TIMU ya mpira ya kikapu ya Savio imetikiswa na Vijana ‘City Bulls’ baada ya kufungwa pointi 77-65 katika Ligi ya mchezo huo Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Donbosco Oysterbay.
Savio inayoshika nafasi ya tatu ndani ya msimamo wa Ligi hiyo ikiwa pointi 45 katika mchezo huo ilishindwa kabisa kuonyesha makali mbele ya wapinzani wao hao.
Kutoonyesha kiwango kizuri kwa wachezaji wa Savio, ilichangia kwa kiasi kikubwa kwa nyota wa timu hiyo, Oscar Mwituka, Cornelius Mgaza na Sylivian Yunzu washindwe kufunga pointi pale walipopata nafasi, huku wenzao wa Vijana,Alfan Mustafa, Fotius Ngaiza, Victor Michael na Momba wakiupiga mwingi muda wote.
Wakati Savio ikipoteza mchezo huo, dada zao DB Lioness pia walipoteza mchezo wao kwa kufungwa na Vijana Queens kwa pointi 48-43.
Katika mchezo huo Vijana Queens, ilianza katika robo ya kwanza kuongoza kwa pointi 14-8, 12-14, 10-9 na 12-11.
Noela Renatus wa timu ya Vijana Queens aliweza kufunga pointi 13, akifutiwa na Frida Zablon aliyefunga pointi 10.
Kwa upande DB Lioness alikuwa Taudencia Katumbi aliyefunga pointi 18, akifuatiwa na Lavendes aliyefunga pointi 11.