MSHAMBULIAJI wa Coastal Union, Mbaraka Yusuph amesema licha ya kutolewa katika hatua za awali kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF), lakini hawajatoka patupu.
Coastal ilitolewa katika mashindano hayo baada ya kufungwa nyumbani na ugenini jumla ya mabao 3-0 na Bravos do Maquis ya Angola, jambo ambalo mchezaji huyo kalichukua kama funzo la kujituma zaidi katika ligi.
“Hakuna kitu kinauma kama kuondolewa hatua za awali katika michuano hiyo. Pamoja na hayo yote hatuna budi kujua kipi kilituangusha ili tufanye vizuri mechi za Ligi Kuu,” alisema.
Aliongeza kuwa, “kwa mechi za Ligi Kuu zilizochezwa zimetoa taswira jinsi ambavyo msimu huu ni mgumu. Unahitaji kujituma ili timu kupata matokeo ya ushindi.”
Kwa upande wake anatamani msimu uwe wa mafanikio ya kufunga mabao mengi, tofauti na uliopita ambapo akiwa Kagera Sugar alimaliza na mabao matano.
“Nikipata nafasi ya kufunga na kutoa asisti, litakuwa jambo bora zaidi kwangu, kwani litapandisha thamani yangu,” alisema.
Mbali na hilo, amesema tangu aanze kucheza Ligi Kuu Bara mchezaji anayemuona kwamba hachuji ni Erasto Nyoni wa Namungo.