Unayoweza kufanya kukamilisha ujenzi wa nyumba chapuchapu

Dar es Salaam. Ili kukamilisha ujenzi wa nyumba kwa wakati, Watanzania wametakiwa kubadilika na kuanza kuchangamkia fursa za mikopo ya nyumba.

Mbali ya ujenzi, pia wametakiwa kutumia mikopo kununua nyumba.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya First Housing, Amulike Kamwela amesema mikopo itawawezesha kumaliza ujenzi wa nyumba kwa wakati badala ya kujenga kidogo-kidogo na kwa muda mrefu. Amesema ujenzi wa aina hiyo huzidisha gharama.

Kamwela amesema hayo hivi karibuni alipozungumzia utendaji wa First Housing ambayo takwimu zinaonyesha imeshika nafasi ya tano kati ya taasisi 31 za fedha zizonatoa huduma za mikopo ya nyumba.

Amesema kupitia mikopo ya nyumba za makazi kutoka taasisi hiyo, mwananchi anakuwa na uhakika wa kumaliza ujenzi kwa wakati.

“Tukiwa na malengo ya kuwa vinara katika sekta hii ya mikopo ya nyumba za makazi nchini, First Housing itaendelea kuwekeza kwenye teknolojia kuboresha utoaji huduma kwa wakati,” amesema.

Kamwela amesema taasisi hiyo itaongeza ujuzi kwa watendaji wake waweze kuendana na mabadiliko yanayotokea kila siku kwenye sekta ya nyumba.

“Kwa mujibu wa taarifa za fedha za Juni, 2024 Taasisi ya First Housing imeshatoa mikopo ya nyumba yenye thamani ya Sh31.3 bilioni ambayo ni ongezeko ikilinganisha na Sh22.8 bilioni iliyokuwapo kipindi kama hicho mwaka jana,” amesema.

Taasisi hiyo ilianzishwa Tanzania mwaka 2017, ikiwa na lengo maalumu la kuwawezesha Watanzania wa kipato cha chini na kati kumiliki nyumba za makazi kupitia mikopo ya nyumba yenye gharama nafuu na ya muda mrefu.

“Tumefurahishwa na matokeo haya kwani yanaonyesha matunda ya jitihada zetu za kusaidia Watanzania kutimiza ndoto zao za kumiliki nyumba,” amesema.

Kamwela amesema, “Siyo tu kwamba jitihada zetu zinawawezesha Watanzania kumiliki nyumba bali pia zinaendana na malengo ya dira ya maendeleo ya Tanzania, hasa katika kuboresha hali ya maisha na kupunguza umasikini kwa watu wote.”

Related Posts