Serikali, kina ‘Boni Yai’ wavutana kuahirisha kesi

Dar es Salaam. Kesi ya Meya wa zamani wa Ubungo jijijlni Dar es Salaam, Boniface Jacob maarufu Boni Yai na mwenzake, mwanaharakati Godlisten Malisa, iliyokuwa imepangwa kuanza kusikilizwa ushahidi leo imekwama baada ya shahidi aliyetarajiwa kudaiwa kuugua ghafla.

Mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Job Mrema ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Dar es Salaam, Kisutu leo Agosti 29, 2024 kuwa shahidi pekee aliyekuwa amefika mahakamani kwa ajili kutoa ushahidi amejisikia vibaya kabla ya kesi kuitwa na akaomba kwenda kuangalia afya yake.

Hivyo, Wakili Mrema akisaidiana na wakili wa Serikali Asiatu Mzamiru, wameiomba mahakama hiyo itoe ahirisho mpaka tarehe nyingine itakayopangwa.

“Kutokana sababu hiyo ndio maana tunaomba ahirisho na sababu hiyo iko nje ya uwezo wetu,” amesema Wakili Mrema.

Hata hivyo, mawakili wa utetezi wanaowawakilisha washtakiwa hao, Peter Kibatala akishirikiana na Hekima Mwasipu na Deogratius Mahinyila hawakufurahishwa na ombi hilo, hivyo wakaomba mahakama tarehe nyingine Jamhuri wakikosa shahidi basi mahakama itumie mamlaka yake kuifuata kesi hiyo.

“Kwanza hawajamtaja hata jina na wakati tuliambiwa wana mashahidi wengi. Kwa hiyo mheshimiwa tunaomba leo urekodi kuwa ni ahirisho la mwisho,” amesema Kibatala na kuongeza:

“Kwa hiyo tutakapokuja tena kama hawatakuwa na shahidi basi utumie mamlaka yako (kisheria) kesi iweze kuondolewa”.

Hata hivyo, Wakili Mrema ameiomba mahakama hiyo ipuuze hoja ya kwamba Jamhuri haikuonesha kujali akidai kuwa Jamhuri imefanya kila namna shahidi kupatikana na kufika mahakamani kutoa ushahidi kama amri ya mahakama ilivyoelekeza.

“Suala la kutokutaja majina ya shahidi hatuoni kama limeathiri haki ya upande wa pili. Kwa hiyo hilo pia tunaomba ulipuuuze. Ukweli ni kwamba shahidi huyo amefika mahakamani asubuhi. Suala la ugonjwa ni la kibinadamu hatuna control (udhibiti) nalo,” amesema Mrema.

Akitoa uamuzi baada ya hoja hizo, Hakimu Swallow amesema amekubaliana na hoja ya upande wa mashtaka na sababu za kuomba ahirisho hilo.

“Kwa kuwa mmasema shahidi alikuwepo akapata dharura ya ugonjwa na ni kwa mara ya kwanza ninapata hiyo sababu naona ni sababu tosha ya kuahirisha kesi hii. Kwa hiyo ninatoa ahirisho mpaka Oktoba 3, 2024.

“Lakini bado mlikuwa na wajibu wa kuleta mashahidi wengi na kama hakutakuwa shahidi Oktoba 3 mahakama itaoma amri itakayofaa kwa wakati huo,” amesema.

Jacob, maarufu kama Boni Yai, mkazi wa  Mbezi Msakuzi, Dar es Salaam, mfanyabiashara na mwanasiasa ambaye aliwahi kuwa meya wa Manispaa ya Ubungo na Malisa, mkazi wa Moshi, mkoani Kilimanjaro, wote kwa pamoja  wanakabiliwa na mashtaka matatu ya uchochezi.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 11805/2024, inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu Ushindi Swallo, wanadaiwa kuchapisha taarifa za uwongo katika mitandao ya kijamii, kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka wanadaiwa kutoa taarifa za uchochezi kuwa Jeshi la Polisi linaua raia, wakilihusisha na kifo cha mwananchi mmoja, Robert Mushi, maarufu kama Baba G na mkazi na aliyekuwa dereva wa magari ya watalii, Arusha, Omari Msamo.

Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani hapo kwa mara ya kwanza Mei 6, 2024 na kusomewa jumla ya mashtaka matatu, mawili kati ya hayo yanamkabili Jacob pekee yake na Malisa anakabiliwa na shtaka moja.

Shtaka la kwanza linalomkabili Jacob pekee ni la kuchapisha taarifa za uwongo kinyume na sheria, akidaiwa kutenda kosa hilo Aprili 22, 2024 jijiini Dar es Salaam.

Anadai kuwa huku akijua na kwa nia ovu ya kuipotosha jamii, alichapisha taarifa katika mfumo wa kompyuta kupitia mtandao wake wa Kijamii X (Twitter) wenye jina la Boniface Jacob @ExMayor Ubungo, inayolihusisha Jeshi la Polisi kuhusika na mauaji ya Baba G.

Shtaka la pili, ambalo pia linamkabili Jacob pia ni la kuchapisha taarifa za uongo, akidaiwa kutenda kosa hilo Machi 19, 2024 katika jiji la Dar es Salaam.

Anadaiwa kuwa kwa nia ovu ya kuupitosha umma, alichapisha taarifa katika mfumo wa kompyuta kupitia mtandao wake wa Kijamii X (Twitter) wenye jina la Boniface Jacob @ExMayor Ubungo.

Katika shtaka Hilo anadaiwa kuandika ujumbe unaolihusisha Jeshi la Polisi na mauaji ya aliyekuwa dereva wa magari ya watalii, Omari Msamo ameuawa na askari wa Jeshi la Polisi wilaya ya Karatu mkoani Arusha.

Shtaka la tatu ambalo pia ni la kutoa taarifa za uongo, linamkabili Malisa pekee yake, akidaiwa kutenda kosa hilo Aprili 22, 2024 katika jiji la Dar es Salaam.

Related Posts