kujiunga na ulimaji wa zao hilo, baadhi yao wamehoji upatikanaji wa haraka wa malipo wakidai kipindi cha nyuma ilimlazimu mkulima kusubiri hadi mwaka mmoja ndiyo apate malipo yake.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne Agosti 27, 2024, Vicent Maduhu mkazi wa kijiji cha Kamahalanga Nzega, amesema licha ya kuacha kilimo hicho kwa muda mrefu changamoto iliyokuwa ikiwakabili ni malipo kuchelewa.
“Mimi nilikua mkulima wa zao hili lakini baadaye niliacha kwa kuwa ilichukua hadi mwaka mzima kupewa malipo ya kile ulichovuna na mpaka sasa tumeona kuna hamasa inaendelea, ila utaratibu wa malipo umefanyiwa kazi kwa kiasi gani” amehoji Maduhu.
Amesema wakulima wengi katika kata yao wameacha kulima tumbaku baada ya kuona wanazungushwa kulipwa fedha zao baada ya kuuza tumbaku yao.
“Sasa Serikali inatakiwa kuwaambia wakulima ni namna gani watapata fedha zao baada ya kuvuna kwa kuwa tumbaku kwa sasa inauzika,” amesema Maduhu.
Naye John Benjamini mkazi wa Nzega amesema amelima zao hilo kwa muda mrefu lakini amebaini katika eneo analoishi, wakulima wengi hawana mitaji jambo linalowafanya kurudi nyuma katika uzalishaji.
“Hapa ninapokaa wengi wanatamani kulima tumbaku lakini hawana mitaji, maana ili ulime tumbaku ya uhakika, lazima upate pembejeo za uhakika pamoja na uwepo wa mabani ya kukaushia, tunaziomba mamlaka kutuwezesha wakulima ili tuweze kuingia kwenye kilimo hiki pamoja na kupewa uhakika wa malipo yetu pale uvunaji unapokamilika,” amesema mkulima huyo.
Akilizungumzia hilo, Said Ntahondi ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Tumbaku Tanzania, kuelezea kuhusu kusuasua kwa malipo ya wakulima kwa miaka ya nyuma, alithibitisha kuwepo kwa changamoto hiyo.
“Ni kweli kulikua na changamoto ya wakulima kucheleweshewa malipo yao na ikasababisha wengi kuacha kulima zao hili, maana changamoto hiyo ilifanya uzalishaji ukashuka kutoka kilo milioni 120 hadi kilo milioni 60 jambo ambalo lilikua baya kwenye kilimo hiki” amesema.
Hata hivyo, amesema baada ya uwepo wa changamoto hiyo Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imefanya mabadiliko makubwa kwenye malipo ya wakulima hao.
Amesema tumbaku ikivunwa hivi sasa na ikapelekwa sokoni, malipo hufanyika ndani ya siku saba mpaka 14.
“Kwa hiyo wakulima wasiwe na hofu, ndani ya siku hizo fedha hupelekwa kwenye akaunti ya Amcos na zitawafikia moja kwa moja,” amesema.
Kwa upande wake Jerry Nashon, Ofisa Ushirika wa Wilaya ya Nzega, amewataka wakulima kujiunga na vyama vya ushirika kwa lengo la kupata urahisi wa kupewa pembejeo za kilimo.
“Wakulima wa tumbaku hapa Nzega nawashauri mjiunge na vyama vya ushirika kwenye maeneo yenu ili muweze kupata fursa za kukopeshwa pembejeo za kilimo kama mbolea na mbegu, ili kilimo mnachofanya kiwe cha tija tofauti na hali ilivyo sasa,” amesema.