Katika mazungumzo yao yaliofanyika kwenye Ukumbi wa Great Hall of the People, Xi alimwambia Sullivan kwamba China ina dhamiri ya kuwa na uhusiano tulivu na Marekani, na kusema katika dunia yenye misukosuko na inayobadilika haraka, nchi hizo zinahitaji kuwa na mshikamano na uratibu na wala sio utengano.
Xi amesema pia kuwa licha ya mabadiliko makubwa, China na Marekani zinaweza kufurahia ushirikiano mzuri.
Biden ajitolea kusimamia kwa uwajibikaji uhusiano kati ya China na Marekani
Sullivan amemwambia Xi kwamba Rais wake Joe Biden amejitolea kusimamia uhusiano huo ili kuepusha migogoro na kwamba rais huyo anatazamia kuwasiliana na Xi katika wiki zijazo.
Sullivan amesema RaisBiden amejitolea kusimamia kwa uwajibikaji uhusiano huo muhimu ili kuhakikisha kuwa ushindani hauchangii migogoro au makabiliano, na kufanya kazi kwa pamoja katika maeneo ambayo maslahi yanalingana.
Soma pia:Jake Sullivan akutana na Wang Yi mjini Beijing, China
Baada ya mkutano huo, Ikulu ya White House ya Marekani ilisema pande hiyo mbili zinapanga mawasiliano kwa njia ya simu kati ya Xi na Biden hivi karibuni.
Katika kile alichoeleza kuwa masaa 14 ya mazungumzo, Sullivan aliangazia masuala mbalimbali yanayotatiza mahusiano kati ya nchi hiyo mbili.
Masuala ya mvutano kati ya China na Marekani
Masuala hayo ni pamoja na mvutano juu ya Taiwan, Bahari ya China Kusini na Urusi pamoja na matakwa ya Marekani kwa China kusaidia zaidi katika kukabiliana na mtiririko wa viungo vya fentanyl, ambayo ndiyo chanzo kikuu cha matumizi ya kupitiliza ya madawa ya kulevya nchini Marekani.
Soma pia:Mshauri wa masuala ya usalama wa Marekani Jake Sullivan anaitembelea China
Lakini tofauti kubwa zinasalia kuhusu baadhi ya mambo, ambapo Sullivan amesema hawajafikia makubaliano mapya kuhusu Bahari ya China Kusini na pia kwamba walikuwa na mjadala mkali kuhusu masuala ya usalama wa kiuchumi na biashara.
Mshauri huyo wa Rais wa Marekani amesema pia kwamba hawakugusia uchaguzi wa Marekani katika mazungumzo yao.
Sullivan akutana na viongozi wengine wa China
Kabla ya kukutana na Xi, Sullivan alikuwa na mazungumzo yasiokuwa ya kawaida na jenerali mmoja anayezingatiwa na wanadiplomasia kuwa mshauri mkuu wa kijeshi wa rais, Zhang Youxia, makamu mwenyekiti wa Kamandi Kuu ya jeshi la China. Pia alikuwa na mazungumzo ya kina na waziri wa mambo ya nje wa China, Wang Yi, siku ya Jumanne na Jumatano.