Kituo cha Sheria Tanzania chazindua ripoti ya haki – DW – 29.08.2024

Pamoja na mambo mengine ripoti hiyo imeonesha kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za kazi, asilimia 51 ya watu wakiripoti kunyimwa fursa ya kufanya kazi, wengi wao wakiwa ni wanawake na watu wenye ulemavu.

Ripoti hiyo ya haki za binadamu imemulika zaidi changamoto zinazoendelea katika maeneo ya kazi, mazingira na biashara.

Kuvunjwa mikataba na kutopewa mikataba bado ni tatizo

Imebainisha kuwa asilimia 69.4 ya wafanyakazi waliripoti kuwa na mikataba ya ajira ikiwa ni ongezeko kidogo ikilinganishwa na asilimia 64.6 ya mwaka 2022.

Mwanamke akiwa katika shughuli ya upanzi wa miti Tanzania
Mwanamke akiwa katika shughuli ya upanzi wa miti TanzaniaPicha: Sascha Quaiser

Hata hivyo malalamiko kuhusu uvunjwaji wa mikataba na kutopatiwa nakala za mikataba ya ajira bado ni mengi.

Mkurugenzi wa kituo hicho cha sheria na haki za binadamu LHRC Dr. Anna Henga amesema hata hivyo kwamba wanawake na watu wennye ulemavu ni kundi linalotengwa katika ajira.

Changamoto za ardhi

Kwa upande mwingine changamoto zilizoainishwa katika umiliki wa ardhi ni pamoja na ucheleweshwaji wa malipo ya fidia kwa ardhi inayochukuliwa kwa matumizi mengine, uthamini wa ardhi usioakisi gharama za maisha pamoja na kutoshirikishwa ipasvyo kwa jamii wakati wa utwaaji wa ardhi kwaajili ya shughuli za uwekezaji hasa katika maeneo yenye viwanda vya uziduaji.

Maoni ya baadhi ya wananchi kuhusiana na changamoto zilizoibuliwa katika ripoti hiyo ya haki za binadamu, ni serikali kuyashughulikia mapungufu yaliyobainishwa.

Kituo cha LHRC kinasema haki za binadamu ni msingi wa biashara endelevu na mwongozo wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 2011, unaolenga kulinda, kuheshimu na kurekebisha haki za binadamu katika biashara.

Related Posts