Jaji Frank Mahimbali wa Mahakama Kuu kanda ya Sumbawanga, ametumia msemo wa sasa wa mashabiki wa timu ya Simba wa ‘Ubaya Ubwela’ kufananisha sakata la watoto wawili wa familia moja wanaogombea jina la Kura.
Jaji alisema usemi huo unaomaanisha ‘ubaya umerudi tena’, kwa mtazamo wa kwanza, mtu anaweza asithamini suala la uhalifu linalowahusisha wawili hao, wakiwa ndugu, kiasi cha kukabana koo kwa matumizi ya majina hayo.
Hata hivyo, akitoa hukumu iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP) dhidi ya Kasanda Mayuma au Machimu, Jaji alikubaliana na sababu za rufaa hiyo na kueleza kuwa kwa ushahidi uliopo,Kasanda ana hatia ya makosa manne ya jinai.
Kulingana na hukumu hiyo aliyoitoa Agosti 26,2024, Jaji Mahimbali ameyataja makosa hayo kuwa ni kutoa taarifa za uongo kwa mtumishi wa umma, kula kiapo cha uongo, kujifanya ni Kura na kujipatia usajili wa ardhi kwa njia ya udanganyifu.
Hukumu ya Jaji Mahimbali inatokana na rufaa iliyokatwa na DPP kupinga hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Bariadi ya kumwachia huru mrufani kwa maelezo kwa ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri ulikuwa haujathibitisha mashtaka hayo.
Sakata lenyewe lilivyokuwa
Katika sakata hilo, shahidi wa kwanzawa Jamhuri katika kesi iliyokuwepo Mahakama ya Wilaya ya Bariadi, ambapo Kura Mayuma Machumu alidai jina hilo ni lake, lakini ndugu yake naye, Kasanda Mayuma Machimu nayea akadai ni lake.
Kwa hiyo Kura akadai ndiye mmiliki wa kiwanja namba 10 na 11 Block L eneo la Kidinda huku Kasanda naye akijaribu kuzima umiliki huo kwa kuwasilisha nyaraka za ardhi akijifanya yeye ndio Kura na baadaye ambaye anasomeka kwenye nyaraka.
Mchezo ulianzaje? Ilielezwa kortini kuwa Septemba 16,2021 katika ofisi ya mtendaji wa mtaa wa Majengo katika Wilaya ya Bariadi, Kasanda alitoa taarifa za uongo kwa Diana Kabando kuwa yeye ndio Kura Mayumu Machimu.
Kwamba nyaraka za ardhi yake (ya Kura) ambazo ni hati za umiliki wa viwanja hivyo ziliungulia ndani ya nyumba hivyo akamuomba amwandikie barua itakayompatia taarifa ya upotevu wa mali (loss report) katika kituo cha Polisi.
Hii kwa mujibu wa ushahidi huo, ingemsaidia kupata hati mpya ya umiliki wa viwanja hivyo wakati akifahamu fika kuwa taarifa alizokuwa ametoa ni za uongo.
Hakuishia hapo, kwani Septemba 22,2021 akiwa mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi Mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Bariadi, Caroline Kiliwa, alikula kiapo kuwa ameamua kuachana na jina la Kura na sasa ataiitwa Kasanda Mayuma Machimu.
Mbali na hivyo akapeleka hati ya kisheria (deed poll) ya kubadili majina kwa Msajili wa Hati akijifanya kuwa yeye mwanzo alikuwa anaitwa Kura na sasa amebadili jina na atajulikana kwa jina la Kasanda Mayuma Machumu.
Kama hiyo haitoshi, mjibu rufaa huyo afanikiwa kupata hati mya ya umiliki wa viwanja hivyo yenye namba 77693 kwa viwanja namba 4 na 5 Block L Kidinda ambavyo vinamilikiwa kihalali na ndugu yake aitwaye Kura Mayuma Machimu.
Kutokana na matenda hayo, mrufani alikamatwa na kufunguliwa mashitaka hayo manne ambayo aliyakanusha na kuulazimisha upande wa Jamhuri kuita mashahidi 8, ili kuthibitisha mashitaka dhidi ya mrufani ambaye ni ndugu na Kura.
Shahidi wa kwanza, Kura Mayuma, alieleza baada ya kugundua kwamba nyaraka zake za umiliki wa ardhi zimechezewa, alienda Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kulalamikiwa viwanja vyake kubadilishwa umiliki kinyemela.
Katika ushahidi huo, ulienda mbali ambapo wakala wa vitambulisho vya Taifa (Nida), walieleza kuwa kumbukumbu zilizopo katika mifumo yao, zilithibitisha Kura Mayuma na Kasanda Mayuma ni watu wawili tofauti kwa kila hali.
Shahidi kutoka Nida alieleza kuwa wawili hao wanatofautiana kuanzia tarehe ya kuzaliwa, picha na alama za vidole na hiyo ilitosha kumaliza ubishi kuwa ni mtu mmoja huku ndugu wawili nao wakipigilia msumari kuwa ni watu wawili tofauti.
Katika utetezi wake kortini mbele ya mahakama ya Wilaya ya Bariadi, Kasanda alisema majina yake ya awali aliyopewa na wazazi wake ni Kura Mayuma Machimu na kwamba ilipofika mwaka 2021 alianza kutumia Kasanda Mayuma Machimu.
Aliongeza kusema kuwa viwanja namba 10 na 11 kitalu L ni vyake na alivipata tangu mwaka 1993 na kwamba vina majina ya Kasanda Mayuma Machimu na Kura Mayuma Machimu na kwamba nyumba yake iliungua na nyaraka zote kuungua.
Kwa ufahamu wake, anajulikana kwa majina yote mawili na baada ya ajali ya moto na baada ya kuwasilisha ripoti ya polisi ya kupotelewa na mali kwenye ofisi ya ardhi, alipewa nyaraka mpya zilizokuwa na majina Kasanda Mayuma Machimu.
Kuhusu kama yeye ni Kura Machimu, kulikuwepo na shahidi wa pili wa utetezi ambapo aliunga mkono alichokisema baba na kusema ndio maana yeye (mtoto) anaitwa Aron Kura Machimu lakini hakutoa cheti za kuzaliwa wala kitambulisho.
Mahakama yamwachia, DPP akata rufaa
Mahakama ya wilaya ya Bariadi baada ya kupima ushahidi wa Jamhuri na ule wa utetezi, ilihitimisha kuwa upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha mashitaka na kuacha mashaka na kumwachia huru mrufani katika kesi hiyo.
DPP hakuridhishwa na hukumu hiyo ambapo alikata rufaa akiegemea sababu 10, moja akisema hakimu alikosea kisheria aliposema shitaka la kwanza la kutoa taarifa za uongo kwa ofisa wa umma halikuthibitishwa wakati lilithibitishwa.
Hoja nyingine ni kuwa hakimu alifanya makosa ya kisheria kwa kuamua kuwa hati ya mashitaka ilikuwa na dosari kwa kutoonyesha ni aya ya ngapi katika kifungu cha 122 cha kanuni ya adhabu kilikiukwa bila kueleza ni nini hasa hakikuonyeshwa.
Pia DPP alisema Hakimu huyo alikosea kisheria pale alipojichanganya kwamba shitaka la kwanza halikuthibitishwa wakati huo huo katika hukumu hiyo hiyo alikiri kuwa kosa hilo lilithibitisha kikamilifu na mashahidi wa upande wa mashitaka.
DPP alilalamika kuwa hakimu huyo alikosea kisheria alipoamua kuwa jina la Kura Mayuma linaloonekana kwenye Nida lilianza kutumika mwaka 2023 bila kuzingatia fimu ya Nida iliyoonyesha lilianza kutumika tangu mwaka 2019.
Kwa ujumla wake, DPP alisema hakimu huyo alikosea kisheria kwa kushindwa kuainisha ipasavyo ushahidi wa mashahidi mbalimbali wa Jamhuri ambao walithibitisha pasipo kuacha mashaka, kuwa Kasanda alitenda makosa hayo.
Hukumu ya Jaji ilivyokuwa
Katika hukumu yake, Mahimbali alianza kwa kusema hiyo ilikuwa ni rufaa ya kushangaza ambapo ndugu wawili wanapigana kwa mapembe na kukabana koo kwa sababu ya kugombea jina na jina lenyewe ni Kura Mayuma Machimu.
“Usemi wa sasa wa mashabiki wa Simba uliobatizwa kwa jina la Ubaya Ubwela au Ubaya umerudi tena ndio unaweza kutumika kuelezea sakata hili. Mwanzo mtu anaweza asithamini suala la uhalifu lililopo katikati ya ndugu hao,”alisema Jaji.
Hata hivyo, baada ya Jaji kuchambua sababu za rufaa na mawasilisho ya pande, anaona mrufani huyo alifikishwa mbele ya mahakama kwa makosa manne ambayo kwa hitimisho lake, anaona makosa yote manne yalithibitishwa.
Kwa uchambuzi na uzito wa ushahidi alioupitia na kuuchambua, anaamuru kufutwa kwa amri ya mahakama ya Wilaya ya Bariadi kuwa mrufani hakuwa na hatia kwa kuwa maamuzi hayo ya hakimu yalifikiwa kimakosa.