Mbeya. Kasi ndogo utekelezaji wa ujenzi wa mradi barabara njia nne yenye urefu wa kilometa 29 kutoka Uyole hadi eneo la Songwe Wilaya ya Mbeya mkoani hapa, imeibua maswali kwa wananchi na kuwatia hofu kwamba huenda usikamilike kwa wakati uliopangwa.
Wananchi wamepaza sauti zao baada ya kushuhudia kuondolewa kwa magari na vifaa vya ujenzi vya mkandarasi, Kampuni ya China Henan International Cooperation Group Co.Ltd (CHICO), anayetekeleza ujenzi huo kwa takribani mwezi mmoja sasa, jambo lililowatia hofu.
Wakati wananchi wakihoji hayo, Wakala wa Barabara (Tanroads) Mkoa wa Mbeya amewatoa hofu, huku akitaja sababu ya kusimama kwa mradi huo kuwa ni shughuli ya kutoa miundombinu iliyo chini ya ardhi ikiwepo ya maji na nyaya za TTCL.
Hata hivyo, chanzo cha ndani kutoka kampuni ya mkandarasi kimebainisha kwamba Serikali haijawalipa fedha, hivyo wameamua kusitisha ujenzi huo kwa sababu hawana fedha za uendeshaji ikiwemo kulipa mishahara ya wafanyakazi.
Akizungumza na Mwananchi leo Agosti 29, 2024, ofisini kwake jijini Mbeya, Msimamizi Mkuu wa mradi huo ambaye ni Meneja wa Tanroads Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Matari Masige amesisitiza kuwa mradi huo unaendelea kutekelezwa na suala la kuondoa vifaa lisiwape hofu wananchi.
Mhandisi Masige amesema wakati mradi ukiendelea kutekelezwa, kuna maeneo mkandarasi anahamisha miundombinu mbalimbali iliopo ardhini huku akiwataka wananchi kuondoa hofu kwani mradi utakamilika kwa wakati.
“Kuna maeneo ni vigumu kumwaga kifusi juu ya miundombinu hususan ya maji, utaratibu ni kwamba lazima itolewe ili kuendelea na utekelezaji wa ujenzi wa mradi.
“Wananchi wasiwe na hofu, mradi utakamilika na kupunguza adha ya msongamano wa magari nyakati za asubuhi na jioni katika barabara kuu ya Tanzania na nchi jirani ya Zambia (Tanzam) ambayo imekuwa finyu kutokana na kutumiwa na idadi kubwa ya magari,” amesema.
Amesema lengo la serikali ya awamu ya sita ni kuhakikisha barabara hiyo inakamilika kwa wakati na kubainisha kuwa sasa mradi umefikia asilimia 16 ya utekelezaji na ifikapo mwaka 2025, ujenzi utakamilika na kuchochea shughuli za kiuchumi,” amesema.
Masige amesema ifikapo mwaka 2025, mradi huo ukikamilika utakuwa chachu ya kufungua fursa za kiuchumi kufuatia umuhimu wake wa kuunganisha mataifa mbalimbali nchini.
“Mradi huu ukikamilika utakuwa na tija kubwa kiuchumi na kupunguza msongamano wa magari kwani kutakuwa na barabara mbili kulia na kushoto hivyo hivyo na kuwezesha wamiliki wa vyombo vya moto kwenda mwendo wanaopenda,” amesema.
Wakati meneja huyo wa Tanroads akieleza hayo, chanzo chetu cha habari kutoka ndani ya kampuni ya mkandarasi, kimesema mradi huo umesimama kwa sababu Serikali imechelewa kulipa fedha hadi sasa ni robo tu ya fedha yote ya mradi ndiyo imelipwa tangu wameanza kazi na sasa mwaka mmoja na nusu umepita.
“Kwani tulianza utekelezaji wa mradi Machi 2023 na tulipaswa kukamilisha na kukabidhi serikalini Aprili 2025 na uwenda muda wa mradi ukaongezwa kwa sasa tunaelekea msimu wa mvua,” amesema.
Chanzo hicho kimebainisha kwamba awali kulikuwa na wafanyakazi 350 hadi kufika Julai 21, 2024, wamelazimika kuwapunguza 310 na kubakiwa na wafanyakazi 40 ambao ni waajiriwa wa kampuni hiyo kutokana na changamoto ya fedha za kuwalipa mishahara.
Awali akizungumza na Mwananchi, mkazi wa Ilomba jijini hapa, Amani Agustino amesema ujenzi wa barabara hiyo ni kama umesimama kwani hakuna kazi inayoendelea zaidi ya kupigwa vumbi.
“Kimsingi tunafika hatua ya kuhoji ni kuona ukimya wa utekelezaji wa mradi huu, tulizoea kuona magari, vifaa na vibarua wakipiga kazi lakini sasa hakuna kuko kimya,” amesema.
Mamalishe, Aneth John amesema kwa sasa wanapigwa vumbi asubuhi hadi jioni, ni vema Serikali ikaharakisha ujenzi wa barabara hiyo ili kuwasaidia kuwa sehemu salama.
Dereva bodaboda kijiwe cha Sabasaba, Meshack Daniel amesema kipande cha barabara kutoka darajani, eneo la Nanenane hadi Makasini kimekuwa finyu baada ya mkandarasi kukwetua maeneo ambayo zinajengwa barabara nne.
“Hilo eneo ni hatari sana, hata magari makubwa siyo rahisi kupishana na hakuna kituo cha abiria wala sehemu ya kujibanza, tukifika hapo kama kuna foleni tunamuomba Mungu atuvushe,” amesema.