Muswada sheria hifadhi ya jamii kicheko kwa wanachama

Dodoma. Bunge limepitisha muswada wa marekebisho ya sheria za hifadhi ya jamii wa mwaka 2024, ambapo sasa mwanachama wa mfuko atalipwa mafao bila kujali kama mwajiri amekamilisha kuwasillisha michango kwenye mfuko ama la.

Hii ni tofauti na ilivyokuwa awali, mwanachama alipostaafu na kama mwajiri hakukamilisha michango alitakiwa kufuatilia ikamilike kwanza, hoja iliyoibua maswali mengi kwa wabunge katika vikao tofauti wakihoji ni kwa nini mstaafu anahangaishwa.

Muswada huo uliopitishwa leo Agosti 29, 2024 pia utamruhusu mwanachama ambaye hajafikia umri wa kustaafu kutumia sehemu ya mafao yake kama dhamana kwa mkopo wa nyumba.

Marekebisho mengine ni kuruhusu mfanyakazi aliyeajiriwa na mwajiri zaidi ya mmoja kuchangiwa na waajiri wote kwa ridhaa yake, kama ilivyo kwa madaktari wanaofanya kazi katika zaidi ya hospitali moja.

Muswada huo wa sheria unaruhusiwa mnufaika wa mafao ambaye kwa kipindi husika anatumikia kifungo gerezani, kuridhia kwa maandishi kwamba mafao yake au sehemu yoyote ya mafao yake ilipwe kwa mnufaika atakayetajwa kama vile familia yake.

Pia mnufaika aliyepata ajali au tatizo lolote anaweza kudai mafao wakati wowote, baada ya kuondolewa ukomo wa muda.

Marekebisho hayo yalisomwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, alipowasilisha muswada huo uliosomwa bungeni kwa mara ya pili na ya tatu na hatimaye marekebisho yanayopendekezwa yawe sehemu ya sheria za nchi.

Muswada huo umefanya marekebisho katika Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii, Sura ya 50, Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma, Sura ya 371 na Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi, Sura ya 263.

“Kifungu cha 33 kinapendekezwa kurekebishwa kwa kufuta neno ‘thirty three’ (33) na kuweka neno ‘thirty six’ (36). Lengo la marekebisho haya ni kuongeza kiwango kinacholipwa kwa wategemezi pale ambapo mwanachama atakuwa amefariki,” amesema.

Amesema kifungu cha 12A kinapendekezwa kuongezwa ili kuruhusu mfanyakazi aliyeajiriwa na mwajiri zaidi ya mmoja kuchangiwa na waajiri wote kwa ridhaa yake.

“Lengo la marekebisho haya ni kumpa mwanachama uhuru wa kuchangiwa na zaidi ya mwajiri mmoja,” amesema akitoa mfano wa madaktari wanaofanya kazi kwenye hospitali zaidi ya moja kuchagua mwajiri yupi achangie au wote wachangie.

Amesema vifungu vya 52 na 76 vimerekibishwa kumruhusu mwanachama ambaye hajafikia umri wa kustaafu kutumia sehemu ya mafao yake kama dhamana kwa mkopo wa nyumba.

“Lengo la marekebisho haya ni kutoa ufafanuzi kwa kuwa vifungu hivyo vinazuia matumizi ya mafao kama dhamana ya mkopo,  isipokuwa kwa mkopo wa nyumba kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 20,” amesema.

Ridhiwani amesema kifungu cha 24 kimefutwa na lengo la marekebisho hayo,  ni kuondokana na dhana iliyojengwa katika kifungu hicho inayoruhusu mwanachama kutoa kiasi cha mchango wake katika mfuko wa hifadhi ya jamii na kuondolewa uanachama, kwani inakinzana na kanuni za hifadhi ya jamii kutokana na dhana ya kifungu hicho kutumiwa kwenye mfuko wa akiba na siyo katika mfuko wa hifadhi ya jamii.

“Kifungu cha 45 kinapendekezwa kurekebishwa kuweka masharti kwamba, mnufaika wa mafao ambaye kwa kipindi husika anatumikia kifungo anaweza kuridhia kwa maandishi kwamba mafao yake au sehemu yoyote ya mafao yake ilipwe kwa mnufaika atakayetajwa.

“Lengo la marekebisho haya ni kuimarisha ushiriki wa mtu anayetumikia kifungo katika utoaji wa mafao yake kwa mnufaika,” amesema.

Kifungu cha 23 kimefutwa na kuandikwa upya kuruhusu michango iliyowekwa na mwanachama baada ya umri wa kustaafu hadi kufikia miaka 70 kuzingatiwa katika ukokotoaji wa malipo ya mafao ya pensheni.

“Lengo la marekebisho haya ni kuongeza wigo wa upatikanaji wa mafao ya pensheni kwa mwanachama ambaye amefikisha umri wa kustaafu lakini hajakidhi vigezo vya kupata pensheni na amekuwa akichangia kuanzia umri wa miaka 61 mpaka 70,” amesema.

Ridhiwani amesema marekebisho mengine yaliyofanywa ni kuruhusu vyama vya wafanyakazi au mtu mwingine yeyote, kuwawakilisha waajiriwa katika madai ya fidia katika mfuko.

Amesema marekebisho hayo yanaelnga kuzuia mgongano wa masilahi kwa kuwa maofisa kazi na wakaguzi  wa Mamlaka ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi ni sehemu ya watu wanaotekeleza sheria hiyo.

Amesema marekebisho mengine yanahusu kifungu cha 48(6) ili kumwezesha mwajiriwa ambaye amepata ulemavu wa kudumu, kuendelea kupokea pensheni hata baada ya kurejea kazini au kupokea mafao ya uzeeni.

“Lengo la marekebisho haya ni kuweka usawa kati ya wanufaika ambao wanapokea mafao kwa mkupuo na wanaopokea pensheni,” amesema.

Amesema suala la ukomo wa muda katika kudai mafao limeondolewa kwa kufuta kifungu cha 48, hivyo mnufaika anaweza kudai mafao pasipo na ukomo wa muda.

Ridhiwani amesema muswada umeongeza kifungu kipya cha 11A kuwezesha watu waliojiajiri katika sekta binafsi kujiunga na kufaidika na mafao ya hifadhi ya jamii katika mpango wa uchangiaji kwa mujibu wa sheria na kwamba, lengo ni kuongeza wigo wa hifadhi ya jamii kwa watu waliojiajiri.

Amesema muswada umerekebisha kifungu cha 15 kwa kuweka wajibu kwa mkurugenzi mkuu kuhakikisha hesabu ya kiwango chote imewekwa kwenye mfuko wa hifadhi ya jamii hata kama kiwango hicho kilikatwa na mwajiri na hakikuwasilishwa katika mfuko wa hifadhi ya jamii.

Amesema lengo la marekebisho hayo ni kulinda masilahi ya wanufaika wa mafao ya mfuko wa hifadhi ya jamii.

Amesema kifungu cha 12(1) kimerekebishwa kuainisha asilimia za kiwango cha uchangiaji kinachopaswa kuwasilishwa na mwajiri kwenye mfuko.

“Kifungu cha 12(3) kinapendekezwa kufutwa ili kuruhusu mwajiri kuchangia kwa kiasi kikubwa au kiasi chote. Kifungu cha 12(5) kinapendekezwa kurekebishwa kuainisha namna ya uchangiaji kwa wanachama waliojiajiri,” amesema.

Amesema marekebisho mengine ni kufutwa kifungu cha 58(2) ili kutojumuisha motisha katika mshahara unaotumika kwenye ukokotoaji wa fidia ili kuweka usawa kwa wanufaika katika malipo ya fidia.

Related Posts