Ethiopia imeelezea wasiwasi huo baada ya Misri ambayo kwa muda mrefu imekuwa katika msuguano na nchi hiyo kutuma vifaa vya kijeshi nchini Somalia katika hatua ambayo huenda ikazidisha mvutano kati ya mataifa hayo mawili ya Ethiopia na Misri.
Ethiopia yasema haiwezi kukaa kimya amani ya kanda inapoyumbishwa
Katika taarifa, wizara ya mambo ya nje ya Ethiopia imesema kwamba kanda hiyo inaingia katika hali hatari na kuongeza kuwa nchi hiyo haiwezi kukaa kimya huku wahusika wengine wakichukuwa hatua za kuyumbisha amani ya eneo hilo.
Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa Ethiopia inafuatilia matukio hayo.
Haikubainika wazi mara moja kile kilichotumwa na Misri nchini Somalia lakini balozi wa Somalia nchini Misri Ali Abdi jana aliitaja shehena hiyo kuwa muhimu.
Hatua ya Misri ni mwanzo wa utekelezaji wa matokeo ya mkutano wa Cairo
Katika taarifa, Abdi alisema kwamba hatua hiyo ya Misri ni ya kwanza ya kiutendaji katika kutekeleza matokeo ya mkutano wa kilele uliofanyika hivi karibuni kati ya Misri na Somalia mjini Cairo nchini Misri kati ya Rais wake Hassan Sheikh Mahmoud na mwenzake wa Misri Abdel Fattah El-Sisi.
Misri itakuwa nchi ya kwanza kupeleka vikosi vyake Somalia
Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Somalia, Abdi ameongeza kuwa Misri itakuwa nchi ya kwanza kupeleka vikosi vyake Somalia kusaidia kuboresha usalama wa nchi hiyo baada ya kuondoka kwa kikosi cha sasa cha Umoja wa Afrika kinachojulikana kama ATMIS, kinachojumuisha vikosi vya Burundi, Djibouti, Ethiopia, Kenya na Uganda, na ambacho kitakamilisha shughuli zake nchini humo na kukabidhi kikamilifu majukumu ya usalama kwa jeshi na polisi wa nchi hiyo kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
Ujumbe huo mpya wa AUSSOM, unatarajiwa kuanza kutekeleza majukumu yake mwezi Januari mwaka 2025.
Ethiopiaimeonya kuwa hatua hiyo ni ya hatari na kuishutumu Somalia kwa kushirikiana na washirika ambao hawakutajwa kuyumbisha amani ya eneo la Pembe ya Afrika.
Misri na Ethiopia zimekuwa katika mvutano kwa miaka mingi
Kwa miaka mingi, Misri na Ethiopia zimekuwa katika mvutano na kurushiana maneno ya uchochezi juu ya mradi wa bwawa kubwa la Ethiopia kwenye Mto Blue Nile, ambalo Misri inasema linatishia usalama wake wa maji.
Kwa muda mrefu, Misri imekuwa ikichukulia bwawa hilo lenye thamani ya dola bilioni 4.2 kama tishio lililopo, kwani inategemea Mto Nile kwa asilimia 97 ya mahitaji yake ya maji.
Soma pia:Misri yaionya Ethiopia kuhusu matumizi ya mto Nile
Mazungumzo ya muda mrefu juu ya bwawa hilo tangu 2011 hadi sasa yameshindwa kuleta makubaliano kati ya Ethiopia na majirani zake wanaozungukwa na mto huo.
Uhusiano kati ya Somalia na Ethiopia pia ulivunjika baada ya Ethiopia mwezi Januari kufikia makubaliano na eneo lililojitenga la Somalia, Somaliland kuiruhusu Ethiopia kutumia sehemu yake ya bahari.