Bunda. Watu watatu wamefariki dunia na wengine 13 kujeruhiwa, baada ya gari walilokuwa wamepanda kupata ajali katika Kijiji cha Sanzate wilayani Bunda Mkoa wa Mara.
Ajali hiyo imehusisha gari aina ya Hiace iliyokuwa imebeba waombolezaji wakielekea katika Kijiji cha Mugeta wilayani Bunda kwa ajili ya maziko.
Akizungumza kwa njia ya simu, Diwani wa Nyamuswa Ibrahim Mganga amesema ajali hiyo imetokea leo Jumatano Agosti 28,2024 saa 9 alasiri.
“Gari lilikuwa na waombolezaji 16 wakielekea Mugeta kwa ajili ya mazishi lakini walipofika katika eneo hilo tairi la nyuma lilipasuka hivyo gari kukosa mwelekeo,” amesema.
Amesema katika ajali hiyo watu wawili wamefariki papo hapo, huku mmoja akifariki baada ya kufikishwa hospitalini.
Amesema majeruhi wamepelekwa katika Kituo cha afya Ikizu pamoja na hospitali teule ya wilaya ya Bunda zilizoko wilayani Bunda.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Salim Morcase amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo, ambapo amesema waombolezaji hao walikuwa wakielekea katika kijiji cha Mugeta wilayani Bunda kwa ajili ya mazishi.
“Mwili wa marehemu umechukuliwa katika hospitali ya Manispaa ya Musoma leo na gari lililohusika kwenye ajali ni gari binafsi na sio gari la abiria, dereva anashikiliwa wakati mmiliki anasakwa,” amesema.
Amesema ajali hiyo imetokea baada ya tairi la mbele la kushoto kupasuka kwa pamoja na tairi la nyuma hivyo gari kukosa mwelekeo.
Ajali hii imetokea siku tatu baada ya ajali nyingine iliyohusisha Hiace iliyokuwa imebeba abiria ikitokea mjini Mugumu wilayani Serengeti kuelekea mjini Bunda kupata ajali katika Kijiji cha Kyandege wilayani Bunda.
Katika ajali hiyo iliyotokea Agosti 25,2024 watu tisa walifariki dunia na wengine 20 kujeruhiwa huku chanzo cha ajali kikielzewa kuwa ni mwendokasi uliopelekea tairi la nyuma kupasuka kisha gari kupinduka mara kadhaa.
Baada ya ajali hiyo dereva aliyejulikana kwa jina la Emmanuel Matoto alitoroka na hivyo kupelekea polisi kuanza msako wake huku likimshiikilia mmiliki wa gari hilo, Sospeter Kamoga.