LIGI Kuu Bara itasimama kwa wiki mbili kupisha mechi za timu za taifa na mashindano ya klabu barani Afrika, huku Pamba Jiji ikipanga kuzitumia siku takribani 22 za mapumziko hayo kuboresha kikosi chake na kucheza mechi za kirafiki.
Pamba Jiji ambayo ilicheza mechi yake ya mwisho Agosti 24, mwaka huu itarejea tena dimbani Septemba 15 kuvaana na Singida Black Stars katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, katika mbili za Ligi Kuu timu hiyo imeambulia suluhu dhidi ya Dodoma Jiji na Tanzania Prisons.
Akizungumzia mipango ya timu hiyo katika kipindi hicho cha mapumziko, Meneja wa Pamba Jiji, Ezekiel Nyangoma, alisema kikosi kitaendelea kujifua vikali kwa kuboresha mapungufu, kutengeneza muunganiko na kucheza mechi za kirafiki dhidi ya Geita Gold na Stand United.
“Tutaendelea kufanya mazoezi kuboresha timu na katika kipindi hiki tutacheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Geita Gold na Stand United, tumepanga mchezo mmoja tucheze hapa nyumbani na mwingine tutoke, lengo ni kuendelea kuona timu iko sawa na maendeleo ya wachezaji,” alisema Nyangoma
Mwenyekiti wa klabu hiyo, Bhiku Kotecha alisema uongozi unaendeleza utamaduni wa kutoa motisha ya fedha kwa timu kama ilivyokuwa Championship, isipokuwa kwa sasa wanaweka kwenye akaunti za benki za wachezaji badala ya kuwapa mikononi baada ya mchezo kukamilika.
Msimu uliopita kwenye Ligi ya Championship katika harakati za kupanda daraja, uongozi wa Pamba Jiji ulikuwa unatoa wastani wa Sh5 milioni mpaka Sh10 milioni za motisha kwa wachezaji wakipata ushindi, ambapo zilikuwa zinakabidhiwa uwanjani baada ya mechi.
“Motisha ipo ukitaka nitakupa orodha uone nani kaingiziwa nani bado, tumejipanga kisasa hatuwapi mkononi wakifanya vizuri wanaingiziwa kwenye akaunti matumizi ya hela yanakuwa mazuri kuliko kukaa na hela mkononi,”
“Lakini bonasi ipo hata wakitoka droo wanapata, kwa undani zaidi tutaeleza baadaye lakini unielewe nikisema kwamba kila kitu kipo wala hakuna shida na mishahara yao wanapata kwa wakati hakuna mtu anadai,” alisema Kotecha.