Manaibu gavana Kenya walalamikia kutokuwa na kazi – DW – 29.08.2024

Manaibu Gavana hao wakiongozwa na Naibu Gavana wa Laikipia Reuben Kamuri wanasema magavana wengi wanawakabidhi wasaidizi wao wakuu majukumu yao na kuwaacha wao bila kazi.

Manaibu wa magavana hao wamefika mbele ya kamati ya bunge la Seneti inayosimamia masuala ya ugatuzi ambapo wamewasilisha ombi la kutaka kubadilishwa kwa sheria ya usimamizi wa serikali za kaunti ili kubainisha majukumu na mipango wanayopaswa kusimamia kwenye serikali za kaunti. 

Majukumu ya kusimamia mipango panapotokea majanga

Reuben Kamuri, Naibu Gavana wa Laikipia amesemawanataka washirikishwe katika utekelezaji wa mipango akihoji kuwa kuna baadhi ya maazimio ambayo hupitishwa kwenye mabaraza ya mawaziri kwenye serikali za kaunti na hakuna anayewafuatilia mawaziri kuhakikisha yametekelezwa.

“Kazi ya kamati ndogo zinazobuniwa, mipango inayotekelezwa kwenye kaunti na usimamizi wa kuhakikisha serikali ya kaunti inatoa huduma ipasavyo tayari ni jukumu kubwa sana. Na unapaswa kuwa macho kuwasimamia na kuhakikisha mawaziri wanatekeleza majukumu yao,” alisema Kamuri.

Janga la mafurikon kaunti ya Kajiado, Kenya
Janga la mafurikon kaunti ya Kajiado, KenyaPicha: Thomas Mukoya/REUTERS

Wamesema wanataka wapewe majukumu kama vileya kusimamia mipango ya kujiandaa kwa majanga, na kuongoza kamati zote ndogo za serikali za kaunti.

Suali lingine tata waliloliibua ni kuhusu bajeti za ofisi zao. Wanataka idhini itolewe ya kupitishwa kwa bajeti zao ili kuboresha jukumu lao la usimamizi. Lakini Mohammed Abbas, mwenyekiti wa kamati ya ugatuzi ya bunge la Seneti anahoji kwamba:

“Mnaposema mnataka kuwa na majukumu na kisha mnataka mpewe bajeti ya ofisi, inakanganya kwa kuwa bajeti hiyo itakuwa chini ya ofisi ya magavana,” alisema Abbas. 

Bajeti ya manaibu gavana

Kumekuwepo na matukio nchini ambapo baada ya magavana na manaibu wao waliowachagua kugombea ofisi nao wanaanza kutofautiana pindi wanapoingia madarakani. Matukio kama haya yamewafanya baadhi ya magavana na manaibu wa magavana kuondolewa madarakani kwa mashtaka ya usimamizi mbaya wa ofisi.

William Oduol, ni naibu gavana wa kaunti ya Siaya ambaye mwaka jana aliepuka kuondolewa madarakani baada ya kura ya kukosa imani na utendakazi wake ilipopitishwa na bunge la kaunti ya Siaya wakati alipotofautiana na Gavana wake James Orengo.

“Nafikiri ni muhimu kututengea mgao wa kiwango chochote, iwe asilimia 2 au 30, kutoka kwenye bajeti inayoundwa kwa ajili ya ofisi ya magavana,” alisema Oduol.

Kamati ya seneti kuhusu ugatuzi imepapokea mapendekezo hayo na itawasilisha ripoti mbele ya bunge wakati seneti itakaporejelea vikao vyake mwezi ujao.

Related Posts