Mawaziri 70 kujadili uvuvi, uchumi wa buluu Dar

Dar es Salaam. Mawaziri 70 kutoka mataifa wanachama wa Umoja wa Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) wanatarajia kukutana kwa siku tano nchini kujadili uchumi wa buluu na kuweka mkakati wa pamoja kuimarisha sekta ya uvuvi.

Mkutano huo utakwenda sanjari na kongamano la kimataifa kuhusu mikakati ya Uboreshaji wa Mnyororo wa Uzalishaji wa Vyakula vya Majini ulioandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Shirika la Chakula Duniani la Umoja wa Mataifa (FAO).

Hayo yamesemwa leo Agosti 29, 2024 na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega wakati akizungumza na waandishi kuhusu mkutano huo unaotarajiwa kufanyika kati ya Septemba 9 hadi 13 mwaka huu.

Ulega amesema Rais Samia Suluhu Hassan ndiye anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya ufunguzi huku Rais wa Zanzibar akifunga mkutano huo.

Amesema lengo la mkutano huu wa nane wa mawaziri wa OACPS ni kujadili sekta ya uvuvi katika nchi wanachama ikiwa ni pamoja na kuweka mkakati wa pamoja wa sera wa uvuvi na ufugaji wa viumbe maji ili kuimarisha sekta ya uvuvi katika kuchangia uchumi wa nchi wanachama.

“Pia, mkutano huo utatumika kama jukwaa jumuifu litakolokutanisha watunga sera na watalaamu wetu na wenzao kutoka mataifa wanachama ili kujadili fursa na changamoto zilizopo kwenye uchumi wa buluu na hatimae kujifunza mikakati ya kutatua changamoto hizo,” amesema Ulega.

Amesema uwepo wa mkutano huo nchini utafungua fursa za uwekezaji kwenye uchumi wa buluu hususan kwenye maeneo makuu mawili ya uvuvi na ufugaji samaki.

Jambo hilo litaendelea kuboresha mahusiano ya matumizi ya rasilimali za maji ya asili na zile za ukuzaji viumbe maji, baina ya wadau wetu wale wa mataifa wanachama.

 “Pia wigo wa masoko ya nje ya mazao yetu ya uvuvi, kuongeza uwanda mpana wa wavuvi wetu kujifunza namna ya kuendesha shughuli zao kwa tija, kujenga mahusiano mema kimataifa, na zaidi sana kuvutia uwekezaji kwenye eneo la uvuvi wa bahari kuu,” amesema.

Related Posts