Dodoma. Mwili wa Michael Richard (36) aliyeuwa kwa kupigwa na watu wasiojulikana umeagwa na kusafirishwa kwenda wilayani Kongwa kwa maziko, huku mke na watoto wake wanne wakishindwa kuhudhuria kutokana na kuuguza majeraha hospitalini.
Tukio hilo lilitokea Mtaa wa Mbuyuni, Kata ya Kizota wilayani Dodoma usiku wa kuamkia jana Agosti 28.
Baada ya Michael kuuawa, mke na watoto kujeruhiwa, nyumba waliyokuwa wakiishi ilichomwa moto.
Katika tukio hilo, Agnes Yared (34) ambaye ni mke wa Michael na watoto wake, Ezra (8), Witnes (6), Ephraim Michael (3) na Glory Michael (1) walijeruhiwa na wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Ibada ya kuaga mwili wa Michael imefanyika katika Kanisa la Anglikana lililopo Mtaa wa Mbuyuni, Kata ya Kizota. Maziko yamefanyika leo Agosti 30, Kibaigwa mkoani Dodoma.
Akizungumza katika ibada ya kuaga mwili wa Michael, Diwani wa Kata ya Kizota, Jamal Ngalya amesema haingii akilini majirani wasisikie vilio vya familia hiyo wakati wakipigwa na watu hao wasiofahamika.
“Nawaza mtoto mdogo anashikiwa fimbo anachapwa anaweza kulia ulioko mita 400 unasikia, mlio jirani mlishindwa kusikia vilio vya watoto. Huyu bwana naambiwa alikuwa anatoka Bahi (Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma) kaanza kuona, je angechelewa si tungeua watu wote mle ndani?” amehoji.
Ametoa ushauri kwa Polisi Kata kushughulika na mfumo wote wa majirani, akisema watu hawawezi kufanya ukatili wa namna hiyo lakini wakabaki wanawaangalia.
“Hili naomba niwaambie nitalifuatilia na mkutano wangu nitakaoufanya nitawaambia na tutajua nani kafanya,” amesema Ngalya huku akitokwa machozi.
Mwinjilisti wa Kanisa la Anglikana Mtaa wa Mbuyuni, Gershom Mbele amesema wanaomboleza kwa sababu ya ukatili uliofanyika katika mtaa huo, na kuwa jambo hilo linalopaswa kupaziwa sauti ni Kanisa kwa kuwataka watu waache uovu na dhambi.
“Hawajui kuwa iko hukumu ambayo inawasubiri. Ukiua kwa upanga lazima ufe kwa upanga. Neno la Mungu ni amini na kweli huwa halidanganyi,” amesema.
Amesema hivi sasa watu wanaogopa binadamu kuliko wanyama kwa kuwa wamekuwa ni hatari na kirusi kibaya kuliko wanyama.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma, Dk Sara Ludovick amesema majeruhi wanne wanaendelea vizuri.
“Jana tulipowapokea majeruhi wawili kati ya wanne walikuwa hawana fahamu lakini leo wamepata fahamu zao na wote wanaendelea na matibabu kama kawaida,” amesema.
Amesema Agnes na mtoto mmoja walikuwa hawana fahamu lakini leo wote wanafahamu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi jana Agosti 28 alisema tukio hilo lilitokea saa 9.00 usiku na kwamba, Michael alivamiwa nyumbani kwake na kupigwa na kitu chenye ncha butu kichwani na kusababisha kifo chake. Pia walimjeruhi mke na watoto wake.
Alisema uchunguzi wa awali unaonyesha chanzo cha tukio hilo ni kulipa kisasi. Alisema msako unaendelea.