Mapya yaibuka maandamano ya wananchi Simiyu

Simiyu. Zikiwa zimepita siku nane tangu wakazi wa Mji Mdogo wa Lamadi Wilaya ya Busega mkoani Simiyu, wafanye maandamano ya kupinga ukimya wa Jeshi la Polisi kushughulikia matukio ya kupotea watoto, wafanyabiashara wamewatuhumu baadhi ya askari kupora na kuiba mali zao wakati wa vurugu hizo.

Hata hivyo, alipotakiwa kuzungumzia malalamiko hayo leo Alhamisi Agosti 29 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Edith Swebe amesema tayari mwenyekiti wake wa ulinzi na usalama mkoa (RC), ameshalizungumzia na kulitolea maagizo.

Maandamano hayo yaliyofanyika Agosti 21, mwaka huu, yalisababisha vurugu, uharibifu wa mali na kifo cha mwanafunzi, Meshack Paul (20) aliyeuawa kwa kupigwa risasi na polisi wakati wa kudhibiti maandamano hayo.

Tuhuma hizo zimeibuliwa na wananchi jana  jioni Jumatano Agosti 28, 2024 mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kenani Kihongosi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Sokoni Mjini Lamadi.

Wakazi hao wamedai uporaji wa mali na fedha ulifanywa na baadhi ya askari kwa kivuli cha kukamata watu wanaodaiwa kuhusika na maandamano hayo.

Baadhi ya wakazi hao wakitoa malalamiko mbele ya Kihongosi, wamedai licha ya uwepo wa kituo cha polisi, kimeshindwa kuwasaidia kufanyia kazi ripoti na malalamiko wanayoyapeleka.

Wamemuomba Kamanda Swebe kuwaondoa askari wote kituoni hapo.

Masuka Bangili, mkazi wa Kitongoji cha Makanisani, amedai kuwa wakati wa maandamano hayo, polisi walishindwa kutimiza majukumu yao ya kudhibiti vurugu badala yake wakawa wanafanya uhalifu wa kupora mali na fedha za wafanyabiashara.

“Haya yote yametokana na kupuuzwa kwa malalamiko ya kinamama waliopotelewa na watoto, lakini cha ajabu ni Jeshi la Polisi kutumia risasi za moto kudhibiti wananchi waliokuwa kwenye maandamano, hiki Kituo cha Polisi Lamadi …. unapeleka malalamiko yako hayafanyiwi kazi,” amedai Bangili.

Mfanyabiashara katika mji huo, Joseph Mtua amedai kuwa, wakati akiwahudumia vinywaji wateja dukani kwake, polisi walifika na kumkamata kisha kumpandisha kwenye gari lao na kuacha duka likiwa wazi bila uangalizi wowote.

“Baadaye walitoka askari wengine watatu na kuingia dukani kwangu wakafungua droo ya meza ninayotunzia fedha za mauzo ya biashara yangu wakachukua Sh600,000 na kuchukua vinywaji vilivyokuwa kwenye friji. Sisi wafanyabiashara katika vurugu hizi za Lamadi tumeathirika sana,” amedai Mtua.

Mfanyabiashara, Maria Lutabu amedai kuwa, baada ya mabomu ya machozi kupigwa alijifungia kwenye kibanda chake cha biashara kilichopo eneo la sokoni, lakini askari walifika wakavunja mlango na kuingia ndani na kuanza kumpiga huku wakisema ‘kumbe ni mwanamke.’

Amedai askari hao walimpora fedha zake zilizokuwa kwenye mkoba.

Mkazi mwingine wa Lamadi, Frola Balele amedai kuwa, mtoto wake ambaye ni mwanafunzi wa shule ya msingi alikamatwa na kupelekwa kituo cha polisi akiwa na Sh5,000 ambazo alinyang’anywa, huku akiomba arudishiwe fedha hizo.

Hata hivyo, mkuu wa mkoa huo, Kihongosi alimpatia Sh5,000 mama huyo kwenye mkutano huo.

Naye, Salome Justine amedai kuwa, polisi walivunja mlango wa nyumba yake na kuingia ndani na kuanza kuwapiga.

“Hili zoezi la kutuliza ghasia lilijaa vitendo vya uhalifu vilivyofanywa na Jeshi la Polisi ambalo limepewa dhamana ya kulinda raia na mali zao,” amesema Justine.

Akizungumzia tuhuma hizo, Kihongosi amewataka wananchi wenye ushahidi usio na shaka kuhusu kuporwa fedha na mali zao na askari wakati wa maandamano hayo, wapeleke malalamiko yao kwa kamanda wa polisi mkoa ili uchunguzi uanze mara moja.

Kihongosi amesema hakuna mtu aliye juu ya sheria huku akiwaahidi wakazi hao kuwa polisi watakaobainika kufanya uhalifu huo, watachukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria.

“Kuna mambo lazima yapatiwe mwarobaini, Serikali haijawahi kushindwa jambo, ndiyo maana tumesema hapa usalama ni kipaumbele chetu cha kwanza, vyombo vinapoleta taarifa fulani viacheni vifanye kazi.”

“Yale mapungufu ambayo mmeyatoa kuvunjiwa na kuporwa, hayo tunashughulika nayo na RPC amehihakikishia watasimamia hilo na wale wote mliotoa malalamiko yenu mmeripoti kwa RPC tutasimamia na haki zenu mtazipata,” amesema Kihongosi.

Katika hatua nyingine, mkuu wa mkoa amewataka wananchi wa Lamadi kutotumiwa na wanasiasa kwa masilahi yao binafsi, bali walinde amani na kudumisha utulivu.

Amesema zinapotokea changamoto kama hizo washirikiane kuzipatia ufumbuzi kuliko kusababisha vurugu.

“Msikubali kugombana na Serikali yenu, msikubali kupingana na Serikali yenu kwenye mapungufu tuambieni, kwenye shida elezeni na viongozi wanapokuja wasikilizeni na iwapo hamtaridhika mnakwenda ngazi nyingine ya juu,” amesema mkuu huyo wa mkoa.

Related Posts