KITENDO cha nyota wa Tanzania Prisons, Jeremiah Juma na Samson Mbangula kurejea kikosini, kumemfanya Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mbwana Makatta kupata hali ya kujiamini akisema kwa sasa kazi inaanza upya katika Ligi Kuu Bara.
Prisons imeanza kwa ugumu Ligi Kuu baada ya kucheza michezo miwili bila kufunga bao, wakiambulia matokeo ya 0-0 mfululizo dhidi ya Pamba Jiji na Mashujaa zote wakicheza ugenini.
Katika mechi hizo, maafande hao waliwakosa baadhi ya nyota wake wakongwe akiwamo Mbangula, Jeremiah Juma na nahodha Jumanne Elfadhil.
Makatta alisema katika mechi mbili hajaridhishwa na matokeo licha ya kwamba hawakupoteza mchezo wowote lakini kutofunga mabao imemuumiza akili.
Kocha huyo aliyerejea katika timu hiyo baada ya kuipandisha daraja Pamba Jiji, alisema baada ya mechi hizo kwa sasa wanaendelea na mazoezi kwa ajili ya mchezo ujao dhidi ya Tabora United, Septemba 14 ugenini, ambapo Mbangula, Jeremiah na Elfadhil wanatarajiwa kuliamsha kwa mara ya kwanza.
“Sehemu ya beki wamefanya vizuri kwakuwa hawajaruhusu bao, tunachokomalia kwa sasa ni umaliziaji baada ya michezo iliyopita kutofunga mabao naamini kuanzia mchezo ujao furaha itaanza rasmi.
“Hatukuanza na wachezaji wazoefu kikosini ili kuwapa nafasi vijana ambao tumewaongeza, matokeo yake tumeyaona walifanya vizuri lakini wale waliokuwa na changamoto wamerejea,” alisema Makatta.
Kwa upande wa Elfadhil ambaye ni’ nahodha alisema kutokuwapo kwao haikuwa tatizo la moja kwa moja kwani lengo ni kutengeneza kikosi cha leo na baadaye kwani kuna muda wa kupumzika.
Alisema matokeo waliyoanza nayo si mabaya sana kutokana na kuanzia ugenini akikiri ligi kuanza kwa ushindani kwa kila timu kuhitaji ushindi ili kujiweka pazuri mapema.
“Tunaenda kujipanga upya na mechi ijayo, ligi imeanza kwa ugumu na si kwamba kutokuwapo kwetu ndio imekuwa hivyo moja kwa moja ila muda mwingine unawapa nafasi wengine na hawajafanya vibaya,” alisema mkongwe huyo.