NFRA kununua tani 100,000 za mahindi Rukwa

Rukwa. Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) anatarajia kununua tani 100,000 za mahindi kwa wakulima mkoani Rukwa kupitia mfumo maalumu wa kidigitali.

Sambamba na mkakati huo, NFRA imehamasisha wakulima wadogo na wafanyabiashara kuuza mazao katika vituo mbalimbali vilivyopo kila wilaya na kuepukana na matapeli.

Hatua hiyo imekuja baada ya Serikali kuja na mfumo rasmi wa mkulima akipima mahindi anapata malipo kwa wakati katika kituo husika.

Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Agosti 29, 2024 kuhusiana na hatua  ya  malipo ya  awali ya wakulima waliyokuwa yakilalamikia, Meneja wa NFRA Mkoa wa Rukwa, Marwa Range  amewatoa hofu wakulima kuwa hakuna atakayedhulumiwa.

Marwa amesema Serikali imekuja na mfumo mpya ambao mkulima atauza nafaka kwenye kituo chake na atalipwa malipo yake katika kituo husika.

Amesema katika vituo vyao, wanatumia mizani ya kidigitali kupima uzito wakati wa kununua nafaka kwa wakulima mkoani humo.

“Wakulima wadogo wasisite kuleta nafaka zikiwa safi maana tumepanga kununua mahindi meupe katika msimu huu wa ununuzi,” amesema.

Amesema kwa sasa Serikali imekuja na utaratibu mpya ambapo kila kituo kitakuwa kinafanya malipo baada ya kununua mazao hayo.

Meneja huyo ametaja vituo vya ununuzi wa mazao kuwa ni Mazwi, Kanondo na Laela huku Wilaya ya Kalambo vikiwa ni Matai na Mkombo na Nkasi ni Namanyere, Mtenga Kasu na Ntalamila.

Amesema NFRA kwa Kanda ya Sumbawanga inatarajia kununua tani 100,000 za mahindi sambamba na tani 15 za mpunga kwa kutumia mfumo mpya wa kidijitali lengo ni kuongeza ufanisi wa manunuzi ya mahindi.

Mkulima kutoka Wilaya ya Sumbawanga Vijijini, Martine Nakuja amesema kwa sasa wamekuwa wakipeleka mazao yao kwenye vituo na kulipwa kwa wakati tofauti na hapo awali.

“NFRA wamekuja na mfumo mzuri wa kupima mahindi kwa mizani ya kidijitali na tunalipwa kwa wakati, hivyo ni ngumu mkulima kuibiwa,” amesema mkulima huyo.

Related Posts