WATU 6,597 miongoni mwao wakiwemo wajasiriamali 97 katika wilaya tano za Karatu, Ngorongoro- Loliondo, Monduli, Longido na Arusha DC wamepatiwa elimu na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuhusiana na masuala mbalimbali yanayohusiana na viwango.
Elimu hiyo ilianza kutolewa na maofisa wa TBS katika wilaya hizo za Mikoa ya Arusha na Manyara kuanzia Agosti 16 na itahitimishwa Agosti 29, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusiana na kampeni hiyo, Meneja Uhusiano na Masoko wa TBS, Gladness Kaseka, alisema elimu hiyo inatolewa kwa wananchi kupitia maeneo ya wazi, ikiwemo minadani , stendi, sokoni na maeneo mengine yenye mikusanyiko ambapo watu wengi wamejitokeza kwa wingi kupata elimu hiyo.
Kwa mujibu wa Kaseka kampeni hiyo ina lengo la kuelimisha wananchi kuhusiana na umuhimu wa kutumia bidhaa zilizothibitishwa ubora, jinsi ya kutoa taarifa za bidhaa hafifu pamoja na zile ambazo hazijaisha muda wake wa matumizi.
Alihimiza wananchi kabla ya kununua bidhaa wahakikishe wanasoma kwa umakini taarifa zilizopo kwenye vifungashio ili kujiridhisha kama bidhaa hizo zimethibitishwa ubora na kama hazijaisha muda wake wa matumizi pamoja na taarifa zingine za msingi.
Kwa mujibu wa Kaseka TBS imeamua kufikisha elimu hiyo kwa wananchi kwa kutambua kuwa vita ya bidhaa hafifu sio ya Shirika hilo peke yake, bali ni ya Watanzania wote.
Aidha, alitaka wananchi waache kununua bidhaa kwa mazoea na badala yake waangalie muda wake wa mwisho wa matumizi na pindi wakikutana na bidhaa ambazo hazina ubora, au zimeisha muda wake wa matumizi au kutilia mashaka bidhaa yoyote wasisite kuwasiliana na TBS kupitia namba ya bure ya kituo cha huduma kwa wateja.
Aidha, Kaseka alisema kupitia kampeni hiyo waliweza kutoa elimu kwa wajasiriamali kuhusiana na taratibu za kufuata ili kuthibitisha ubora wa bidhaa zao wanazozalisha kabla ya kuzipeleka sokoni.
Kwa mujibu wa Kaseka Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, inatambua mchango wa wajasiriamali katika kukuza uchumi, ndiyo maana imebeba jukumu la kugharamia gharama zote za wajasiriamali kuthibitisha ubora wa bidhaa zao bure.
Alitoa wito kwa wajasiriamali hao kuchangamkia fursa hiyo ambapo wakishafika TBS na barua ya utambulisho kutoka SIDO mchakato wa kuthibitisha ubora bidhaa zao bure unaanza mara moja.
Aliwaambia wajasiriamali hao kwamba ili waweze kuimihili soko la ushindani ndani na nje ya nchi ni lazima bidhaa zao ziwe zimethibitishwa ubora na kupata alama ya ubora ya shirika hilo.
Alifafanua kuwa bidhaa ikishakuwa na alama ya ubora inampa uhakika mlaji kwamba bidhaa husika ni salama na inavuka mipaka ya Tanzania na kwenda kuuzwa nje bila vikwazo vyovyote.
“Kwa hiyo tumeamua kuwafikia wajasiriamali na wananchi katika ngazi za wilaya ili kuwapatia utaratibu unaotakiwa kwa ajili ya kupata alama ya ubora ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza,” alisema Kaseka.
Hadi sasa TBS imetoa elimu hiyo katika wilaya zipatazo 97 nchi nzima na kwa mujibu wa Kaseka kampeni hiyo ya kutoa elimu itakuwa endelevu.