Aliyeiua Namungo mzuka umepanda | Mwanaspoti

BAADA ya kucheza mechi ya kwanza Ligi Kuu Bara baada ya kukosekana kwa takribani mwaka mmoja na nusu, huku akifunga bao lililowapa Tabora United ushindi, beki wa kushoto Salum Chuku, amesema licha ya kikosi chao kuchelewa kuanza maandalizi lakini ana imani kitafanya vizuri msimu huu.

Chuku aliyejiunga na Tabora United kwenye dirisha kubwa akitokea Mwadui FC, aliiwezesha timu hiyo kupata ushindi wa mabao 2-1 mbele ya Namungo huku akifunga bao la ushindi baada ya kukosekana kwenye ligi hiyo kwa takribani msimu mmoja akiuguza majeraha ya mkono.

Chuku aliliambia Mwanaspoti kwamba ushindi walioupata ulitokana na kufanyia kazi mapungufu yaliyosababisha wakapoteza mchezo wa kwanza kwa mabao 3-0 mbele ya Simba, huku uwepo wa baadhi ya mastaa wao wa kimataifa waliokamilisha masharti ya vibali ukiwapa nguvu.

Alisema kikosi chao kilihitaji ushindi huo ili kuwa na mwanzo mzuri kwenye ligi na kurudi mchezoni, huku wakipanga kutumia mapumziko ya takribani wiki mbili kupisha mechi za kimataifa, kujiimarisha na kuboresha kikosi chao ambacho bado kinatafuta muunganiko.

“Nilifurahi kufunga bao na kuisaidia timu yangu kupata pointi tatu nawashukuru wachezaji wenzangu wote na benchi la ufundi kwa ushirikiano tunaopeana kwa namna tunavyoenda kwa umoja huu naamini tutaendelea kufanya vizuri,” alisema Chuku

“Kitu cha kwanza tulichofanya ni kuhakikisha tunapunguza makosa tuliyofanya mchezo wa kwanza na tulipata nafasi ya kutumia wachezaji wote ikatuongezea nguvu na kukawepo mabadiliko hii iliweka utulivu kwenye timu,” allisema “Kwahiyo kikosi kilitimia na kuwa vile ambavyo mwalimu anataka na Mungu akatusaidia tukapata ushindi. Tulichelewa kuanza maandalizi ya ligi kwahiyo tutatumia nafasi hii kuendelea kujiandaa na kujiweka vizuri zaidi.”

Related Posts