CCM yaagiza ujenzi hospitali Temeke ukamilishwe

Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimeiagiza Manispaa ya Temeke kusimamia ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Temeke iliyopo Mbagala Rangi Tatu ukamilike kwa wakati ili kutoa huduma kwa wananchi Dar es Salaam na mikoa ya jirani.

Agizo hilo limetolewa leo Alhamisi Agosti 29, 2024 na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla wakati akikagua ujenzi wa hospitali hiyo uliofikia asilimia 60 ukitarajiwa kukamilika Juni 2025.

Amesema ujenzi huo ukikamilila utakuwa na manufaa makubwa ikiwemo huduma za matibabu bingwa na kwa wananchi wa maeneo ya Mbagala na mkoa wa Pwani na utapunguza msongamano katika hospitali ya Rufaa ya Temeke.

“Mradi huu naufahamu nikiwa Mkuu wa Mkoa (Dar es Salaam), nilisimamia mchakato wa kumpata mkandarasi, kilichotushawishi kuijenga mahitaji ya kuwa na Hospitali ya Wilaya Temeke itakayotusaidia kupunguza mzigo wa wananchi.

“Tunashukuru Serikali kuridhia Mbagala kuwa na hospitali ya kisasa yenye ghorofa sita. Hii itakuwa hospitali ya mfano endelea kusimamia kwa kasi, maana mmeniambia inakamilika Juni 2025, mliyemuadi ni mwenezi na mlezi wa CCM Dar es Salaam, maana yake kufuatilia ni kazi nyepesi,” amesema Makalla.

Amewaambia uongozi wa Temeke na mkandarasi anayejenga mradi huo, kwamba Oktoba 2024 CCM ina jambo lake hivyo wafanye hima kukamilisha ujenzi utakaokuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa Mbagala katika kupata huduma za matibabu.

Makalla amemtaka pia mkandarasi anayekeleza ujenzi huo kuhakikisha anazingatia mahitaji ya watu maalumu watakaokwenda kufuata huduma katika hospitali ili ujenzi wa ghorofa usiathiri kundi hilo.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Dk Jonas Lulandala amesema ujenzi huo ukikamilika utawezesha wananchi kupata huduma za kibingwa, huduma za upasuaji kuanzia watu saba hadi 14 kwa siku na kuwezesha wajawazito kujifungua kuanzia 30 hadi 40 kwa siku.

Amesema thamani ya ujenzi huo ni zaidi ya Sh10 bilioni ambapo pia ikamilika itakuwa na wodi ya wazazi, wanawake, watoto na wanaume sambamba na kupunguza rufaa zisizo za ulazima kwenda Hospitali ya Temeke.

Mbunge wa Mbagala, Abdallah Chaurembo ameishukuru Serikali ya kutekeleza mradi huo, ambao ukikamilika utawanufaisha wananchi wa jimbo hilo, akisema kila mwaka halmashauri ya Temeke inaweka fedha za kufanikisha ujenzi huo.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Mtemvu amemuahidi Makalla kuifuatilia miradi yote ambayo mwenezi huyo alifanya ziara ya kukagua kisha kumpa mrejesho.

Related Posts