WATENDAJI WA UBORESHAJI WA DAFTARI WATAKIWA KUWEPO VITUONI MUDA WOTE

Mwenyekiti Wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe.Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele, akizungumza wakati akifunga mafunzo ya siku mbili kwa Waratibu wa Uandikishaji wa mkoa, Maafisa Waandikishaji, Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ugavi na Maafisa TEHAMA wa halmashauri yaliyoanza jana Agosti 26 na kumalizika leo Agosti 27, 2024 Mkoani Mkoani Mara.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Bw. Kailima Ramadhani, akizungumza wakati wa mafunzo ya siku mbili kwa Waratibu wa Uandikishaji wa mkoa, Maafisa Waandikishaji, Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ugavi na Maafisa TEHAMA wa halmashauri yaliyoanza jana Agosti 26 na kumalizika leo Agosti 27, 2024 Mkoani Mkoani Mara.

***************Na Mwandishi wetu

Watendaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wametakiwa kuwepo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura muda wote hata kama hakuna waombaji wa kujiandikisha vituoni.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele wakati akifunga mafunzo kwa watendaji wa uboreshaji ngazi ya mkoa wa Mara na halmashauri za mkoa huo.

Amesema watendaji wa vituo wanapaswa kuwepo vituoni muda wote kuanzia saa mbili kamili asubuhi hadi saa 12 kamili jioni kila siku katika siku saba za kujiandikisha zilizowekwa na Tume.

“Muda wa kufungua na kufunga kituo uwe ni ule uliopangwa ili waombaji wanapohitaji kuja kituoni kujiandikisha watukute kituoni,” amesisitiza Mhe. Mwambegele.

Tukio kama hilo la kufunga mafunzo limefanyika pia mkoani Simiyu ambako Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Magdalena Rwebangwira amewataka watendaji hao kufuatilia kwa karibu zoezi hilo ili lifanikiwe, kutoa kipaumbele kwa makundi mbalimbali na kuwa makini katika usambazaji na utunzaji wa vifaa.

Akifunga mafunzo ya watendaji Mkoani Manyara, Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Asina Omari kwa upande wake amehimiza uhamasishaji wa wapiga kura na kuwa Tume inatarajia wapiga kura halali tu ndio wapatiwe kadi za mpiga kura.

“Mnahimizwa kuhamasisha wananchi wenye sifa ili wajitokeze kujiandikisha na kupata haki yao ya kikatiba itakayowawezesha kushiriki kuwachagua viongozi wao. Aidha ni matarajio ya Tume kuwa baada ya zoezi hili kukamilika watu watakaopatiwa kadi watakuwa ni wapiga kura halali,” amesema Jaji Asina.

Mafunzo haya yanafanyika ikiwa ni maandalizi ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mzunguko wa nne unaojumuisha mkoa wa Mara, Simiyu na baadhi ya halmashauri za Mkoa wa Manyara ambazo ni Halmashauri ya Mji wa Babati na Halmashauri za Wilaya za Babati, Hanang na Mbulu ambapo uboreshaji utaanza tarehe 04 Septemba, 2024 hadi 10 Septemba, 2024 na vituo vitakuwa vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.

Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama Kuu Asina Omari akizungumza wakati akifunga mafunzo hayo mkoani Manyara.

Sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo kutoka mkoa wa Manyara.

Meza Kuu wakiwa katika picha wakati wa kufunga mafunzo kwa mkoa wa Manyara.
Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Magdalena Rwebangira akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo kwa upande wa Mkoa wa Simiyu.

Washiriki wakisikiliza kwa makini hotuba ya kufunga mafunzo.

Washiriki kutoka Mkoa wa Simiyu wakishiriki mafunzo kwa vitendo.

Related Posts