Dar es Salaam. Wakati Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla akisema kuna mabasi 200 yaendayo haraka yanayoyotarajiwa kuanza kazi katika barabara ya Mbagala, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), Dk Athuman Kihamia amesema hayo ni maelekezo ya Serikali.
Makalla ameeleza hayo leo Alhamisi Agosti 29, 2024 akiwahutubia wananchi wa Mbagala katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Maturubai wilayani Temeke, baada ya kufanya ziara ya siku 10 katika wilaya tano za Mkoa wa Dar es Salaam.
“Hii miundombinu ya barabara imekalimilika muda mrefu tangu nikiwa mkuu wa mkoa wa hapa (Dar es Salaam), nimefuatilia, niseme nisiseme? Mwenezi wenu nina habari nimefuatilia na wamenihakikishia wapo katika hatua ya mwisho kuleta mabasi 200 Desemba ili yaanze kufanya kazi,” amesema Makalla.
Ameongeza kuwa, chama hicho tawala, kimezungumza na Serikali kuhusu mwenendo wa mradi huo na kuhakikishia kuwa utaanza Desemba kwa mabasi 200 ya kuanzia akiwataka watumiaji wa barabara hizo kuwa watulivu.
Hata hivyo, Mwananchi lilipomtafuta Dk Kihamia na kumuuliza kuhusu kauli hiyo, amesema kwa kuwa imetolewa na kiongozi wa juu wa CCM, ndiyo maelekezo ya Serikali.
“Kilichoelezwa na Makalla ndiyo maelekezo ya Serikali, hawezi kuongea kitu kisichokuwepo,” amesema.
Mei 4, 2024 mwaka huu, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tamisemi, iliigomea Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) iliyotaka kuanza huduma katika barabara ya Mbagala (Kilwa) ifikapo Februari 2025, lakini kamati hiyo ilikataa ikisema ni mbali.
Kamati hiyo iliwataka Dart ihakikishe mradi huo uanze mwaka huu, kwa ujenzi wa miundombinu yake ulishakamilika kwa asilimia 98.9 kwa mujibu wa bosi wa taasisi hiyo, Dk Kihamia aliyewaambia wajumbe wa kamati kwamba wanamsubiri mzabuni kuleta mabasi hayo.
Katika hatua nyingine, Makalla ameitaka Tamisemi na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kukaa meza moja na kuangalia namna ya kumaliza changamoto ya vibanda ili mradi wa mabasi ya mwendokasi uanze.
“Wote ni Serikali naomba mkae pamoja mzungumze mmalize mgogoro ili mwendokasi ukianza pachangamke na watu wafanye biashara,”amesema Makalla ambaye ni mlezi wa CCM mkoani wa Dar es Salaam
Kada wa zamani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa amewataka wakazi wa Dar es Salaam kukiunga mkono CCM akisema kimejipambanua kuwaletea maendeleo tofauti na vyama vingine.
“Nilipotea kwenda Chadema, sasa na nyinyi (wananchi) sitaki mpoteee kwa kujiunga na vyama vya upinzani,” amesema Mchungaji Msigwa aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa inayojumuisha mikoa ya Mbeya, Njombe, Iringa, Songwe na Rukwa.