Simba yawashtukia Al Ahli yatega mitego mitatu

SIMBA wajanja. Tayari viongozi wa timu hiyo wamekaa kikao na kuamua ni namna gani wataicheza mechi ya mkondo wa kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika ugenini Libya dhidi ya Al Ahli Tripoli na sasa wametega mitego mitatu wanayoamini ikifanikiwa basi wana uhakika wa kushinda ugenini jijini Tripoli.

Simba na Tripoli zitakutana Septemba 13 mwaka huu katika mechi ya awali itakayochezwa Libya na ile ya marudiano inatarajiwa kupigwa Septemba 20 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Wekundu wa Msimbazi wanaamini hazitakuwa mechi nyepesi kutokana na ubora wa sasa wa Tripoli iliyoitoa Uhamiaji Zanzibar katika mechi za awali kwa jumla ya mabao 5-1, hivyo imeandaa mikakati mitatu ambayo itatumika kuhakikisha Mnyama anashinda mechi zote mbili na kutinga makundi kwa kishindo.

Mkakati wa kwanza ambao Simba imeupanga ni kupata mechi mbili za kirafiki zitakazokuwa na ushindani kabla ya kwenda kuwavaa Walibya.

Ikumbukwe Simba mara ya mwisho ilicheza mechi ya Ligi Kuu, Jumapili iliyopita dhidi ya Fountain Gate na kushinda 4-0 kisha kuwapa mapumziko wachezaji, kabla ya mapumziko hayo mafupi kufutwa na vigogo wakitakiwa kambini kujiandaa na mchezo wa Jumamosi hii dhidi ya Al Hilal ya Sudan. 

“Tunahitaji mechi za kirafiki zenye ushindani kabla ya kwenda Libya. Kocha anataka kuona maendeleo ya kikosi chake kabla ya kuwavaa Tripoli hivyo tunatarajia kuwa na mechi mbili na mojawapo itachezwa Jumamosi dhidi ya Al Hilal,” alisema kiongozi huyo aliyegusia pia watacheza mechi nyingine kabla ya kuondoka, japo haijafahamika.

Karata ya pili ya Simba ni kutafuta namna ya kuwahi Libya, huku ikiweka mezani mpango wa kukodi ndege binafsi itakayowapeleka Libya na kuwarudisha nchini baada ya mechi.

Simba inafanyia kazi mpango huo kutokana na kutokuwapo kwa ndege inayofanya safari za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam hadi Libya.

“Tunataka tuwahi kufika huko, tunajua kuna njia kadhaa ikiwamo kupita Misri lakini tunaangalia uwezekano wa kukodi ndege binafsi ili kupunguza mzunguko na uchovu kwa wachezaji. Tukifanikiwa nitakujulisha,” aliongeza kiongozi huyo wa Simba.

Na karata ya tatu ambayo Simba imeipanga ili kuwamaliza Tripoli ugenini ni kutuma watu mapema nchini Libya ambao watafanya maandalizi yote ya mechi kabla ya timu kamili kutia timu katika taifa hilo.

“Pamoja na yote hayo, lazima kuna watu watatangulia huko. Huu umekuwa mpango wetu wa mara kwa mara tunaposhiriki mashindano ya CAF. Siwezi kusema ni lini lakini wawakilishi wetu watakuwa Libya siku nne hadi tano kabla ya mchezo,” alisema.

Ofisa habari wa Simba, Ahmed Ally alisema mipango ya mechi hiyo ya ugenini inaendelea na taarifa rasmi ya timu inaondoka lini itatolewa na klabu.

“Tunajua mchezo unaofuata ni dhidi ya Tripoli, tunaendelea na maandalizi. Kuhusu safari itakuwa lini na tutaendaje, tutatoa taarifa rasmi siku chache zijazo,” alisema Ahmed.

Simba na Tripoli zote zimemaliza katika nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu za mataifa yao.

Related Posts